Makamu Mkuu wa Chuo cha
International Medical and Technological University (IMTU), Profesa PV
Prabhak Rao (mwenye koti la blue) na viongozi wengine wakisindikizwa na
polisi kuingia kwenye Kituo cha Oysterbay, Dar es Salaam jana, kwa ajili
ya mahojiano kuhusiana na upatikanaji wa viungo vya binadamu eneo la
Mpigi Bunju. Picha na Rafael Lubava
Watumishi wanane wa IMTU mbaroni kwa tuhuma za kuhusika na tukio hilo
Mtaalamu abainisha jinsi maiti zinavyotumika kufundishia vyuoni Dar es Salaam.
Wakati ikibainika kuwa viungo vya miili
ya binadamu vilivyookotwa juzi katika Bonde la Mto Mpiji nje kidogo ya
Jiji la Dar es Salaam vilitoka katika Chuo Kikuu cha Kimataifa cha Tiba
na Teknolojia (IMTU), jana Jeshi la Polisi liliwatia nguvuni watumishi
wanane wa chuo hicho kuhusiana na sakata hilo.
Kukamatwa kwa watumishi hao kumeelezwa
na Kamanda wa Polisi Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Suleiman Kova kuwa
ni baada ya uchunguzi wa awali kubaini kuwa viungo hivyo kwa mara ya
mwisho vilikuwa katika maabara ya IMTU.
Alisema tukio hilo lilitokea juzi jioni
eneo la Bonde la Mbweni Mpiji ambako iligundulika mifuko ya plastiki 85
yenye mabaki ya viungo vya binadamu.
Kutokana na tukio hilo, Polisi imeunda
jopo la wapelelezi saba likiongozwa na Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu,
Jafari Mohamed kusaidiana na daktari wa jeshi hilo kufanya uchunguzi wa
miili hiyo.
“Katika uchunguzi wetu tulibaini kuwa
hivyo viungo vya binadamu vilitolewa katika Chuo cha IMTU na
kusindikizwa na mfanyakazi wa ngazi ya juu kwa ajili ya kutupwa eneo la
Bonde la Mbweni Mpiji,” alisema Kova.
Alisema mifuko hiyo ilikuwa myeusi ikiwa
na viungo vya aina mbalimbali vikiwamo vichwa, miguu, mikono, moyo,
mapafu, vifua na mifupa ya aina mbalimbali.
“Viungo hivyo havikuwa na harufu wala uvundo wa aina yoyote na vilionekana vimekaushwa na kukakamaa,” alisema.
Alisema katika eneo hilo walikuta vifaa
vinavyotumika hospitali kama glovu, nguo maalumu (apron) 20 na karatasi
mbili zenye maswali ya kujibu.
Kova alisema viungo hivyo vilichukuliwa na kupelekwa Hospitali ya Taifa ya Muhimbili (MNH).
Alisema jeshi hilo limefungua jalada la
uchunguzi ili kujua sheria gani imevunjwa na kwa nini viungo hivyo
vilitupwa hapo na kwa nini wasitumie utaratibu mzuri wa kuhifadhi na
kwamba endapo kuna makosa ya kisheria, hatua zitachukuliwa na Ofisi ya
Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP).
Muhimbili wapokea mabaki
Meneja Uhusiano wa MNH, Aminiel
Aligaesha alisema jana kuwa hospitali hiyo imepokea vifurushi 40 vyenye
mabaki ya miili ya binadamu na kuhifadhiwa wakisubiri maelekezo ya
polisi... “Hili ni suala la polisi, ninachoweza kusema ni kweli
tumepokea vifurushi hivyo jana (juzi) usiku.”
Wakati Kova akisema hayo, uongozi wa
IMTU ulikiri kuhusika na mabaki ya miili hiyo yaliyotupwa katika mto huo
usiku wa kuamkia Jumapili iliyopita.
Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Dk
Fariji Mtango alisema jana kwamba anaamini miili hiyo inaweza kuwa ni
ile iliyotoka katika chuo hicho, ambayo imekuwa ikifanyiwa mazoezi na
wanafunzi kwa kuwa walihitaji kuiteketeza na walishatoa agizo hilo.
Alisema walitoa agizo kwamba mabaki hayo
yapelekwe Muhimbili kwa mujibu wa utaratibu wao kwa kuwa hayakuwa na
matumizi tena, kwa kuwa ndiyo sehemu yenye uwezo wa kuyateketeza na
kutoa jukumu hilo kwa mmoja wa wakufunzi wa chuo hicho ambaye jana
alikuwa safarini.
“Sasa zaidi hatujui kilichoendelea
lakini tulipoangalia jana (Jumatatu) tulikuta sehemu yalipohifadhiwa
imesafishwa, hivyo inawezekana ni sehemu ya vile vilivyoondolewa hapa.
Hatukutarajia kwamba vingetupwa katika eneo lisilokuwa sahihi kama
ilivyofanyika,” alisema.
Dk Mtango alisema hiyo ilikuwa moja ya
hatua za kupisha wakaguzi ambao walitarajiwa kukuta maeneo yote ya
kufundishia yakiwa katika hali ya usafi na unadhifu.
“Hawa wakaguzi wanapokuja wanatakiwa
waone vitu vyote vikiwa sawa. Hata kama wangeona hayo mabaki ya miili ya
binadamu isingekuwa tatizo, bahati nzuri wamekuja jana na wamefanya
kazi yao vizuri,” alisema.
Muda mfupi baada ya kutolewa kauli hiyo,
viongozi tisa wa chuo hicho na walinzi wawili walikamatwa mnamo saa
7.30 mchana na kupelekwa katika Kituo cha Polisi Oysterbay ambako
wanashikiliwa, lakini baadaye Kova alisema waliokamatwa ni wanane.
Jana mchana eneo la chuo cha IMTU
lilikuwa chini ya ulinzi mkali wa polisi waliotanda kuanzia getini,
mapokezi na kwenye bustani za chuo hicho na wengine waliovalia sare
maarufu kama ‘tigo’ ambao walikuwa wakishika doria mbele ya chuo hicho.
Hatua kuchukuliwa
Dk Mtango alisema uongozi wa chuo hicho
umeshtushwa na kutupwa kwa mabaki hayo katika utaratibu usiokubalika na
utafanya uchunguzi na kuchukua hatua kwa wote waliohusika.
“Tunaanza na huyu ambaye tulimpa hili
jukumu. Yeye ndiye aliyetakiwa kusimamia na anaujua wazi utaratibu wetu.
Kwa sasa hajafika hapa na hata simu yake haipatikani. Tunaarifiwa
kwamba amekwenda Zanzibar,” alisema.
Juzi jioni, ilitokea taharuki baada ya
wananchi kubaini viungo hivyo na taarifa kuanza kusambaa katika mitandao
ya kijamii na baadaye vyombo vya habari na hadi jana mjadala kuhusu
suala hilo ulikuwa mzito na wananchi wakihoji miili hiyo ni ya watu
gani, imetoka wapi na imetupwa na watu gani.
Shuhuda wa tukio hilo, Mariam Nkumba
alisema mara ya kwanza aliona mifuko yenye viungo hivyo Jumapili
alipokwenda kuponda kokoto katika eneo hilo lakini hakubaini kulikuwa na
nini.
Siku hiyo, Nkumba alisema aliondoka
katika eneo hilo saa 12 jioni bila kujua nini kilikuwa ndani ya mifuko
hiyo na siku iliyofuata (Jumatatu), alikwenda kuchukua mfuko mmoja ili
ahifadhie kokoto zake, ndipo aliposhtuka kuona viungo vya binadamu.
“Mifuko ilikuwa mingi kweli, yote
ilikuwa imejaa viungo vya binadamu. Mpaka sasa sijala na sina hamu ya
kula. Ukiiona ile miili huwezi kula chakula,” alisema.
Mfanyakazi wa Kampuni ya Ujenzi ya Skol
iliyopo karibu na eneo hilo, Supery Kaijunga alisema mara alipopata
taarifa kutoka kwa Nkumba alianza kutoa taarifa kwa wananchi wengine ili
kwa pamoja wajue la kufanya.
Baadaye walitoa taarifa polisi ambao walifika saa mbili usiku na kukusanya mabaki yote na kuondoka nayo.
Hata hivyo, Kaijunga alieleza wasiwasi wake kuhusu wingi wa miili hiyo na kuhoji walikuwa watu gani na walitoka maeneo gani.
“Tukio hili siyo la kawaida na
halijawahi kutokea huku kwetu. Tunakuwa na wasiwasi sana labda nasi
maisha yetu yatachukuliwa kama hawa; polisi wafanye uchunguzi wa kina
kubaini ukweli wake,” alisema Kaijunga.
No comments:
Post a Comment