SAKALA JUU YA GARI LA DUDE: MASALA MAPYA YAIBUKA

Kumbe! Lile gari aina ya Toyota Vitz la staa wa sinema za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’ ambalo hivi karibuni lilikamatwa kwa msala wa kuhusika na ujambazi jijini Dar, limeibua mapya likiwa bado linashikiliwa na polisi kwenye Kituo cha Kijitonyama a.k.a Mabatini.
Gari aina ya Toyota Vitz la staa wa sinema za Kibongo, Kulwa Kikumba ‘Dude’.
Habari za kifukunyuzi zinadai kwamba ndinga hilo si mali ya Dude kama ilivyoelezwa awali, bali ni la mwanamke ‘anayechepuka’ naye aliyetajwa kwa jina moja la Lily ambaye eti ni mke wa mtu (Samson).
Akizungumza na mwanahabari wetu kwa njia ya simu kutoka Meatu mkoani Simiyu, Samson ambaye ni mume wa Lily alisema alistaajabu aliposikia Dude akisema gari ni lake wakati ni la mkewe aliyefunga naye ndoa mwaka 2011 na yeye alishiriki kulinunua.

“Huyo Dude anajua ukweli wa mambo, gari si lake, ni la mke wangu tena fedha ya kulinunulia haikutosha ikabidi nimuongezee laki nne kwa kuwa alikuwa akidaiwa kwa usumbufu mkubwa.
“Isitoshe katika vijana waliokamatwa na gari hilo, mmoja ni mdogo wa mke wangu na siri zote za yeye kutoka na Lily huwa ndugu zake wananisimulia.

“Mara kadhaa nimemuonya Dude lakini huwa anakana kuwa hatoki naye bali ukaribu wao ni kutokana na sanaa na kudai ni kama ndugu kwa kuwa alikuwa akijuana na mama yake,” alisema.
Baada ya madai hayo kuwa ‘hoti’, Ijumaa Wikienda lilimsaka Lily ambaye hakuwa tayari kuzungumza kama gari hilo ni lake au la Dude na kusisitiza aulizwe Dude ambaye alikiri kufahamiana naye huku akikubali kumfahamu Samson pia.

Kulwa Kikumba ‘Dude’ akiwa ndani ya ofisi za Global.
Ili kupata mzani wa habari hiyo, Ijumaa Wikienda lilimvutia waya Dude aliyekiri kuwafahamu Samson na Lily kuwa ni wanandoa japokuwa wana migogoro.
“Matatizo yao ya ndoa wasihamishie kwangu, gari ni langu na lilikuwa linauzwa, Lily nimemlea kisanii maana marehemu mama yake mzazi nilikuwa namuita dada, ndiye aliyenikabidhi Lily mwaka 2003.
“Nimejaribu kumsaidia kisanii, sitaki kuchafuka, Lily ni mwanangu nimemlea,” alisema Dude.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger