MIMI
ni mkristo wa dhehebu la Roma. Mafundisho mengi tunayopewa kuanzia
Ubatizo, Komunyo ya Kwanza na Kipaimara, tunafundishwa kuhusu kutenda
mema, kupendana wenyewe kwa wenyewe na hata kuwapenda maadui zetu.
Tunaambiwa, akija mtu akakupiga kofi shavu lako la kushoto, wala
hata usimrudishie, bali mgeuzie na upande ule wa kulia na
akishakutundika hivyo vibao vyake, muombe Mwenyezi Mungu amsamehe.
Tunafundishwa kusamehe, ndiyo maana katika moja ya maandiko yaliyo
katika vitabu vya dini, kama Injili na Biblia, kuna mistari inayosema
samehe saba mara sabini.
Kwa wale ndugu zangu wasio wakristo, nitaomba niwaombe radhi kwa
kuanza na utangulizi huu. Ni kwa sababu leo nazungumza na mtu ambaye
wengi wetu tunaamini ni mtumishi wa Mungu. Mtu yeyote anayesambaza neno
la Mungu, huwa ni mtumishi wake. Neno zuri la Mungu husambazwa kupitia
mihadhara, misa, maombi na hata nyimbo kama Flora Mbasha anavyofanya.
Leo nikiambiwa niwataje waimbaji wa Injili kumi bora nchini, jina la
Flora Mbasha litakuwa katikati yao, likigawa kundi moja juu yake na
lingine chini yake. Hii ni kwa sababu ni mmoja wa waimbaji wazuri wa
muziki huu. Hujisikia furaha ninaposikiliza ujumbe uliomo katika nyimbo
zao, ingawa baadhi ya kazi zake huchezeka, lakini ujumbe wake maridhawa
hubakia kuwa fumbo.
Familia ya watu wa muziki wa Injili nchini, imepata mshtuko mkubwa
wiki chache zilizopita, baada ya waimbaji, ambao ni wanandoa, Emmanuel
na Flora Mbasha kupamba vichwa vya habari baada ya kutokea mzozo wa
kifamilia kati yao, ambao unadaiwa kusababisha mwanaume kupandishwa
kizimbani kwa tuhuma za ubakaji.
Sitaki kuzungumzia suala lililopo kortini kwa sababu sheria
zinakataza, isipokuwa nataka kuzungumza na mdogo wangu Flora kwa sababu
alichokifanya katika kipindi chote cha mtafaruku baina yao, hakikupaswa
kufanywa naye hasa kwa jinsi alivyofanikiwa kujitengenezea taswira ya
kuheshimika mbele ya jamii.
Huwa najaribu kusema mara nyingi, ustaa ambao baadhi yetu hatulali
kwa kuutafuta una gharama kubwa. Ukishakuwa mtu maarufu, unajinyima
baadhi ya haki zako za msingi, kama vile masuala yako binafsi kubaki
kuwa ya kwako.
Ninafahamu Flora, kama mke ana haki ya kukataa baadhi ya mambo
kufanyika katika ndoa yake. Sisi tulio katika ndoa tunafahamu, kuna
maisha magumu kweli, wakati mwingine mume na mke huweza kukaa hata mwezi
mzima bila kuzungumza, lakini kwa sababu ya kuhifadhi matatizo yenu
yasitoke nje, mnakaa kimya.
Akija jirani, hawezi kujua kama hamzungumzi kwa namna mtakavyompokea kwa bashasha na kumpa ushirikiano.
Kama kukaa kimya ili mambo hayo yaishe yenyewe kimyakimya mnashindwa,
kinachotokea ni kuwafuata ndugu wa karibu, ambao mara nyingi huwa ni
wale waliowazidi umri. Mnapeleka tatizo lenu, mnaitwa, mnajadiliana kwa
pamoja, mnaondoka na muafaka!
Haya mambo yangeweza kufanywa na Flora, hasa kwa kuwa jamii
inamtambua kama mtu mwenye woga na Mungu. Sasa kama mtu anayetakiwa kuwa
mfano, anaondoka nyumbani kwake na kwenda kusikojulikana, tena wakati
mumewe akiwa katika matatizo, unataka watu wakutazame kwa macho yapi?
Sitaki kusema nani mwenye makosa kati yao, ninachotaka kusema ni
kitendo cha Flora kuifanya jamii ione ni kama anayefurahia matatizo
yanayomzonga mumewe. Hii siyo sawa, hata kama ndani hatuongei, nje sisi
ni kitu kimoja.
Wakati akiwa madarakani, Rais wa Marekani, Bill Clinton aliwahi
kukutwa na tuhuma za kumbaka mfanyakazi wa Ikulu, Monica Lewinsky.
Katika kipindi chote cha sakata hilo, mkewe Hilary, alikuwa upande wake,
hakumuacha, alikuwa tayari kufa naye, kuliko kuongeza petrol kwenye
moto. Nani anajua waliishije wakiwa chumbani kwao?
Flora anatakiwa kutambua kuwa kuna ndoa chache sana zinaishi kwa upendo kama tunavyoziona.
Kitu kikubwa tunachopaswa kufanya, hasa kwa mastaa ni kuzilinda ndoa zetu kwa mikono yetu wenyewe.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment