Regina Kihosa (62), mkazi wa Kosolameba mkoani Kigoma amelazwa katika
Hospitali ya Taifa Muhimbili kufuatia gonjwa la ajabu lililompata huku
akidai kwamba limetokana na wachawi ambao wanausumbua mji wake.
KWANZA AMEPOTEZA WATOTO WANANE
Mama huyo
amelazwa katika hospitali hiyo jengo la Sewahaji,wodi namba 24
akiendelea na matibabu na ana mawazo mengi kwa kile anachokidai kwamba
wachawi wanachezea mji wake na kati ya watoto wake kumi aliowazaa wanane
wamefariki kwa muda mfupi kwa magonjwa ambayo wakipimwa hospitalini
hayaonekani.
Aliendelea kudai kwamba watoto wake wawili waliobaki wamekua waoga
na wamekimbia kutoka nyumbani kwake kuhofia kurogwa na kuuawa pia mume
wake aliyemtaja kwa jina la Ndeki Mashati naye alifariki kwa gonjwa la
ajabu la kujaa maji tumboni.
Regina akizungumza kwa shida huku akionekana mwenye uso wa majonzi na mawazo mengi alikuwa na haya ya kusema:
“Gonjwa linalonitesa lilianza mwaka jana kwa kuumwa chini ya meno
huku maji yakitoka sehemu hiyo, baadaye ulitokea uvimbe chini ya ulimi
ambao kadiri siku zilivyokwenda uliongezeka kukua ndipo nilipelekwa
Hospitali ya Mkoa Maweni kule Kigoma lakini sikuweza kupata tiba na
kurudi nyumbani kutokana na ugonjwa kutojulikana.
“Hali yangu nikiwa nyumbani ilizidi kuwa mbaya, sikuwa na mtu wa
kunihudumua wala kuniliwaza, ingawa madaktari wa Maweni walinishauri
nije Muhimbili lakini kutokana na umaskini nilikata tamaa, sikuwa na
nauli, nilitamani Mungu achukue uhai wangu kuliko kupata maumivu makali
kiasi hiki, nashindwa kula nashindia uji.
KUCHANGIWA NAULI
“Watoto wangu wawili waliobaki
walikuwa na hofu wakawa wanatangatanga baada ya kuwaona ndugu zao wanane
walivyokufa vifo vya kutatanisha kwa muda mfupi wa miaka minne,
walikimbia, nilibaki nyumbani peke yangu, nilifikiri jinsi ya kufika
Muhimbili bila mafanikio, namshukuru Mungu alinipa nguvu ya kwenda
kanisani kutoa kilio changu na mikachangiwa shilingi elfu sitini.
“Baada ya kupata fedha hizo nilijikongoja hadi kituo cha mabasi
nilipata usafiri hadi Tabora, nililala pale katika kituo cha mabasi
kesho yake nilikuja hapa Dar nilifika Kituo cha Mabasi Ubungo usiku saa
sita, nililazimika kulala kituoni kwani sikuwahi kufika wala sina ndugu
hapa jijini, kesho yake nilipanda daladala hadi Muhimbili.
“Ninawashukuru waumini wa kanisa walionichangia kwani baadhi ya
wananchi walisema wamechoka kunichangi kutokana na misiba ya kila
kukicha, nilijisikia vibaya kwani mimi sikupenda wanangu wafe ili nipate
michango yao.
AOGOPA KURUDI KWAKE
“Nawahukuru sana madaktari
wa hapa Muhimbili kwani tangu nije mwishoni mwa mwezi wa tatu wamekata
nyama ya mdomoni na kuifanyia uchunguzi pia wamechukua vipimo vingine
ikiwa ni pamoja na kunipiga picha ya x ray.
Na kuhusu chakula wananijali sana, kinachoniumiza ni kwamba hata
nikipona nitaenda wapi? Pale kwangu hakuna amani tena, napaogopa,
nikiangalia makaburi ya watoto wangu na mume wangu nashindwa kulala,”
alisema mama huyo huku akitokwa machozi
Mama huyo anaomba msaada kwa wasamaria wema kumsaidia, aliyeguswa
awasiliane na afisa ustawi ya jamii wa Muhimbili ambaye yupo naye karibu
kwani yeye hana simu. Anapatikana kwa namba 0683 406680.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment