SIKU chache zimekatika tangu kusambazwa kwa picha
feki inayodaiwa ni ya mama wa Miss Tanzania 2006, Wema Sepetu, Mariam
Sepetu, wawili hao wako kwenye mkakati mzito wa kuwasomea kisomo cha
Albadili wale wote waliohusika kwa namna yoyote ile kuitengeneza picha
hiyo na kuitupia mitandaoni, Risasi Jumamosi linakumegea.
Picha hiyo iliyosambazwa kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii ikiwa
na kichwa cha mama Wema, lakini sehemu ya kuanzia shingoni kwenda chini
si yeye na mhusika alikuwa hana nguo, ilizua gumzo kwa wiki mbili sasa
huku watu wanaojiita Timu Dengue wakitajwa kuhusika.
KINYWANI MWA CHANZO CHA HABARI
Kwa mujibu wa chanzo chetu, mama
Wema na mwanaye wameamua kusoma Albadili ili kuwaadabisha wale wote
waliohusika na sakata hilo lenye kufedhehesha.
“Mama Wema na mwanaye
walikasirishwa sana na watu waliotengeneza ile picha na kuitupia kwenye
mitandao ya kijamii kama Instagram.
“Wiki iliyopita baadhi ya wasamaria wema walikwenda nyumbani kwa mama
Wema na kumtajia majina ya wahusika, lakini hawakuwa na ushahidi hivyo
yeye na Wema wameamua kujiunga kiimani zaidi kwa kusoma Albadili.
“Wamesema kwanza kabla ya tukio hilo la Abdadili wametoa siku saba
kwa yeyote anayejijua amehusika na picha zile za kutengeneza aende
mwenyewe kwa mama Wema, nyumbani kwake, Sinza-Mori (Dar) ili kuomba
msamaha.
“Kama zitapita siku saba na hakuna atakayejitokeza, Albadili itasomwa
na mmoja baada ya mwingine watakufa. Tayari wameshawasiliana na mashehe
ambao watasoma Albadili hiyo,” kilisema chanzo hicho.
WEMA AYEYUKA HEWANI
Baada ya kusikia kutoka kwa chanzo chetu cha
uhakika, juzi Risasi Jumamosi lilimsaka Wema ili kumsikia anasemaje
kuhusu kuwepo kwa madai hayo lakini muda mwingi wa maandalizi ya habari
hii, simu yake haikuwa hewani!
MAMA WEMA SASA
Baada ya kumkosa Wema, Risasi Jumamosi lilimtafuta
mama yake, naye kwa njia ya simu na alipopatikana aliombwa kutoa
ufafanuzi juu ya madai hayo.
KUHUSU ALBADILIAkizungumza kwa hasira huku sauti yake ikionesha dalili kwamba bado hayuko sawa, mama Wema alisema:
“Ni kweli, nimeshapanga kufanya hivyo, nitasoma Albadili. Haiwezekani
watu wakae na kuamua kunichafua mimi, nimewakosea nini cha mno mpaka
kufikia kufanya vile! Siwezi kukubali hata kidogo.”
KUHUSU MASHEHE
“Ni kweli pia, nimeshawasiliana na mashehe. Wao
wako tayari wanachosubiri ni kupita kwa siku ambazo nimetoa. Kama hakuna
atakayejitokeza kuomba radhi, kisomo cha Albadili kitasomwa, wataanza
kupukutika mmoja baada ya mwingine kweli nasema.”
SIKU SABA ZINAANZA LINI?
“Jumamosi ijayo (leo) itakuwa siku ya kwanza. Kwa hiyo mpaka Ijumaa ya Julai 11 (mwaka huu), itakuwa siku ya mwisho.”
NENO LAKE KWA WAHUSIKA
“Nawaambia wale wote wanaojijua walihusika
na ile picha ya uongo, ya kutumbukiza kichwa changu kwenye picha
nyingine na wale waliohusika kuitupia kwenye mitandao, waje waniombe
radhi kabla siku saba hazijaisha, sitanii jamani.”
UKWELI WAKE
“Mimi ni Muislamu safi, nasema sijawahi kupiga picha
za namna hiyo katika maisha yangu tangu nizaliwe mpaka utu uzima wangu
huu na wala sijawahi kufikiria.”
KUMBUKUMBU YA WEMA
Katika Gazeti la Risasi Mchanganyiko, Toleo la
Juni 25, mwaka huu, ukurasa wa mbele kulikuwa na habari yenye kichwa;
Wema azimia!
Habari ile ilimhusu Wema kupoteza fahamu kufuatia kuiona picha hiyo kwenye mitandao akidai ililenga kumchafulia mama yake jina.
KILIO KWA TCRA
Kumekuwa na wimbi la watu kuchafuana kwenye
mitandao ya kijamii ambapo ukiacha watu maarufu kutengenezewa picha
chafu, pia wanafunzi wa vyuo wamekuwa waathirika wakubwa.
Hata hivyo, baadhi ya wananchi waliowahi kuzungumza na gazeti hili
kwa nyakati tofauti walitoa kilio chao kwa Wizara ya Sayansi na
Teknolojia kupitia Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kudhibiti
usambazwaji wa picha chafu mitandaoni.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment