KIFO CHA NGWEA BADO NI UTATA....PICHA YAKE AKIWA MOCHWARI IMEIBUA MASWALI MENGI YANAYOHITAJI UCHUNGUZI WA KINA.

KIFO cha msanii wa Hip Hop Bongo, Albert Kenneth Mangwea a.k.a Ngwea au Mangwair kilichotokea Jumanne wiki hii jijini Johannesburg, Afrika Kusini ‘Sauzi’, kimeendelea kuwagawa Watanzania katika makundi na kusababisha utata, Ijumaa linakuhabarisha

Kwa mujibu wa ripoti za awali za tukio hilo, Ngwea na mwenzake M 2 the P walizimika wakiwa usingizi ambapo wote walikimbizwa kwenye chumba cha wagonjwa mahututi (ICU) katika Hospitali ya St. Helen Joseph nchini humo.
Ilidaiwa kuwa katika harakati hizo ilithibitika kwamba Ngwea alishafariki dunia huku mwenzake akiwa hoi bin taaban.
Hata hivyo, hospitali hiyo haikueleza chanzo cha kifo hicho kwa sababu ya kusubiri uchunguzi wa mwili wa marehemu.
Habari za kifo cha msanii huyo zilisambaa kwa kasi katika mitandao ya kijamii huku kila mtu akisema lake juu ya tukio hilo baya kwenye ulimwengu wa mastaa Bongo.
Ilisemekana kuwa kabla ya kukutwa na mauti, staa huyo wa ngoma ya Mkasi alikuwa nchini humo kwa ziara za kimuziki ambapo Jumanne iliyopita ndiyo ilikuwa arejee Bongo.


MADAI MAZITO KUTOKA SAUZI
Katika tukio hilo lililowagawa Watanzania, baadhi ya watu walidai kuwa inawezekana staa huyo aliuawa ili adhulumiwe mzigo wa ‘unga’ na watu waliokuwa wamempa tenda ya kuufikisha nchini humo huku wengine wakisema walijiovadozi na pombe kali.
“Katika hali ya kawaida inawezekanaje watu wawili wakajiovadozi kwa wakati mmoja? Kama ni ulevi, huo ni ulevi wa aina gani? Haiwezekani watu walewe sawa kisha wazimike sawa.
“Hapa kuna dalili ya kuwepo kwa  mchezo mchafu. Kifo cha Ngwea kina harufu ya kudhulumiana kwenye mzigo, si unajua siku hizi ndizo dili za baadhi ya wasanii wetu?” alidai Baba P kwenye mtandao wa Twitter.

ALIJIDUNGA MADAWA YA KULEVYA?
Madai mengine mazito ni kwamba eti wawili hao walijidunga madawa ya kulevya ambayo inasemekana yalikuwa feki au famba kama wanavyosema watu wanaodili na unga.
Kuhusu hilo ilidaiwa kuwa huenda unga waliokutana nao siku hiyo ulikuwa ‘kitu orijino’ tofauti na ule wa Kinondoni, Dar hivyo dozi iliwazidi.
Iliendelea kusemekana kuwa ukijiovadozi ‘kitu cha Sauzi’ huwa mtumiaji anagonga ‘kick’ kama wanavyosema watumiaji ambapo kitaalam huweza kusababisha kusimama ghafla kwa mapigo ya moyo kisha kifo.

KUZIDISHA BANGI?
Wapo waliodai kuwa huenda jamaa hao walizidisha matumizi ya kilevi cha bangi ambapo mjadala ulikuwa mkubwa, wengi wakihoji kama kuna uwezekano wa kilevi hicho kusababisha kifo.
“Nijuavyo mimi mtu akivuta bangi sana huweza kupata madhara katika ubongo lakini siamini kama inaweza kuua,” alisema Juma Kisaki akichangia juu ya kifo hicho mtandaoni.

ALILALA, ASUBUHI HAKUAMKA
Kwa mujibu wa watu waliokuwa na Ngwea katika nyumba aliyofikia kwa rafiki yake, jamaa huyo alilala vizuri lakini cha ajabu asubuhi hakuamka kama walivyopanga kwani alikuwa asafiri siku hiyo kurudi Bongo.
“Inawezekanaje mtu alale bila tatizo halafu afe usingizini? Kwa vyovyote kuna kitu. Au labda walipuliziwa sumu chumbani? Kwani hakukuwa na watu wengine ambao waliamka salama? Kweli ni utata juu ya utata,” aliandika Anonymous kwenye mtandao wa Twitter.

KWA NINI UTATA?
Ni utata kwa sababu hakuna uhakika wa moja kwa moja kwamba nini kilichukua uhai wa msanii huyo maarufu Bongo matokeo yake kila mtu anasema lake.

MAMA MANGWEA ANASEMAJE?
Akizungumza na ripota wa Ijumaa mjini Morogoro, Dustan Shekidele, mama mzazi wa Ngwea, Denisia Mangwea (63), alisema kitendo cha mwanaye huyo kumuahidi kwenda Morogoro kulifanyia ukarabati kaburi la marehemu baba yake kitabaki kichwani mwake kwa muda mrefu.
Akiwa nyumbani kwake Kihonda, Mazimbu Road, mama huyo alisema siku za karibuni aliongea na mwanaye kwa njia ya simu na kumuahidi kwenda Moro kulifanyia ukarabati kaburi la baba yake, marehemu Kenneth Mangwea.
”Albert aliniambia angekuja Morogoro wiki ijayo baada ya kutoka Afrika Kusini, leo (Jumatano) naambiwa naletewa maiti ambayo tutaizika jirani na kaburi la baba yake?” alihoji na kuangua kilio.
Mama huyo alisema kuwa Ngwea ni mwanaye wa sita na wa mwisho aliyemzaa mwaka 1982 ambaye hajawahi kumwambia kama ana mchumba au mtoto.

HALI YA DAR
Tofauti na Morogoro ambako watu walikuwa wamekusanyika nyumbani kwa wazazi wa marehemu, jijini Dar baadhi ya waombolezaji walionekana kuhangaika kutafuta sehemu ulipowekwa msiba wa msanii huyo.
Watu wengi walifika nyumbani kwa marehemu Sinza-Mori na wengine kwenda kwa kaka yake, Mbezi.
Hata hivyo, ilibainika kuwa kabla ya mwili wa marehemu kupelekwa Morogoro, utafikishwa Mbezi kwa kaka yake kisha kuelekea Morogoro kwa mazishi.
Wakati hayo yakiendelea, baadhi ya wasanii wa kada mbalimbali walikusanyika kwenye Viwanja vya Leaders, Kinondoni, Dar kujipanga namna ya kuchangia chochote katika msiba huo wakati wakisubiri mwili uwasili kutoka Sauzi.

HALI YA MWILI WA MAREHEMU
Ijumaa lilifanikiwa kupata picha ya mwili wa marehemu. Kwa kuutazama tu alitokwa na damu puani na masikioni wakati akikata roho.

POMBE KALI ZAKUTWA CHUMBANI
Ilidaiwa kuwa ndani ya chumba alicholala Ngwea kulikuta bapa (chupa) mbili za pombe kali aina ya Vodka hali iliyowafanya baadhi ya watu kuamini pombe zilichangia kusindikiza kifo hicho.

RIPOTI FEKI YASAMBAA MTANDAONI
Katika hali ya kushangaza, juzi baadhi ya mitandao iliweka ripoti inayodaiwa ni feki.
Katika ripoti hiyo, ‘madaktari’ waliouchunguza mwili wa Ngwea walibaini kwamba kabla ya kifo chake yeye na mwenzake walizidisha kileo na unga.
Pia wawili hao eti hawakuwa na mpangilio mzuri wa chakula kwa maana kwamba walikuwa wakinywa pombe kali bila kupata msosi wa nguvu kama ‘nyama choma’.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger