KATIKA hali ya kushangaza, mtu mmoja ambaye ni fundi seremala aitwaye
Emmanuel Carlos, mkazi wa Kwabinyau Magomeni jijini Dar amekutwa akiwa
amejinyonga saa mbili asubuhi Septemba 23, mwaka huu katika kile
kinachodaiwa kuchoshwa na mgogoro wa kifamilia.
Habari kutoka eneo la tukio zinasema kwamba, kwa muda mrefu, marehemu
alikuwa na mgogoro usioisha na mkewe Mariamu Suleimani uliosababisha
wawili hao kulala katika vyumba tofauti ndani ya nyumba yao.
Baadhi ya majirani wa eneo hilo walisema kutokana na ugomvi huo,
marehemu alikuwa akirudi nyumbani usiku akiwa amelewa na kumtukana
matusi mkewe huku baadhi wakienda mbali na kudai alikuwa haachi hela ya
matumizi.
Hata hivyo, mkewe marehemu anadaiwa kuwa na biashara yake ya samaki
na alikuwa akijituma ili kuhakikisha anapata nauli ili arejee nyumbani
kwao.
Kwa mujibu wa maelezo yaliyopatikana, mtu wa kwanza kujua kuhusu
suala hilo alikuwa ni kijana wake mwenye umri wa miaka saba, Celestine
Carlos aliyekwenda chumbani kwa baba yake kuomba hela ya shule, ambapo
alimkuta akining’inia kwenye dari baada ya kuwa amejifunga kamba kwenye
feni.
Akizungumza na waandishi wetu Mariamu alisema kuwa siku moja kabla ya
tukio, mumewe alirudi nyumbani na kumtukana huku akilia na kumwambia
kuwa atamkumbuka sana katika maisha yake na kwamba kabla ya kupambazuka
mmoja wao atakuwa amekufa.
“Siku iliyofuata alipoamka alinikuta naosha vyombo, akanitazama kwa jicho baya kisha akaenda chumbani kwake ambako alijifungia.
Nusu saa baadaye alikuja mwanaye Celestine na kuniomba hela ya shule,
nikamwambia aende akachukue kwa baba yake, alipoingia akarudi na
kuniambia baba yake ananing’inia, jambo nililoona kama utani lakini
baadaye nilienda na kumkuta akiwa amejinyonga,” alisema Mariamu huku
akilia kwa uchungu.
Naye mjumbe wa serikali ya mtaa huo, Jumanne Mneka alikiri kufahamu
mgogoro wa familia hiyo na kusema walikuwa wakiwasuluhisha kila mara.
“Juzi kati tu tumetoka kuwapatanisha, nashangaa leo saa mbili asubuhi
napokea taarifa kuwa Emmanuel amejinyonga, nimehuzunika sana,” alisema.
Majirani wakiwa wameshtushwa na kushangazwa na jambo hilo, waliungana
na wapita njia kwenda kushuhudia tukio hilo, hali iliyoufanya mtaa huo
usipitike kwa muda.
Waandishi wetu waliwashuhudia polisi wakifika
eneo hilo na kuuchukua mwili na kuupeleka katika Hospitali ya
Mwananyamala kwa ajili ya uchunguzi. Marehemu ameacha mke na watoto
wawili.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment