MREMBO AAGA DUNIA AKIJIANDAA KWENDA DUBAI

BINTI mmoja aliyefahamika  kwa  jina la Suzana Adamu (20), mkazi  wa Mazizini- Ukonga jijini Dar amefariki dunia kwa kugongwa na gari akitoka  kukamilisha taratibu za  viza kwa ajili ya kwenda  Dubai kufanya kazi.
Ndugu wa marehemu Suzana Adamu wakilia kwa uchungu.

Kwa mujibu wa  mashuhuda  wa ajali  hiyo, ilitokea Agosti Mosi, mwaka huu saa 2:30  usiku katika Mtaa wa Mahita ambapo mrembo huyo alikuwa akitoka mjini kwa  ajili ‘shoping’ pia  kuaga ndugu na jamaa ili kesho yake apande ndege kwenda Dubai ambako alipata kazi ya mkataba wa miaka miwili.
Ndugu na jamaa wakiomboleza msiba huo.
Ilidaiwa kuwa, akiwa anarudi nyumbani kwao, alipofika eneo hilo alizolewa na gari lililokuwa limekodiwa  na watu waliokuwa wanatoka  ufukweni kula Sikukuu ya Idd.

Mashuhuda walisema dereva wa gari hilo alikuwa  mwendo kasi na hivyo kumvaa binti huyo aliyekuwa akitembea kwa miguu.Imeelezwa kuwa, kutokana na mwendo kasi, baada ya kumgonga Suzana gari hilo lilikwenda  kugonga ukuta.Mwili wa marehemu ukishushwa kwenye gari nyumbani kwao.
Akizungumza na Amani kwenye msiba wa binti yake, baba mzazi wa mrembo huyo, Adamu Mohamed alisema siku ya maziko ya marehemu huyo ndiyo ilikuwa safari yake ya kwenda Dubai.
“Ndugu mwandishi, kaburini ndiyo Dubai ya mwanangu. Sasa si mkataba tena wa miaka miwili bali amepata mkataba wa kudumu huko alikokwenda,” alisema mzee huyo kwa masikitiko.

Marehemu Susan Adamu enzi za uhai wake.
Alisema Suzana ni mtoto wake wa nne kuzaliwa, amemuacha katika  wakati mgumu kwa sababu alikuwa   tegemeo kubwa ndani ya familia. Marehemu Suzana alizikwa Agosti 2, mwaka huu katika Makaburi ya Kijiji cha Mfuru, Kata ya Maneremango, Wilaya ya Kisarawe mkoani Pwani.
Mmoja wa marafiki wa marehemu aliyejitambulisha kwa jina moja la Aisha, alisema kifo cha Suzana ni pigo kubwa kwao kwani alikuwa mkarimu aliyependa kuwasaidia wenzake.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger