WASANII wa sinema wanaounda Kundi la Bongo Muvi, wamemshutumu Rais wa
Shirikisho la Filamu Tanzania, Simon Mwakifwamba kwamba amewaingiza
chaka katika uteuzi wa mjumbe anayewawakilisha katika Bunge la Katiba
lililoanza juzi mjini Dodoma.
Wakizungumza katika kikao cha dharura kilichoitishwa ghafla Jumatatu
iliyopita kwenye viwanja vya Leaders, Kinondoni, jijini Dar, wasanii
tofauti wa burudani waliungana na kuweka mikakati ya kuhakikisha
wanapata wawakilishi wengine watakaoweza kuwatetea kikamilifu.
“Sisi hatuelewi kwa nini Mwakifwamba ametuchezea mchezo, alitakiwa
kutuita na kutuambia kuwa kuna kitu kama hicho, lakini alipeleka majina
yake kumi na mwisho wa siku amechaguliwa Paul Mtenda mtu ambaye tuna
uhakika hana uwezo wa kuongea na kutusaidia kwa lolote huko bungeni,”
alisema mmoja wa wasanii hao akiungwa mkono na wenzake.
Wasanii hao wakiongozwa na Mwenyekiti wa Bongo Muvi, Steve Mengere
‘Steve Nyerere’ walisema watamuweka chini Mwakifwamba mara tu akirejea
kutoka Dodoma ili wamkemee.
“Hii imethibitisha kwenye tasnia tuna matatizo, alitakiwa
kutushirikisha wote lakini yeye amekaa na watu wake akaamua kuteua na
mwisho wa siku ndiyo wakampitisha Mtenda, sisi tumemkubali lakini
hatujafurahishwa na tabia ya Rais kwani ameweka wazi tofauti zetu,
tutahakikisha wanaingia watu wengine wenye nguvu,” alisema Steve
Nyerere.
Lakini akijibu shutuma hizo, Mwakifwamba alisema taasisi zote
zilituma maombi baada ya matangazo kutoka na kupelekwa kwa katibu wa
bunge. Aliwataja baadhi ya waliotuma kuwa ni yeye mwenyewe, Yvonne
Cherly ‘Monalisa’, Suzan Lewis ‘Natasha’, Mike Sangu, Deo Songa, Paul
Mtenda na Emmanuel Myamba ‘Pasta Muyamba’.
“Mimi naweza kuwaona kama hawana hoja huko hawakuwa wakipelekwa watu
maarufu, waliangalia CV na mpaka sasa sijajua ni vigezo gani
vinavyotumika lakini ninachofahamu kuna wizara inayohusika ambayo iko
chini ya Mhe. William Lukuvi na mchujo ulipita kwa watu wa intelijensia
kisha majina yote yakapelekwa kwa Rais yeye ndiye alipitisha majina
yake, hivyo kama wamepanga kuniweka chini mimi niko tayari na
nitawashinda kwa hoja kwa sababu kwanza wao si wanachama wa TAFF,”
alisema Mwakifwamba.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment