POLISI WA KENYA WALA KICHAPO KIKALI KUTOKA KWA POLISI WA UGANDA BAADA YA KUKAIDI AMRI.

MAAFISA watatu wa polisi wa utawala (AP) walijeruhiwa kwenye mapigano yaliyozuka kati yao na wenzao wa Uganda kwenye kisiwa kinachozozaniwa cha Migingo.
Mzozo huo wa mwishoni mwa wiki ulianza pale maafisa wa Uganda waliokuwa na sare rasmi walipoenda katika ufuo wa karibu wa Nyandiwa kurekebisha mashua yao.


Lakini wakazi wa Nyandiwa waliwazuia kutia nanga wakisema kwa vile walikuwa na sare na bunduki, walihofia wangeliwahangaisha kwa kuwapokonya samaki wao.
Mmoja wa wavuvi wa eneo hilo Bw Oloo Okello, alisema maafisa hao wa Uganda walirejea Migindo wakuwa na hasira bila ya kurekebisha boti lao.



“Waliporejea walisema kwamba polisi wa Utawala wa Kenya wa kitengo cha kushika doria mpakani, Rural Border Patrol Unit (RBPU), walio kisiwani Ugingo hawatakiwi kutia guu Migingo.
Lakini maafisa hao watatu wa polisi wa Kenya walipuuza tangazo hilo na kwenda kisiwani Migindo kununua bidhaa.
Ni wakati huo walipoanza kutandikwa na maafisa hao wa Uganda, huku maafisa wa usalama wa Kenya, wakiwemo polisi wa kawaida wakitazama kwa mbali bila kufanya lolote.
Maafisa hao wa polisi wa Kenya hawakuwa na silaha wakati huo na inasemekana walipigwa kutokana na agizo kutoka Kampala, ingawa Taifa Leo haikuweza kuthibitisha madai hayo.
Ripoti nyingine zinasema kwamba maafisa hao wa Uganda walikuwa wakienda eneo la Nyandiwa na wakazuiwa na polisi hao wa Utawala. Inadaiwa kuwa polisi wa Utawala wa Kenya walikuwa wamesisitiza kuwa, kama maafisa hao wa usalama wa Uganda walikuwa na lasima ya kuingia kwenye eneo la Kenya, basi hawakuwa na budi kuacha silaha zao.
Onyo
Jambo hilo liliwaudhi maafisa hao wa Uganda ambao inasemekana waliwaonya Wakenya nao wasithubutu kuweka guu Migingo.
Naibu Kamishna wa Kaunti wa eneo la Nyatike, Bw Moses Ivuto, alisema ingawa tukio hilo ni la kusikitisha, suala hilo tayari limeanza kushughulikiwa na wakuu wa serikali zote mbili.
Alisema inawezekana kuwa mkuu wa polisi wa Uganda katika kisiwa cha Migingo huenda hakuwa na habari kuhusu tukio hilo.
“Inawezekana mkuu wa polisi wa Uganda aliye Migingo hakuelewa kuwa maafisa wake waliingia eneo la Kenya wakiwa na silaha. Kawaida huwa polisi wa upande mmoja hawaruhusiwi kwenda eneo jingine akiwa na silaha,” akasema.
Kaimu kamanda wa polisi hao wa Utawala katika eneo hilo Bw  Peter Gikonyo, alisema wanafanya juhudi kuhakikisha maafisa wa usalama wa nchi hizo jirani kwenye kisiwa cha Migingo wanafanya kazi kwa ushirikiano.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger