Na Gustav Chahe, Mufindi( Kamanda wa matukio)
MAHAKAMA ya Wilaya ya Mufindi imetupilia mbali mashtaka yaliyokuwa yakiwakabili Naibu Katibu Mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Hamad Yusuph na wenzake 42.
Kiongozi huyo pamoja na wenzake walikuwa wakikabiliwa na makosa matatu likiwemo la kufanya mkutano bila kibali pamoja na kuharibu mali ambazo ni kofia za pikipiki (helmenti) 2 za polisi katika tukio lililosababisha kuuawa aliyekuwa mwandishi wa habari wa kituo cha televisheni cha Channel Ten Daudi Mangosi katika kijiji cha Nyololo wailayani Mufindi.
Kutokana na tuhuma hizo Chadema iliweka pingamizi za kutaka kesi hiyo ifutwe kwa kuwa ilifunguliwa kinyume cha sheria.
Wakili wa Chadema Lugaziya akisaidiana na mwanasheria wa Chadema Luka Sinkala Mwenda waliweka pingamizi kuwa aliyetoa amri ya kusitisha mkutano na kusababisha kifo cha mwandishi wa habari huyo ni kamanda wa Polisi Michael Kamuhanda ambapo aliingilia kazi ya OCD wa Mufindi kwa kuwa hakupaswa kutoa amri hiyo, kwamba wakati amri ya kusitisha mkutano ilitolewa wakati hakukukuwa na vurugu na polisi walipiga mabomu wakati watu wanatawanyika.
Pingamizi zingine ni kwamba aliyetoa amri ya kutawanya mkutano hakuwa na cheo chochote.Wakati Chadema ikizuiliwa Chama cha Mapinduzi (CCM) katika jimbo la Bububu Zanzibar walikuwa na mkutano wa kampeni za uchaguzi..
Polisi walisema wanazuia mkutano kwa kuwa sensa inaendelea wakati huo sheria ya uchaguzi haizuii shughuli zingine kufanyika na kwamba walitaka polisi waeleze sheria ya sensa inayozuia shughuli zingine kufanyika inatoka wapi...
Watuhumiwa walipoambiwa watawanyike walitawanyika bila kugoma na mkutano uliofanyika ulikuwa wa ndani kwa kuwa ulikuwa ukifanyika ofisini baada ya mkutano wa hadhara kusitishwa na kwamba watuhumiwa waliofikishwa mahakamani walikamatwa nje ya eneo la tukio kwa kuwa walikuwa wametii amri.
Watuhumiwa hao walikamtwa maeneo ya Igawa mpakani mwa Mkoa wa Iringa na Mbeya baada ya kutoka katika eneo waliloamriwa kutawanyika.
Akitupilia Mbali kesi hiyo, Hakimu wa Wilaya ya Mufindi D. Nyakunga alisema pingamizi zilizowasilishwa na Chadema hazikujibiwa hata moja na upande wa utetezi.
"Hakuna pingamizi yoyote iliyojibiwa na upande wa utetezi. Hayo ni matumizi mabaya ya kifungu namba 91 kinataka upande wa utetezi kujibu pingamizi.
"Pia ni matumizi mabaya ya muda na fedha za serikali na walipa kodi. Kwa sababu hizo, kesi hii inafutwa" alisema Nyakunga.
Naibu Katibu Mkuu wa wa Chadema Zanzibar Hamad Yusuph na wenzake walifunguliwa kesi hiyo baada ya kukamatwa wakati wa ufunguzi wa matawi Septemba 2, 2012 ambapo Mwangosi aliuawa na polisi kwa kupigwa bomu.
No comments:
Post a Comment