KANISA LAGEUZWA DAMPO


Kanisa la Nabii Josephat Gwajima la Kibaha, Pwani
Stori: Matsoni Msama, Kibaha
KANISA la Nabii Josephat Gwajima la Kibaha, Pwani limegeuzwa dampo baada ya takataka kutupwa nyuma ya kanisa hilo.
Sehemu ya nyuma ya kanisa hilo ikiwa na lundo la taka. 
Gazeti hili lilikwenda kanisani hapo na kukuta rundo la takataka nyuma ya kanisa hilo na eneo lote limetawaliwa na harufu kali hali iliyofanya baadhi ya watu wa Mtaa wa Kibondeni uliopo katika Kata ya Mkuza, lililopo kanisa hilo kuishi kwa shida.
Hali hiyo imemfanya mwenyekiti wa shirika lisilo la kiserikali liitwalo Community Development Agenda Countrywide (CDAC), Bumija Senkondo ambalo makao makuu yake yapo  mtaani hapo kumuandikia barua yenye Kumb.Na. BMS/HMK/US/01/14 ya Mei 7, mwaka huu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha akimpa siku 30 kuondoa takataka hizo la sivyo atashirikiana na waumini na wananchi wengine kumburuza mahakamani.
Senkondo katika barua hiyo amesema kitendo cha kugeuza jalala eneo hilo ni ukiukwaji wa kifungu cha 41(1) cha sheria ndogo za usafi wa mazingira za mwaka 2011 za Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kashfa kwa nyumba hiyo ya ibada kwani inafanya waumini washindwe kuabudu sawasawa.
“Nimeamua kuandika barua hii kutokana na kukiukwa kwa sheria hiyo kwa makusudi na watendaji wa Halmashauri ya Mji wa Kibaha na kusababisha kero kwa baadhi ya wakazi wa Mtaa wa Kibondeni na waumini wa kanisa,” imesema sehemu ya barua hiyo.
Mwenyekiti Bumija amesema wakati huu wa mvua, maji machafu yanatoka katika uchafu huo na kutiririka kwenda kwenye makazi ya watu lakini pia ni mazalia ya mbu, hivyo kuweza kuzaliwa mbu wanaosababisha ugonjwa wa dengue.
Gazeti hili lilifika ofisi ya mkurugenzi wa mji wa Kibaha lakini hakuna ofisa aliyekuwa tayari kuzungumzia suala hilo kwa madai kuwa mkurugenzi alikuwa nje ya ofisi kikazi.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger