WAFAHAMU SAMAKI AINA YA POMBOO ASILI YAKE NI NCHI KAVU? ,SOMA HAPA KUJUA ZAIDI


POMBOO ni mnyama wa baharini ambaye yupo kundi moja na samaki wengine kama vile nyangumi na porpoises.
Kuna kama aina 40 za pomboo ambao wamegawanyika katika makundi makubwa 17. Makundi haya yana pomboo wanaotofautiana sana kwa ukubwa.
Wapo ambao urefu wao ni wastani wa meta 1.2 au futi 4 huku wakiwa na uzito wa wastani wa kilo 40.
Hawa ni pomboo wenye umbo dogo sana wa kundi la Maui, lakini wapo wenye urefu unaofikia meta 9.5 au futi 30 na uzito wa tani kumi.
Pomboo hupatikana katika maeneo mengi duniani lakini mara nyingi hupenda kuishi katika maeneo yasiyo na kina kirefu cha maji.
Chakula kikubwa cha pomboo ni samaki. Familia ya pomboo jamii ya Delphinidae, ambao ndio wanaongoza kwa wingi duniani, iliibuka miaka michache iliyopita.
Asili ya kundi hili, kwa mujibu wa taarifa zilizopo, ni tangu miaka milioni kumi iliyopita katika kipindi cha Miocene.
Asili ya jina
Jila la Kiingereza la pomboo, dolphin, linatokana na neno la Kigiriki- delphís. Neno hili lina asili katika neno jingine, delphu, linalomaanisha tumbo la uzazi.
Kwa maana hiyo, wataalamu wanasema kuwa kuna uwezekano Wagiriki wa kale walimpatia samaki huyu jina kutokana na umbo lake wakilifananisha na tumbo la uzazi.
Jina hili lilibadilika badilika kulingana na jamii husika inayolitumia. Mathalani, likitafsiriwa kwa Kilatini, neno hili huitwa delphinus linalotokana na tafsiri ya Kirumi ya neno la Kigiriki likimaanisha delphinos.
Lakini baadaye likabadilika kutokana na mabadiliko ya lugha ya Kilatini na kuwa dolfinus ambalo katika Kifaransa cha kale lilikuwa daulphin.
Lakini zipo baadhi ya jamii ambazo hapo kale walimwita samaki huyu kama nguruwe na baharini. Jina hili nalo linatokana na umbo lake.
Hivi sasa jina dolphin linatumika kumaanisha samaki wote walio katika familia ya delphinidae. Hapa kunaweza kuwa na mchanganyiko kidogo kwa sababu familia hii inahusisha pia na baadhi ya jamii za nyangumi na samaki mwingine ajulikanaye kama orca.
Pia jina hili linatumika kutambulisha familia ya pomboo wa mtoni, yaani Platanistoidea, inayojumuisha pia familia ya Iniidae (pomboo anayepatikana katika Mto Amazon), Lipotidae (anayepatikana katika Mto Yangtze) na Platanistidae (anayepatikana katika mito ya Ganges na Indus).
Kwa ujumla, jina nyangumi linatumika kumaanisha samaki wa jamii hii ambao wana umbo kubwa sana wakati wale wengine wenye umbo dogo wakiwekwa katika kundi moja na pomboo. Hili hufanyika zaidi sana huko Marekani.
Jina dolphin hutumika zaidi kumaanisha bottlenose dolphin, ambalo ndilo kundi kubwa kabisa la pomboo na ambao wametawanyika katika maeneo mengi duniani.
Ingawa nyangumi mkubwa naye yupo katika familia ya delphinidae, kuna watu ambao humwesabia kama dolphin.
Ingawa majina ‘dolphin’ na ‘porpoise’ yanatumika kumaanisha aina moja ya samaki, lakini porpoises hawahesabiwi kuwa ni pomboo kwa sababu wana umbo tofauti na pomboo waliozoeleka.
Umbo hili ni kama vile kuwa na mdomo mfupi pamoja na meno yenye umbo kama la sepetu. Samaki hawa pia wana tabia tofauti na pomboo wanaojulikana zaidi.
Kwa mujibu wa mgawanyiko uliotengenezwa na wanasayansi, porpoises yupo katika kundi la familia ya Phocoenidae na wanaonekana kuwa na asili moja na delphinidae walio katika kundi dogo la odontocetes.
Kuzaliana
Mnamo mwaka 1933, pomboo watatu wa ajabu walionekana katika pwani ya Ireland. Walipochunguzwa walibainika kuwa ni pomboo waliozaliwa baada ya kujamiiana kwa jamii mbili tofauti za pomboo wajulikanao kama Risso na bottlenose dolphins. Baada ya kuona hivyo, wataalamu wakaanza kulifanyia utafiti suala hilo.
Jambo hilo likajirudia kwa pomboo wa jamii mbili tofauti waliokuwa wakifugwa pamoja nao wakazaa ndama. Katika utafiti huu, pomboo jamii ya bottlenose na rough-toothed dolphin walijamiiana na kuzaa.
Tangu hapo taarifa zimekusanywa za kutosha zinazoonyesha kuwa kuzaliana baina ya jamii tofauti za pomboo ni jambo la kawaida. Wengi wa pomboo ambao wanazaliwa kutokana na jamii mbili tofauti wanapatikana sana huko SeaWorld, California.
Jamii kubwa ya pomboo wanaotokana na kuzaliana kwa jamii mbili tofauti wanajulikana kama wolphin. Pomboo huyu anatokana na kujamiiana kwa killer whale na bottlenose.
Wolphin wawili hivi sasa wanaishi katika bustani ya Sea Life Park huko Hawaii; wa kwanza akizaliwa mwaka 1985 kutoka kwa baba ambaye ni nyangumi na mama ambaye ni bottlenose.
Pamoja na hawa wanaofugwa, lakini wolphins pia wamewahi kuonekana wakiishi katika bahari pamoja na pomboo wengine.
Asili
Pamoja na nyangumi na porpoises, pomboo wanatokana na wanyama walio katika kundi la Artiodactyl. Hapo kale wanyama hawa walikuwa wakiishi nchi kavu.
Wazazi wa pomboo wa hivi sasa walianza kuishi baharini miaka milioni 55 iliyopita katika kipindi cha Eocene epoch.
Pomboo wa kale, alipochunguzwa katika maabara wakati anapokuwa na mimba, kuna viungo vya miguu ya nyuma ambavyo huonekana wazi katika mifupa yao ndani ya mwili. Viungo hivi vina urefu wa takriban sentimeta 2.5 au inchi moja.
Hata pomboo wa hivi sasa, mwili wake una vichipuo vya mifupa katika eneo lake la kiuno (kwa ndani) vinavyoaminika kuwa ni mwendelezo wa lile umbo la miguu ya nyuma ambayo alikuwa nayo mnyama huyu wakati akiishi nchi kavu kabla hajahamishia maisha yake baharini miaka mingi iliyopita.
Oktoba 2006, pomboo jamii ya bottlenose alikamatwa huko Japan akionekana kuwa na umbo la ajabu kidogo.
Huyu alikuwa na viungo kama mapezi mafupi katika kila upande katika eneo lake la viungo vya uzazi.
Baadaye, wanasayansi walisema kuwa kuna uwezekano kuwa mapezi hayo ni mwendelezo wa ile mifupa ya ndani kwenye eneo la kiuno ambayo inasimama badala ya miguu ya nyuma ya pomboo wa kale.
Itaendelea.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger