MTOTO
Marisela Karoli (14) amewaomba wanaharakati wa masuala ya haki za watoto
kumsaidia ili arudi shuleni badala ya kuolewa kama anavyolazimishwa na
mama yake mzazi, Yohana Binde.
Akizungumza
nyumbani kwa msamaria mwema aliyemhifadhi, mtoto huyo alisema alitoroka
kijijini kwao Idindiri, Tarafa ya Pahi, wilayani Kondoa, Dodoma
akikwepa kuolewa.
Mtoto
huyo aliyekuwa anasoma darasa la tano katika Shule ya Msingi Idindiri,
alisema mama yake mzazi alipokea mahari ya sh 600,000 kutoka kwa
mwanaume anayetaka kumwoa, aliyemtaja kwa jina la Christian Dodi.
“Mwezi
wa tano walikuja nyumbani kuleta barua ya posa, mama akanilazimisha
kuipokea, akasema nikikataa atanipiga. Nikaipokea, walipoondoka nikampa
mama, ndani ya ile bahasha kulikuwa na sh 25,000.
“Mwezi
uliopita (Juni) walikuja nyumbani kuleta mahari sh 600,000 mama
akapokea,” alisema na kuongeza kuwa Alhamisi ya Juni 12 mama yake
aliwapeleka hospitali ya misheni kupima afya halafu wakaingia parokiani
kuandikisha ndoa, lakini Padri Kalani wa Parokia Katoliki ya Kinyasi,
alikataa kuandikisha ndoa hiyo kwa kuwa yeye (Marisela) ni mdogo.
Kwa
mujibu wa Marisela, baada ya mama yake kuona ndoa haitangazwi, alimtaka
aende akaishi na mwanaume huyo hadi atakapokua, ili aolewe.
Alisema
Juni 22 wakati wadogo zake wakipata Ekaristi katika parokia hiyo,
alitoroka na kwenda Kijiji cha Keikei anakoishi bibi yake mzaa mama
aitwaye Maria Vicent ambapo alilala na kutoroka alfajiri ya Juni 23.
“Niliamka
saa 11 alfajiri nikatoka nje kama nakwenda kujisaidia, nikakimbilia
barabarani, likapita basi la Ibony nikapanda. Sikuwa na nauli,
nikamwambia kondakta anisaidie nauli yangu atapewa na dada yangu anaishi
huku (Dar),” alisema Marisela ambaye ni mtoto wa pili kati ya sita wa
mama yake mzazi.
Alisema
baada ya mama yake kugundua ametoroka, alimtuma mtu kumfuata, jambo
alilokataa na kukimbilia mafichoni huku akisisitiza kwamba anahitaji
zaidi kusoma.
Marisela
anayeishi mafichoni kwa sasa, alitumia fursa hiyo kuwaomba wananchi
wenye nia ya kumsaidia ili arudi shule wafanye hivyo.
Na Irene Mark
No comments:
Post a Comment