Akizungumza kwa tabu akiwa kwenye Hospitali ya Burhani iliyopo maeneo ya Posta, Dar alikolazwa, Dk Cheni alisema kuwa aliugua kwa muda mrefu na alipokwenda hospitali aliambiwa ana malaria kisha akapewa dozi.
DOZI YA MALARIA
Alisema kuwa pamoja na kutumia dozi hiyo ya malaria, hali yake ilizidi kuwa mbaya ndipo ikabidi afanyiwe vipimo mbalimbali, akagundulika ana ugonjwa hatari wa Dengu.
Ukweli ugonjwa huu ni hatari sana jamani. Nimeugua kwa muda mrefu bila kujua ni kitu gani hadi ulipogundulika hivi karibuni, namshukuru Mungu kidogo naendelea vizuri na bado napatiwa matibabu hapa hospitali,” alisema staa huyo mkubwa wa filamu Bongo.
DRIPU KWA FUJO
Dk Cheni alilazwa hospitalini hapo Jumanne iliyopita ambapo alikuwa akiongezewa ‘dripu’ kwa fujo kutokana na kuwa na homa kali.

Dk. Cheni akizidi kupatiwa matibabu.
MASTAA HAWAKAUKI WODINIKufuatia hali hiyo watu mbalimbali wakiwemo mastaa wa Bongo walikuwa wakiingia na kutoka wodini, kila mmoja akitaka kumjulia hali.
Baadhi ya mastaa walioripotiwa kufika wodini hapo ni pamoja na mke wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Mrisho Kikwete, Mama Salma Kikwete, mastaa wenzake, William Mtitu, Elizabeth Michael ‘Lulu’, Steven Mengere ‘Steve Nyerere’, Salum Mchoma ‘Chiki’, Mrisho Zimbwe ‘Tito’ na wengine kibao.
MISS NAYE AKUMBWA
Wakati staa huyo akiendelea na matibabu, muda mfupi baadaye gazeti hili lilipokea taarifa nyingine ya aliyewahi kuwa Mshiriki wa Miss Tanzania na Miss East Afrika namba 2, 2008, Aneth John Mwakaguo kuwa naye amelazwa kwa gonjwa hilo.
Habari za uhakika zilieleza kwamba mrembo huyo alikimbizwa kwenye Hospitali ya Kairuki iliyopo Mikocheni, Dar ambapo alilazwa wodi namba 7 akiwa hoi.
Hadi gazeti hili linakwenda mitamboni bado afya ya mrembo huyo ilikuwa haijaimarika na madaktari walikuwa wakihaha kuokoa maisha yake.

Aliyewahi kuwa Mshiriki wa Miss Tanzania na Miss East Afrika namba 2, 2008, Aneth John Mwakaguo akiendelea na matibabu.
NI MASTAA WATATUMpaka sasa tayari mastaa watatu wamethibitika kupata ugonjwa huo unaotisha jijini Dar. Mastaa hao ni Ray C, Dk Cheni na Aneth John.
IDADI KAMILI
Hadi Alhamisi jioni, idadi ya waathirika wa Dengu ilikuwa imefikia watu 376 huku serikali ikitangaza hali ya hatari na kutafuta tiba ya ugonjwa huo kupitia Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii iliyopo chini ya Waziri Dk. Seif Rashid.
ELIMU YA DENGU
Homa ya Denge kama ilivyoelezwa hapo juu ni tishio. Virusi vya ugonjwa huo husabazwa na mbu aina ya Aedes ambaye yupo katika mgawanyiko wa jamii tisa; Aedes Australis, Aedes Albooictus, Aedes Aegypti, Aedes Contator, Aedes Cinereus, Aedes Ructcus, Aedes Polynesiensis, Aedes Scutellaris na Aedes Vexans.
Mbu wa kike aina ya Aedes anapomng’ata binadamu mwenye maambukizi ya Homa ya Dengu huanza kuathirika mwenyewe na baada ya siku 8-10 huathirika zaidi kiasi cha mate kubeba virusi vya homa hiyo.
KUONGEZEWA DAMU
Dengu pia husambazwa kwa njia ya kuongezewa damu au kupewa viungo vya mtu aliyeathirika.
WAKATI WA KUJIFUNGUA
Inawezekana kwa mama kumwambukiza mtoto wakati wa ujauzito au kwenye kujifungua.
MWINGILIANO WA DAMU
Yapo maambukizi ya mtu na mtu wakati wa kujamiiana au mwingiliano wa damu lakini kitaalam inafafanuliwa kwamba si kawaida hali hiyo kutokea.
DRIPU ZA MAJI
Ugonjwa huo unadhibitiwa kwa kumpa mgonjwa dawa ili kuzuia kutapika, maumivu ya mwili na kupewa dripu za maji lakini hakuna dawa maalum za tatizo hilo na mgonjwa akipona huweza kuugua tena.
PAKA SASA HAUNA TIBA
Ugonjwa huu mpaka sasa hauna tiba ya uhakika, kinachifanywa kwa wagonjwa wanaogudulika kuwa nao ni kutibiwa tu dalili ili usizidi kusambaa mwilini.
WALIOATHIRIKA
Taarifa kutoka kwa wataalamu wa afya zinasema kuwa, mpaka sasa takribani watu milioni 100 duniani kote wameambukizwa ugonjwa huo na wengine milioni 2 wamefariki dunia baada ya kuugua.
USHAURI
Watu wanashauriwa kufanya vipimo mara kwa mara hasa wanapohisi kuwa na malaria na siyo kumeza dawa za kutuliza maumivu au dozi ya malaria kwa mhusika anaweza kufa ghafla.
Imeandaliwa na Gladness Mallya, Imelda Mtema na Hamida Hassan
No comments:
Post a Comment