AMA kweli hujafa hujaumbika.
Msichana Jacqueline
Willson Aluma ambaye alikuwa mwanafunzi wa Shule ya Sekondari ya Dira
V, iliyopo jijini Dar es Salaam alizaliwa akiwa mzima na wala hakuwa na
tatizo lolote kimwili.
Lakini pasipo kujua lengo na sababu zao, watu wamekuwa wakimfuatilia
binti huyo mdogo mwenye umri wa miaka 18 sasa na kufanikiwa kumjeruhi na
kumpa ulemavu, kwani baada ya matibabu ya miezi mitano katika Hospitali
ya Taifa Muhimbili, ameishia kuwa mtu wa kulala na kutembea kwa tumbo.
Lakini katika hali ya kusikitisha, watu waliomjeruhi na kumpatia
ulemavu huo, walikamatwa na kushtakiwa mahakamani, ingawa kesi yao
imefutwa kwa kinachodaiwa kukosekana kwa ushahidi, lakini chombo hicho
cha haki kikimnyima nakala ya hukumu ili aweze kukata rufaa.
Mara ya kwanza, msichana huyo alikutana na wabaya wake hao Novemba
mwaka 2011 saa tisa alasiri akiwa Kituo cha Daladala cha Jeti, Uwanja wa
Ndege akisubiri usafiri wa kuelekea nyumbani kwao.
Ghafla teksi
moja ilisimama karibu yake na mmoja kati ya watu wanne waliokuwepo ndani
ya gari hilo, alimwambia aingie ili wampeleke nyumbani, akakataa.
“Watu wawili walishuka na kutaka kunikamata kwa nguvu ili waniingize
ndani ya gari, nikapiga kelele, baadhi ya watu waliokuwa karibu
walinisaidia na wale watu wakakimbia,” anasimulia msichana huyo.
Alisema baada ya tukio hilo, watu hao walitoweka machoni mwake hadi walipoibuka tena Januari 14, mwaka 2012.
Anasema siku hiyo alikuwa na mdogo wake Geofrey wakichota maji
bombani, wakati wazazi wao wakiwa kanisani, aliwaona watu wawili
wakitembea kwa kunyata wakielekea upande waliokuwepo, alipowatazama
akawatambua kuwa mmoja wao alikuwa ni miongoni mwa wale waliotaka
kumuingiza ndani ya gari kwa nguvu mwaka uliopita.
“Niliamua kukimbia kuelekea kwa jirani huku nikipiga mayowe kuomba
msaada, mmoja wao alinipiga ngwala na kuanza kunishambulia, nilishindwa
kuinuka, mgongo ulikosa nguvu, mtu mmoja mwenye mbwa alitoka nje
akanikuta niko chini, wakakimbizwa kuelekea bondeni, wazazi wangu
walipigiwa simu, walifika na kunichukua hadi Kituo cha Polisi Kitunda.”
“Nilipelekwa zahanati ya hapo Kitunda ikashindikana, nilihamishiwa
Amana na hali ikazidi kuwa mbaya, nikahamishiwa Muhimbili ambako
nililazwa kwa muda wa miezi mitano, wakati naendelea na matibabu
nilipata taarifa kuwa watuhumiwa wangu wameachiwa na kumtishia maisha
baba, hata hivyo kesi ilipelekwa Mahakama ya Wilaya ya Ilala.
“Baada ya mdogo wangu kuitwa mahakamani kutoa ushahidi, nikiwa
hospitalini niliwahi kuchukuliwa kupelekwa kortini kutoa ushahidi, hali
ilipozidi kuwa mbaya mama akawa ananiwakilisha, lakini cha kunishangaza
Aprili 25, mwaka huu, kesi ilifutwa kufuatia mpelelezi kutokwenda kutoa
maelezo yake.
“Nilipomuuliza huyo mpelelezi wangu sababu ya kutofika mahakamani,
alisema hakupewa samansi ya kuitwa, akasema hata yeye alishangazwa na
hukumu hiyo, sikuridhika, tulipoomba nakala ya hukumu tunazungushwa tu,
tulienda chama cha wanasheria wanawake TAWLA, waliiandikia barua
mahakama Mei,12 Mwaka huu, hata hivyo wamekataa kutupa.
“Uamuzi ulitolewa unanipa hofu, mtuhumiwa yupo mtaani na wanatutishia
maisha, nimelemaa, natembelea tumbo, nimepoteza masomo, haki yangu
mahakamani nimenyimwa, hivi ni nani wa kunitetea kama siyo serikali,
nikalalamike wapi miye mlemavu, nawaombeni serikali mnisaidie kufuatilia
mwenendo wa kesi yangu,” alilalamika binti huyo, ambaye anadai
watuhumiwa wake wanatishia kumuua endapo ataendelea kufuatilia kesi yao.
Naye baba mzazi wa mtoto huyo, Willison alisema anashangazwa na hatua
iliyochukuliwa na vyombo vya dola kulishugulikia suala hili kwani kila
sehemu wanakoenda wanakatishwa tamaa huku watuhumiwa wakizidi kuwatishia
maisha.
“Inaniuma sana kumwona mwanangu amelazwa na watu wanaofahamika lakini
wameachiwa, jalada la kesi hii ni namba 171 ya mwaka 2012 Wilaya ya
Ilala, naomba wanasheria wanisaidie.”
Kwa mtu yeyote aliyeguswa na
habari hii, anayedhani anaweza kuwasaidia ushauri wa kisheria, wanaweza
kuwasiliana na Bwana Willson kwa 0786 515604.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)

No comments:
Post a Comment