HUU NDIO UNDANI POLISI ALIYEUAWA NA MAJAMBAZI

JUMANNE, Juni 10, mwaka huu majambazi yapatayo sita, yalivamia Kituo Kidogo cha Polisi Kimanzichana na kupora silaha na baadaye kumuua askari polisi mmoja, mgambo mmoja na kumjeruhi mwingine na kutoweka.
Marehemu Venance Mushi enzi za uhai wake.
Kwa mujibu wa mashuhuda, majambazi hayo yalifika katika kituo hicho majira ya saa saba usiku, yakiwa yanakokota bodaboda mbili huku wengine wakijifanya wanachechemea kuonyesha kuwa walipata ajali.
Mmoja wa waathirika wa tukio hilo, Mariam Ally, aliyelazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili, wodi namba mbili ndani ya jengo la Mwaisela ambaye ni mgambo, anasimulia jinsi mkasa huo ulivyotokea, baada ya Uwazi kumtembelea.
Mke wa marehemu akilia kwa uchungu na simanzi kubwa.
“Tukiwa kituoni hapo, ghafla tuliona watu wakikokota pikipiki mbili aina ya Boxer huku baadhi yao wakitembea kwa kuchechemea kama vile watu waliopata ajali.
“Hakuna mtu aliyefikiri kama kungekuwa na tukio la uvamizi, walipaki na kusogea kwa ajili ya kupata huduma,” alisema Mariam.

Alisema jambo la kwanza walilofanya ni kumvamia askari aliyekuwa na bunduki na kumpora kisha wakaelekea chumba cha kuhifadhia silaha na kuchukua SMG nyingine kabla ya kuanza kufyatua risasi hewani.
“Nilipoona hali imeshakuwa mbaya, nililala chini na kuanza kupiga simu   kuomba msaada, kumbe simu hiyo ilitoa mwanga hivyo  majambazi  yakanigeukia  na  kuanza  kunishambulia kwa  mapanga  na mateke hadi  nikazimia kutokana na kuvuja damu nyingi.
Mke wa marehemu akiaga mwili.
“Mimi ninachokijua pale  kituoni tulikuwa  na silaha mbili (bunduki mbili aina ya SMG) ambazo zilichukuliwa  na majambazi hao.”
Mtoto mkubwa wa askari mgambo, Venance Urio aliyefia hospitalini  aliyejitambulisha kwa jina la Tumaini alisema siku ya tukio alikuwa Gongo la Mboto.
“Sina la kufanya maana tegemeo langu limeondoka, ameniacha katika wakati  mgumu sana,” alisema wakati wa zoezi la kuaga mwili wa mzazi wake.
Ndugu jamaa na marafiki wakiuaga mwili wa marehemu.
Mke  wa  marehemu aliyejitambulisha kwa jina la Veneranda Urio alisema alifuatwa usiku wa manane na mwenyekiti wa  kijiji akiwa na baadhi ya majirani na kumtaka atoke nje, lakini alikataa kwa kuhofia usalama wake.
“Lakini baada ya kugongewa kwa muda mrefu nikaamua kufungua ndipo nilipoambiwa mwenzangu amevamiwa na majambazi, na kwamba wamempeleka hospitali, nikafanya hima kwenda Muhimbili nilikoambiwa amepelekwa na majeruhi mwenzake, nilimkuta kawekewa pamba kubwa tumboni, alikokuwa amepigwa risasi.
“Kauli ya mwisho ya mume wangu aliitoa baada ya kumshika mkono alisema usiniache tuondoke sote nyumbani.
Kamanda Matei (kushoto) akimjulia hali Mariam Ally katika Hospitali ya Taifa Muhimbili mwishoni mwa wiki baada ya kujeruhiwa na majambazi.
“Hata hivyo, muda wa kuona wagonjwa uliisha nikawa nimetoka kurudi nyumbani huko nyuma akaaga dunia.”
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Pwani,  SACP Ulrich Onesphory Matei alisema tukio hilo ni pigo kubwa na linafanyiwa kazi kwa kiwango cha juu kwani hadi hivi sasa watu 17 wanashikiliwa na uchunguzi unaendelea.
Mariam Ally akionyesha jeraha alilolipata baada ya tukio hilo.
“SMG mbili zilizokuwa kwa ajili ya ulinzi zimechukuliwa, makachero  wa  kutosha wamemwagwa, ni imani yangu wahusika watakamatwa.
“Ninawaomba wananchi kutoa ushirikiano ili tuweze kukomesha vitendo hivi viovu,” alisema kamanda huyo.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger