MIEZI tisa baada ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar
kumhukumu staa wa filambu za Bongo, Kajala Masanja kifungo cha miaka
mitatu jela au faini ya shilingi milioni 13 kwa kosa la utakatishaji
fedha na Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu kumlipia hivyo kuwa huru, hali
ya maisha ya msanii huyo imebadilika ghafla na sasa ameibuka katika
utajiri wenye maswali na majibu.
Chanzo makini kimeliambia gazeti hili kwamba, Kajala ambaye alitoka
mahabusu ya Segerea jijini Dar, Machi 25, 2013 akiwa hana mbele wala
nyuma kiasi cha kutia huruma, sasa anazikamata za kutosha kiasi cha watu
wake wa karibu kumshangaa.
MANUNUZI YAKE
Chanzo kimebainisha kuwa, Kajala
ameagiza kutoka China kontena lenye urefu wa futi 20 likiwa limesheheni
samani za ndani. Samani za ndani ni fenicha mbalimbali.
“Hivi mnajua kwamba Kajala yuko juu. Naweza kusema ni tajiri kwa
sasa, maisha yake ni poa. Hivi ninavyoongea kuna kontena la futi
arobaini linakuja Dar, ndani mna samani tu,” kilisema chanzo hicho.
AMWAGA MILIONI 90 KUTENGENEZA FILAMU
Katika hali
inayoendelea kutafsiriwa kuwa ni kuzidi kuonesha ukwasi alionao, msanii
huyo ameshatumia shilingi milioni 90 kwa ajili ya kutengeneza filamu
zake tatu, kila moja ikitumia bajeti ya milioni 30 za Kibongo.
Filamu ya Kajala ambayo iko njiani kutoka inaitwa Laana. Inadaiwa
mpango wake ni kutengeneza filamu 10 ambazo atakuwa akiziuza kwa nyodo.
Kama ni hivyo atatumia shilingi milioni 300 kwa filamu hizo kumi.
ATUMIA MILIONI 11 KUNUNUA VITO VYA THAMANI
Mbali
na kuvaa magauni na viatu vya bei mbaya, hivi karibu staa huyo alitua
Dar akitokea China ambapo alipigilia vito vya gharama ya maisha ya
familia nzima.
“Juzikati Kajala katoka China na cheni ya dhahabu kainunua dola za
Marekani elfu tatu, bangiri pia ya dhahabu ya dola elfu mbili na mia
tano na hereni za gold (dhahabu) za dola elfu moja mia tano,” kilisema
chanzo.
Kwa mahesabu ya sasa, kiasi hicho cha dola kikibadilishwa na shilingi
ya Tanzania, Kajala alitumia kama milioni 11 kununua vito hivyo tu.
ANAYEMPA JEURI ATAJWA
Inadaiwa mcheza filamu huyo
amekuwa akipata jeuri hiyo kutoka kwa mwanaume bilionea wa Ghana
aliyejulikana kwa jina moja la Safara ambaye walikutana nchini China.
Inadaiwa Safara anaishi Marekani lakini ndiye anayeshika tenda ya
kuinunulia serikali ya Ghana vitu mbalimbali.
MWISHO DESEMBA KUISHI NYUMBA YA KUPANGA
Habari
zikazidi kumiminika kwamba, Safara amemwambia Kajala mwisho Desemba
mwaka huu kuishi kwenye nyumba ya kupanga, mwakani mjengo wake utakuwa
umekamilika.
Hata hivyo, haijaelezwa kama ameshapata kiwanja cha kujengea au la!
Ingawa habari zinasema nyumba anayoishi sasa Kajala imeshalipiwa kodi ya
mwaka mmoja na tajiri huyo wa Ghana.
AMFADHILI WEMA
Ikazidi kudaiwa kuwa, katika ziara ya baadhi ya mastaa jijini Arusha
hivi karibuni wakiongozwa na Wema ambako kulikuwa na shoo ya muziki wa
Kizazi Kipya, Kajala alimsaidia Wema mambo mbalimbali zikiwemo pesa ili
kufanikisha shughuli hiyo iliyohitaji umakini wa hali ya juu.
“Mbali na fedha hizo, Kajala wa zamani si huyu wa sasa, ila
ninashomsifu bado anamheshimu sana Wema, anajua ndiye amechangia
mafanikio yake, kama siku zile asingetoa zile milioni kumi na tatu
Kajala angekuwa gerezani,” kilisema chanzo hicho.
ALIPOTOKA GEREZANI
Inadaiwa baada ya kutoka
Segerea, Kajala aliishi maisha ya kuwa na shida hata shilingi elfu kumi
ilimsumbua, Wema ndiye aliyekuwa akimbeba kwa vijisenti vya matumizi na
baadaye alimwajiri kwenye kampuni yake ya filamu ya Endless Fame kama
sekretari. Kampuni hiyo kwa sasa imesimama.
HUENDA CHINA KINYEMELA?
Baada ya kuona safari
zake zimezaa matunda na kuhisi watu wanafuatilia nyendo zake, likiwemo
gazeti hili, Kajala ambaye husafiri mara kwa mara, amekuwa akidai
anakwenda Zanzibar licha ya hati zake za kusafiria kuoneshwa zimegongwa
mihuri ya China na Dubai.
KAJALA SASA
Alipoulizwa kwa njia ya simu juzi
kuhusiana na ukwasi wake kwa sasa, Kajala alisema anachojua yeye anaishi
maisha ya kawaida, tafsiri kwamba amekuwa tajiri ghafla inafanywa na
watu wanaomuona.
“Mimi naishi kawaida tu, huo utajiri wanauona wao. Unajua haya ni
maisha, leo unakuwa hivi, kesho unakuwa vile ndicho ninachoweza
kukisema, siwezi kusimulia kila kitu,” alisema Kajala.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


No comments:
Post a Comment