MTU mmoja aliyefahamika kwa jina la Samson Ntemi
(44) mkazi wa Msingwi, Wilaya ya Magu mkoani Mwanza amenaswa na Polisi
wakati akifanya jaribio la utapeli wa madini feki huko Kijitonyama
jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Kwa mujibu wa chanzo makini, mtu huyo alianza harakati za utapeli
wake kwa kumpigia simu mfanyabiashara mmoja wa magari akimweleza kuhusu
nia yake ya kununua gari aina ya Canter kutoka kwake kwa kiasi cha
shilingi milioni 32.
Chanzo kilisema kufuatia simu mfululizo za mtu huyo, mfanyabiashara
huyo alipata hofu na kuhisi huenda alikuwa ni tapeli, hivyo kuweka mtego
na kumtaka wakutane Mwananyamala kwa ajili ya kufanya biashara hiyo.
Lakini hata hivyo, walipokutana tapeli huyo alimtaka mfanyabiashara
huyo kuongozana naye hadi Kurasini, akidai ndipo alipokuwa mteja mwenye
kulihitaji gari hilo.
“Nilishangaa jamaa akinibadilishia kauli akidai anayetaka gari ni bosi wake siyo yeye.
Nilipomhoji vizuri akaniambia yeye ni mfanyabiashara wa madini kutoka
Mahenge, Ifakara, mkoani Morogoro aliyefika Dar kutafuta soko huku
akionesha kutolijua vizuri Jiji la Dar,” chanzo chetu kilimnukuu
mfanyabiashara huyo akisema.
Inadaiwa kuwa tapeli huyo alimwonyesha mfanyabiashara huyo madini
hayo yenye thamani ya mamilioni ya shilingi na kumtaka anunue. Baada ya
kuyaona na kugundua kuwa ni feki, alimtaka tapeli huyo kuandamana naye
hadi benki maeneo ya Kijitonyama ili amkabidhi.
Wakiwa njiani, mfanyabiashara huyo aliwasiliana na Polisi wa Kituo
Kidogo cha Mabatini, Kijitonyama ambao walikuja eneo la tukio na
kumkamata tapeli huyo, aliyekiri mbele ya askari kuwa alishawahi kufanya
wizi huo katika miji ya Tarime, Arusha na Shinyanga.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment