Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limemtia mbaroni
bilionea Ally Edha Awadhi ambaye ni mmiliki wa Kampuni ya Lake Oil ya
Mikocheni jijini Dar es Salaam kutokana na madai ya kumtesa mfanyakazi
wake.
Akizungumza na waandishi wa habari hii ofisini kwake wiki iliyopita,
Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kanda Maalum ya Dar, ACP Jafari
Mohamed Ibrahim aliyezungumza kwa niaba ya Kamanda wa kanda hiyo, CP
Suleiman Kova alisema kwamba bilionea huyo na wafanyakazi wake
wanaotuhumiwa kumteka, kumtesa na kumdhalilisha na kumpora mali mmoja wa
wafanyakazi wake (jina linahifadhiwa kwa sababu za kiusalama)
walikamatwa na jeshi lake.
“Watuhumiwa wote walikamatwa hivi karibuni na kuhojiwa kisha wakapewa
dhamana na upelelezi wetu umekamilika ambapo jalada hilo tumelipeleka
Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka (DPP) lakini lilirudishwa polisi kwa
sababu kulikuwa na upungufu, akaagiza lifanyiwe kazi tena,” alisema
Kamanda Ibrahim.
Aliongeza kuwa baada ya jalada kurudi mikononi mwake alimtafuta
mlalamikaji kwa njia ya simu akiwa Mwanza ili aje ahojiwe upya lakini
hajaonekana hali iliyofanya alipeleke makao makuu ya jeshi la polisi
katika Ofisi ya Mkurugenzi wa Makosa ya Jinai (DCI).
“Ukitaka kupata habari zaidi nenda makao makuu ya polisi jalada la kesi hiyo liko huko,” alisema kamanda huyo.
Waandishi wetu walikwenda makao makuu ya jeshi hilo kumuona Mkuu wa
Jeshi la Polisi Tanzania, IGP Ernest Mangu (pichani), lakini
wakaelekezwa kumuona msemaji wake, Advera Senso ambaye alisema upelelezi
wa kesi hiyo unaendelea.
Mlalamikaji wa kesi hiyo ambaye anadai kuteswa na kudhalilishwa
aliamua kumwandikia barua ya malalamiko Waziri Mkuu Mizengo Pinda akidai
kuwa mwenendo wa kesi yake hauendi vizuri hali iliyomfanya waziri mkuu
aliagize jeshi la polisi kulifanyia kazi suala hilo ili haki itendeke.
Waandishi walienda ofisi ya waziri mkuu kutaka kujua kama kuna majibu
ya agizo alilolitoa lakini cha kushangaza hakuna majibu yoyote
yaliyopelekwa na jeshi la polisi kwa kiongozi huyo kwa mujibu wa maofisa
wa ofisi hiyo.
Mwandishi wa Habari wa Waziri Mkuu, Irene Bwire alipoulizwa kuhusiana
na sakata hilo, hakuwa na jibu la kuridhisha akaahidi kulifuatilia ili
kujua limefikia wapi.
Mlalamikaji huyo anadai kufanyiwa unyama huo Mei 2, mwaka jana na
kutoa taarifa Kituo cha Polisi cha Oysterbay, Mkoa wa Kipolisi Kinondoni
lakini akadai hakuna kilichofanywa na jeshi hilo badala yake amekuwa
akipata vitisho vya mauaji jambo linalomfanya aishi kwa kujificha.
Baadhi ya mambo aliyoyalalamikia mlalamikaji ni kupigwa na kujeruhiwa,
kudhalilishwa na kudhulumiwa mali zake na mwajiri wake huyo.
Alizitaja baadhi ya mali hizo kuwa ni pamoja na nyumba, magari yake
mawili ambayo ni Toyota lenye namba za usajili T 786 BZG na Toyota
Fortuner namba T503 BQC, bastola, fedha taslim dola za Kimarekani
100,000, maduka na ofa zake tatu za viwanja huko Kigamboni.
Katika barua aliyompelekea waziri mkuu, mlalamikaji alidai kufanyiwa
unyama huo na Awadhi kwa kushirikiana na mabaunsa pamoja na baadhi ya
wafanyakazi wake katika chumba maalum wakimtuhumu kuiba dola za
Kimarekani milioni 10.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment