TAARIFA za awali kutoka kwa makachero wa Jeshi la Polisi nchini zimefanikiwa kubaini mtandao wa ulipuaji mabomu katika jiji la Arusha, imefahamika. Mpaka sasa taarifa zinadai mtandao uliohusika na milipuko miwili iliyotokea kwa nyakati tofauti jijini hapa ulipangwa ndani ya jiji la Arusha.
Mlipuko wa kwanza ulitokea katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti, Mei 5, mwaka huu na kuua watu watatu, wakati mlipuko wa pili ulitokea Uwanja wa Soweto Juni 15, mwaka huu na kuua watu wanne, huku majeruhi wa matukio yote wakifikia zaidi ya 100.
Akizungumza katika kikao cha Kamati ya Ushauri ya Mkoa wa Arusha (RCC) jana jijini hapa, Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Magesa Mulongo, alisema mbinu hizo zimejulikana kutokana na wananchi waliojitokeza kuwasilisha ushahidi kwa vyombo vya dola.
Alisema mpaka sasa ushahidi unaonyesha kuwa mtandao wa waliolipua wa mabomu hayo ulianzia jijini Arusha, na kikubwa kabisa wanawashukuru wakazi wa Arusha waliokuwa wakifika kutoa ushahidi wa wahusika.
“Ukweli wa mambo haya utajulikana hivi karibuni na Serikali itamchukulia hatua mtu yeyote atakayebainika kuhusika na mtandao huo, bila kujali wadhifa wake. Mambo haya yamedhalilisha na kufedhehesha Taifa,” alisema Mulongo.
Akiwa ndiye Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa, aliendelea kubainisha kuwa upelelezi wa matuko hayo mawili unaendelea kwa umakini mkubwa na kikubwa kinachoangaliwa ni kuepuka kukamata watu wasiohusika.
“Tunachukua umakini ili waliofanya hivi vitendo vya kinyama wasiendelee kutamba, kwani wanajua tukikamata wasiohusika wao watajiona wameshinda hawajakamatwa,” alisema Mulongo.
Mwenyekiti huyo wa Kamati ya Ulinzi na Usalama ya Mkoa aliwataka pia wanasiasa nchini kutoigeuza milipuko ya mabomu hayo kama njia ya kujitafutia umaarufu wa kisiasa.
“Kugeuza tukio hili la kinyama kuwa agenda ya kisiasa kunaidhalilisha Tanzania nje ya nchi na kuleta athari za kupoteza wageni,” alisema Mulongo.
Mulongo alisema taarifa za awali za kikachero zinaonyesha kuwa bomu lililorushwa katika viwanja vya Soweto lilitengenezwa China.
Mkuu huyo wa mkoa alisema, tayari wataalamu kutoka China wamekwisha wasili jijini Arusha kwa ajili ya kufanya utambuzi wa taasisi iliyonunua bomu hilo.
Mulongo katika hotuba yake aliendelea kuwataka wanasiasa kuacha dharau na kueneza maneno yasiyo na ukweli juu ya Serikali, badala yake aliwataka kuheshimu taratibu za nchi ili vyombo vya dola visilazimike kutumia nguvu kukabiliana na watu au kikundi kitakachovunja sheria zilizowekwa.
“Hivi ndugu zangu, lazima tufike mahali tujiulize hawa wanasiasa wanaotumia uongo na nguvu nyingi kuchafua nchi huko duniani, wanafanya hivi kwa faida ya nani?” alihoji Mulongo.
Bomu hilo lilirushwa katika mkutano wa Chama cha Demokrasia na Maendelo (CHADEMA), wakati kikihitimisha kampeni zake za uchaguzi mdogo wa udiwani katika kata nne jijini Arusha Juni 15, mwaka huu.
Hata hivyo, siku mbili baada ya mlipuko huo, chama hicho kilitoa shutuma nzito dhidi ya Jeshi la Polisi na kueleza kuwa askari wa Kikosi cha Kutuliza Ghasia (FFU), ndiye aliyerusha bomu hilo.
Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe, aliwaeleza waandishi wa habari kuwa chama chake kinao ushahidi wa picha na sauti unaothibitisha kwamba polisi ndio wahusika wa mlipuko huo.
Hata hivyo, chama hicho kimegoma kukabidhi ushahidi huo kwa jeshi hilo kwa maelezo kuwa ushahidi huo hauwezi kutolewa kwa polisi, ambao ni watuhumiwa wa tukio hilo.
Chama hicho kilitoa sharti kwa Rais Jakaya Kikwete kuunda Tume ya Mahakama itakayohusisha majaji waadilifu na kusema kuwa kipo tayari kutoa ushahidi huo mbele ya tume hiyo na si polisi.
Mbali na bomu hilo, bomu jingine lilirushwa katika Kanisa la Mtakatifu Joseph Mfanyakazi, Olasiti na kusababisha watu watatu kufariki ambapo nalo liligundulika kutengenezwa nchini Urusi.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment