MTOTO wa
kike mwenye umri wa siku moja amenusurika kufa baada ya kuokolewa na
wasamaria kutoka katika shimo alimotupwa na mama yake mzazi.
Imeelezwa kuwa mwanamke huyo alifanya hivyo ili kulinda ndoa yake changa, kwa kuwa mumewe hakuwa mhusika wa ujauzito huo.
Taarifa
za tukio hilo zimethibitishwa na Mwenyekiti wa Serikali ya kijiji cha
Rwabigaga, Fron Nestory. Alisema tukio hilo ni la usiku wa kuamkia
Jumapili iliyopita katika kijiji cha Rwabigaga kata ya Kamuli wilayani
Kyerwa.
Alidai
siku hiyo ya tukio, mwanamke huyo, Jane Leonard alijifungua salama mtoto
wa kike, lakini baadaye akamwambia mama mkwe wake, kuwa mtoto amepotea
katika mazingira ya kutatanisha.
Nestory
alisema kutokana na taarifa hizo, juhudi za kumsaka mtoto zilianza na
ilipofika asubuhi wamlikuta mtoto huyo kwenye shimo, akiwa amefunikwa
kwa maganda ya maharage na tayari siafu na wadudu wengine, walikuwa
wameanza kumshambulia.
Alisema
jitihada za kumuokoa mtoto huyo zilifanyika, ambapo baada ya kumuosha
alipelekwa katika Kituo cha Afya Kamuli na kupatiwa huduma. Kwa sasa
anaendelea vizuri na tayari amekabidhiwa kwa mama yake mzazi.
Kwa
upande wake, mama mzazi wa mtoto huyo alisema alifanya hivyo, kutokana
na hofu ya kuvunjika kwa ndoa yake changa, kwani imepita miezi miwili tu
tangu aolewe.
Ingawa
hakutaka kuingia kwa undani, imeelezwa hofu yake imetokana na ukweli
kwamba, ameingia katika ndoa mpya akiwa mjamzito, ilhali mumewe wa sasa
si mhusika.
Hata
hivyo, Nestory aliwataka wananchi kuwa na hofu ya Mungu na kuacha
vitendo vya unyanyasaji na ukatili kwa watoto, kwani mtoto ni tegemeo la
taifa kwa ujamla.
Kamanda
wa Polisi mkoani Kagera, Henry Mwaibambe alisema tukio hilo
hajalipata;na alisema ameagiza polisi wilayani Kyerwa, kufuatilia zaidi
na kumpa taarifa juu hilo.
No comments:
Post a Comment