Wachumba wa muda mrefu, staa wa sinema za Kibongo, Rose Donatus
Ndauka na Malick Bandawe ambao maisha yao ya kimapenzi yamekuwa
yakitawaliwa na msuguano wa chini kwa chini, hatimaye wameachana, Ijumaa
Wikienda linakupa mkanda mzima.
TUJIUNGE NA CHANZO
Chanzo makini na cha uhakika
kimemwaga data kwamba wachumba hao ambao walivalishana pete kwa mbwembwe
miaka mitatu iliyopita huku wakipika na kupakua lakini wamekuwa katika
mzozo wa muda mrefu wa kifamilia, ambapo mara kadhaa wameripotiwa
kuchapana wameachana.
“Unajua hawa jamaa wamekuwa na maisha ya
kutoaminiana sana, nadhani wivu ndiyo sababu kubwa, lakini naona safari
hii hali imekuwa mbaya zaidi kwa sababu Rose ameamua kubeba kilicho
chake na kuondoka kwa mwenzake,” kilisema chanzo hicho na kuongeza:
“Hiyo ndiyo habari ya mjini, bidada karudi kwao (Kigogo, Dar) na
mwanaye. Ilikuwa ni lazima ndoa isiwepo kwani licha ya kupata mtoto
hakukuwa na furaha hata kidogo.”
TATIZO NI NINI?
Ingawa chanzo hicho hakikuweza
kuingia kwa undani kuhusu tatizo hasa lililotokea safari hii, lakini
kilibainisha kwamba kabla ya tukio la sasa, mzozo mwingine mkubwa
uliibuka kati yao.
“Kuna kipindi hali ilikuwa tete sana, Malick
akaamua kuchukua mabegi yake na kutokomea kusikojulikana ambako alikaa
kwa muda wa kama wiki mbili.
“Haikujulikana alikuwa wapi kwa muda wote huo, lakini baadaye tukamuona jamaa anarudi na maisha yao yakaendelea.
NDOTO YA NDOA YAYEYUKA
“Lakini wakati bado mambo
hayajatulia, kumeibuka tatizo lingine kubwa ambalo limesababisha Rose
kuamua kuondoka huku ndoto ya ndoa ikiyeyuka,” kilisema chanzo hicho.
VIPI KUHUSU MTOTO?
Katika mtafaruku huo, Malick
alikataa katakata mtoto wake kuondoka na mama yake, lakini kutokana na
umri wa mwaka mmoja wa kijana wao huyo, Naveen, alilazimika kuondoka na
mama yake kwa vile bado ananyonya.
Rose, mmoja kati ya waigizaji warembo wa filamu Bongo, inasemekana
kwamba yupo nyumbani kwa wazazi wake, Kigogo kutoka kwa mchumba wake,
anayeishi Tandale, Tanesco jijini Dar.
IJUMAA WIKIENDA MZIGONI
Baada ya kunyetishiwa
‘ubuyu’ huo, Ijumaa Wikienda lilizama mzigoni ambapo stepu ya kwanza
ilikuwa ni nyumbani walikokuwa wakiishi wapenzi ambapo hawakuwepo.
JIRANI ANASEMAJE?
Akizungumza na gazeti hili juu
ya kuondoka kwa Rose nyumbani hapo, mmoja wa majirani zake
aliyejitambulisha kwa jina moja la Sudi alikuwa na haya ya kusema:
“Rose Ndauka ana muda hatumuoni kama miezi sasa lakini ‘mista’ tunamuonaona labda kama amehama ‘but’ sina uhakika sana.”
ROSE VIPI?
Katika kutafuta ukweli alitafutwa
Rose kila kona baada ya simu yake ya kiganjani kutokuwa hewani lakini
jitihada ziligonga mwamba hivyo zinaendelea.
BOFYA HAPA KUMSIKIA MALICK
Mchumba mtu, Malick
alipoulizwa juu ya ukweli wa sakata hilo, alikiri kutokea na kwamba
baada ya jitihada zake nyingi za kulinusuru penzi lao kushindikana,
amekubali matokeo.
“Nimejitahidi sana kumwelewesha Rose ili apate
kunielewa, ajue namna ya maisha yalivyo, lakini imekuwa ni kama kutwanga
maji kwenye kinu. Nimekubali yaishe.
“Kinachonisikitisha sana ni kuona kuwa mwanangu anakwenda kulelewa na
mwanaume mwingine, inauma sana tena sana,” alisema bila kufafanua maana
ya kauli hiyo.
Katika uchumba wao mrefu, Rose na Malick wamejaliwa mtoto mmoja wa kiume aitwaye Naveen.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment