MKASA WA TRAFIKI NA DEREVA WA GARI DOGO

Sekeseke la aina yake kati ya dereva wa gari dogo aina ya Toyota Pick up na trafiki ambao majina yao hayakujulikana mara moja liliibuka na kuzua maswali mengi kwa mashuhuda huku mambo ya rushwa yakitajwatajwa.  Tukio hilo lilizozua maswali mengi liliibuka juzi Jumatano, Bamaga, Mwenge jijini Dar jirani na kituo cha mafuta cha Bamaga.

Katika tukio hilo, dereva huyo na trafiki walikuwa wakikunjana, ambapo dereva alikuwa akilalamika kuonewa (Haikujulikana kivipi) wakati askari huyo wa usalama barabarani akisisitiza kuwa jamaa huyo alivunja sheria.
Trafiki akimdhibiti dereva wa gari dogo aina ya Toyota Pick up.
Gari aina ya 'Land Rover' (break down) lililotumika kuvuta gari la aina ya Toyota Pick up la dereva huyo.

Trafiki alisikika akimwambia dereva kuwa amevunja sheria za barabarani huku gari lake likiwa bovu hivyo aliamuru gari hilo kuvutwa hadi kituoni kwa ajili ya ukaguzi lakini dereva huyo alikataa.
Pamoja na kuelezwa kuwa gari lake lilikuwa na matatizo na mahali alipoegesha hapakuwa sahihi, dereva huyo alipayuka: “Nawajua nyie trafiki, kazi yenu ni kuonea watu sasa mimi sitoi kitu hapa, labda mniue.“Siendi popote, mkiondoa gari nalala mbele yake ili mnigonge nife, mimi nimesema silitoi.”

Trafiki huyo aliyeonekana kuwa makini na kazi yake, hakuwa na makuu, zaidi alitaka gari livutwe hadi kituoni huko sheria ingefuata mkondo wake baada ya ukaguzi.
 Mashuhuda wa tukio hilo, walisikika wakisema kilichohitajika kilikuwa ni busara ya masikilizano kuliko kuvutana kwa maneno na afisa wa polisi.
Afisa usalama wa barabarani akisisitiza kulichukua gari la dereva huyo kwa ukaguzi zaidi.
 “Sasa kama gari lake anajua ni zima, anabishana nini na polisi? Ikiwa anajiamini kuwa aliegesha sehemu sahihi, hofu yake ni nini? Kama kweli anajua yupo sawa, anatakiwa kukubali kwenda polisi, gari likakaguliwe.

“Wakati mwingine unaweza kuwalaumu tu askari, kumbe ni tabia ya watu kukataa kutii sheria bila shuruti. Sasa anafikiri kwa maneno makali anayotoa kwa huyo askari atamwachia?
Raia wakishuhudia mkasa huo uliotokea katika kituo cha mabasi yaendayo Mwenge cha Bamaga.

 “Anasema eti hatoi kitu, kwani kaombwa rushwa pale au anadhani kila trafiki anayemkamata dereva aliyevunja sheria anataka rushwa?” alisikika shuhuda mmoja akihoji kwa jazba.
Hata hivyo, pamoja na mkwara wa jamaa huyo, gari lake lilifanikiwa kuvutwa kuelekea polisi ambapo jamaa huyo alipanda gari lingine kulifuata.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger