MUIGIZAJI mwenye mvuto wa kipekee Bongo, Elizabeth
Michael Kimemeta ‘Lulu’ juzikati alimsapraizi staa mwenzake wa sinema za
Kibongo, Mahsein Awadh ‘Dk. Cheni’ pale alipomfuata mbele na kummwagia
Dola za Marekani kiasi ambacho hakikujulikana mara moja.
Lulu alifanya tukio hilo mbele ya watu kibao, katika sherehe ya
maadhimisho ya siku ya kuzaliwa (birthday party) ya Dk. Cheni ikiwa ni
pongezi zake kwa staa huyo kufikisha miaka kadhaa tangu alipoiona dunia.
Tukio hilo lililomshtusha Dk. Cheni lilitokea Julai 20, 2014 kwenye
Ukumbi wa Ngorongoro uliopo ndani ya Hoteli ya Lamada, Ilala jijini Dar
es Salaam.
Katika tukio hilo, Dk. Cheni aliambatanisha na shughuli ya
kuwafuturisha mastaa wenzake na wadau mbalimbali wa sinema Bongo katika
Mfungo wa Mwezi Mtukufu wa Ramadhani.
MWANZO WA TUKIO
Ilidaiwa kuwa, Dk. Cheni kwa kuwa aliamua
kuitumia nafasi ya kufuturisha siku hiyo na kusherehekea bethidei yake,
alijipanga vilivyo kuhakikisha kila mhudhuriaji anafurahia uwepo wake
kwenye shughuli hiyo.
Miongoni mwa mastaa waliohudhuria mbali na Lulu ni pamoja na msanii
wa nyimbo za kughani mashairi, Mrisho Mpoto, Vincent Kigosi ‘Ray’, Salum
Mchoma ‘Chiki’, William Mtitu, Jacob Stephen ‘JB’ na Yobnesh Yusuph
‘Batuli’.
Wengine ni mkongwe kwenye Bongo Fleva, Joseph Haule ‘Profesa Jay’,
Halima Yahya ‘Davina’, Wastara Juma, komediani Hemedi Maliyaga ‘Mkwere’,
Kulwa Kikumba ‘Dude’, mwimbaji wa Injili, Emmanuel Mbasha (anayelishwa
keki) na wengine wengi.
ILIKUWAJE?
Ni baada ya futuru kumalizika ndipo wakati wa
shamrashamra za bethidei zilipounga ambapo Chiki aliyebeba jukumu la
u-MC aliwatangazia watu kwamba, miaka kadhaa nyuma, tarehe 20, Julai,
Dk. Cheni alizaliwa jijini Dar es Salaam.
FURAHA, PONGEZI
Kuanzia hapo, furaha za kumbukumbu hiyo ziliibuka
na kwa vile watu walikuwa wameshiba, waliweza kumpa pongezi Dk. Cheni
kwa kumfuata mmojammoja alipokuwa amesimama na mke wake, Sabra wakitumia
staili mbalimbali kwa kila mmoja alivyotaka lakini bila kuvunja
maadili.
Wengi walimpongeza kwa kumkumbatia au kumpa mkono wa heri ulioambatana na zawadi mbalimbali zikiwemo fedha.
LULU ASIMAMA, AENDA KWA DK. CHENI
Lulu ambaye amezoea kumwita Dk. Cheni baba, naye alisimama na kumfuata ‘mtoto’ Cheni ili kumtunza kwa alichonacho.
Macho ya wengi yalitarajia kumuona Lulu amebeba mzigo wa zawadi
lakini walipogundua hana, waliamini angetuza kwa noti za ‘Msimbazi’
ambazo zinatumika Bongo, matokeo yake akaanza kuchomoa dola katika
‘waleti’ yake ya kike na kumtupia.
MPOTO AJIBU MAPIGO
Kama waliambiana, baada ya Lulu kuonesha jeuri
hiyo ya fedha tena zenye hadhi ya kimataifa, Mpoto naye alichomoa
waleti yake na kutoa dola kisha akaenda mbele kumpa Dk. Cheni huku watu
wakishangilia.
DK. CHENI ATOA NENO
Baada ya kuona zawadi hiyo, Dk. Cheni ambaye
alivaa kanzu yenye rangi ya maji ya maharage alijikuta akizidiwa na
furaha kiasi cha kukaribia kumwaga machozi.
Katika kuonyesha furaha yake, Dk. Cheni alifunguka: “Jamani Lulu
utaniua baba yako. Ni mambo gani hayo unanifanyia ya kushtukizana?”
LULU ASAKWA NA MAPAPARAZI
Baada ya shughuli hiyo kumalizika, mapaparazi wa Risasi Mchanganyiko
walimfuata Lulu na kumuuliza dola alizompa Dk. Cheni zina thamani ya
shilingi ngapi za Kitanzania.
Hata hivyo, nyota huyo alikataa kuweka wazi akisema ni siri ya aliyepewa.
“Hiyo ni siri ya Dk. Cheni mwenyewe, mimi nitasema nini sasa jamani?”
Mapaparazi walimfuata Dk. Cheni na kumuuliza ambapo aliminya idadi
kamili ya fedha alizotoa Lulu na Mpoto akisema ni siri yake na mke wake.
Tunampongeza Dk. Cheni kwa kuadhimisha miaka kadhaa ya kuzaliwa
kwake, tunamtakia kila la kheri katika kazi za mikono yake na familia
yake kwa jumla – MHARIRI. Imeandikwa na Musa Mateja, Shakoor Jongo na
Shani Ramadhani.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment