Ingawa tendo la ndoa lisipofanywa kwa kuzingatia kanuni na taratibu,
sambamba na umakini, linaweza kusababisha maradhi, lakini kwa wanandoa,
tendo hilo linatajwa kuwa na manufaa mengi kiafya tofauti na faraja ya
kawaida iliyozoeleka kwa wengi.
Imefahamika kuwa tendo hili likifanyika ipasavyo husaidia kuondoa
msongo wa mawazo, maradhi ya moyo, maumivu ya kichwa yasiyokoma na
kupunguza kasi ya saratani ya tezi dume.
Mhadhiri Mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Sayansi ya Tiba Muhimbili
(Muhas), Dk Yahya Kishashu anasema inategemea tendo linafanywa na nani
na mhusika yupo kwenye mazingira gani.
“Kwa mfano, tendo la ndoa linaondoa msongo wa mawazo iwapo unayetenda
naye unampenda na amekupa maandalizi mazuri. Sidhani kama alimradi
utende hilo tendo na yeyote litakusaidia,” anasema mtaalamu huyo.
Anaongeza kuwa ndiyo maana baadhi ya watu wanatoka nje ya ndoa zao
kwa sababu si mara zote tendo la ndoa linawafurahisha wanandoa.
“Wakati mwingine tendo hilo laweza kuwa karaha kwao,” anasema
Mazoezi
Si hivyo tu, utafiti uliofanyika Canada hivi karibuni umebainisha
kuwa kufanya tendo la ndoa kwa kipindi cha dakika 25 kwa wanamume
kunachoma kalori 100 na kwa wanawake kalori 69.
Tendo hilo likifanyika kwa nusu saa, linaweza kupunguza kalori za
mwili kuliko kutembea kwenye mashine ya mazoezi ya ‘treadmill’.
“Ni sawa na kucheza mpira wa tenisi au kutembea ukipanda mlima kwa
dakika 20 au kucheza gofu kwa kasi kwa dakika 33 au zoezi la yoga kwa
dakika 40,” sehemu ya utafiti hiyo inasema.
Utafiti huo wa Canada ulishabihiana na kampeni iliyofanywa na
Taasisi ya Moyo ya Uingereza ambayo ilisema kuwa dakika 30 za tendo la
ndoa kwa siku ni muhimu kama mazoezi ya kutembea kwa mashine.
Kwa undani zaidi utafiti huo ulichambua na kusema kuwa, tendo la ndoa, lina manufaa kwa moyo na mapafu.
Inaelezwa kuwa vichocheo vinavyotoka baada ya tendo la ndoa
vinasaidia kupunguza kiwango cha msongo wa mawazo na kuongeza
uzalishaji wa seli mpya za ubongo.
Kuhusu mazoezi, Dk Kishashu anasema anakubaliana na utafiti huo na
kusema kuwa ni kweli tendo hilo linasaidia kupunguza kalori, lakini
linapofanyika mara nyingi zaidi linazeesha.
Hata hivyo, wanasayansi wanalipa uzito mdogo tendo hilo katika
muktadha wa ujenzi wa hisia na mwili na kuwa halisisitizwi vya kutosha
kama aina mojawapo ya mazoezi.
Tiba kwa moyo, mapafu na ubongo
Inaelezwa kuwa tendo la ndoa, linasaidia kuondoa msongo wa mawazo hivyo kupunguza hatari ya maradhi ya moyo.
Si hivyo tu, bali tendo hilo husaidia mapafu kufanya kazi yake vyema, kuingiza na kutoa hewa chafu.
Kitaalamu, upo mchakato uitwao ‘Neurogenesis’ ambao husaidia kulinda
seli za ubongo zinazokufa kutokana na uzee. Kuna eneo kwenye ubongo
linaloitwa ‘hippocampus’ ambalo ni eneo linalotengeneza kumbukumbu.
“Kazi kubwa inafanyika kwenye ubongo, wakati wa tendo la ndoa, kiasi
kikubwa cha viamsha raha huanzia kwenye ubongo na kuleta taarifa kwenye
maeneo mengine ya mwili.
Ndiyo maana watu wengi hupotea kiufahamu wakati wa kilele” anasema Dk Gosh, ambaye ni mtafiti.
Hata hivyo, wanaume ambao wanaendelea na tendo la ndoa mara kwa mara
hadi wanapofikisha miaka 50 na zaidi, kwa maana ya kutoa mbegu za kiume
mara kumi kwa mwezi, wapo katika hatari ndogo ya kupata saratani ya tezi
dume. Inaelezwa kuwa mbegu za kiume hazitakiwi kukaa mwilini kwa muda
mrefu.Zinatakiwa zitolewe mara kwa mara ili kuzifanya seli mpya
zizalishwe. Ni kama kusafisha mpira, inasaidia kusitisha ujenzi wa seli
za zamani ambazo zaweza kuwa chanzo cha saratani.
Kwa wanawake, tendo la ndoa husaidia kuundwa kwa misuli ya nyonga
ambapo misuli hiyo ikiwa imara huondoa hatari ya kushindwa kuzuia
mkojo,(urine incotinence) jambo linaloathiri mwanamke mmoja kati ya
wanne wenye umri wa miaka zaidi ya 50.
“ Wakati wa tendo la ndoa, kwa kawaida sakafu ya nyonga za mwanamke
hubana na kuachia. Hii husababisha misuli hiyo kuwa imara’ anasema
mtafiti huyo.Hata hivyo, utafiti wa Chuo Kikuu cha Nottingham nchini Uingereza unaeleza kuwa, wanaume wanaofanya tendo hilo na kumwaga mbegu mara 20 hadi 30 kwa mwezi, wapo katika hatari ya kupata saratani ya tezi dume kwa sababu ya umri wao .
Kuondoa maumivu ya kichwa
Utafiti mwingine umebaini kuwa, wanawake wenye umri mdogo hukumbwa na
msongo wa mawazo iwapo hawatafanya tendo la ndoa kwa muda mrefu.
Wanawake hao, wanapofika kilele cha tendo hilo, damu hutembea kutoka kwenye ubongo, jambo ambalo huondoa maumivu ya kichwa.
Dk Innocent Mosha, Mchunguzi wa magonjwa wa Hospitali ya Taifa
Muhimbili anasema kuwa inawezekana kuwa tendo la ndoa likasaidia
kuondoa msongo wa mawazo iwapo mtu hajalifanya kwa muda mrefu na yupo
katika hali kubwa ya uhitaji.
“Kama mtu hajafanya tendo hilo muda mrefu na hivyo amelikamia, basi akilifanya litamwondolea msongo wa mawazo,” anasema
Anasema mtu ambaye anahitaji kufanya tendo hilo na hajalipata,
aghalabu huwa na msongo wa mawazo lakini kama huliwazi hawezi kuwa na
msongo.
Kwenye utafiti huo, wanawake 83 wenye maradhi ya kichwa walipata nafuu kubwa baada ya kumaliza tendo la ndoa.
Ukaribu/ upendo
Mwanasaikolojia, wa Chuo Kikuu cha Dodoma, Modesta Kimonga anasema
ni kweli kuwa tendo la ndoa linaleta faraja inayoondoa msongo wa mawazo.
Anasema hali hiyo inatokana na nadharia au mfumo wa uambatano katika saikolojia au ‘attachement theory’
“Hii ‘attachment theory’ ipo kwa watoto wanaponyonya maziwa ya mama
zao, na kwa watu wazima ni kwenye tendo la ndoa ambalo linaleta faraja
na ukaribu,” anasema.
Anaongeza: “Faraja hupatikana baada ya wanandoa kutenda tendo hilo na huweza kuondoa kabisa mawazo kichwani au huzuni.”
Watafiti walibaini kuwa vichocheo vya ‘oxtocin’ vinavyotolewa wakati
wa tendo hilo husaidia hisia za upendo na mshikamano kwenye uhusiano ya
muda mrefu.
Lipo ongezeko kubwa la kemikali ya ‘oxtocin’ kwa wanawake na wanaume
baada ya kumaliza tendo la ndoa ambalo husaidia kukuza uhusiano na
ukaribu wao.
Wanaume kulala baada ya tendo la ndoa
Utafiti wa jarida la Sayansi ya Mishipa ya Fahamu na Tabia
uliochapishwa mwaka 2012 umebaini kuwa, dawa za usingizi hufanya kazi
sawa na tendo la ndoa kwa wanaume.
Eneo la mbele la ubongo ‘pre –frontal cortex’, ambalo linahusiana
na ufahamu, au umakini wa kiakili, huzima au kufungwa baada ya kumaliza
tendo hilo.
Kwa baadhi ya utafiti, wanaume kumaliza tendo la ndoa, ni sawa na
kunywa dawa za usingizi za ‘diazepam’ zenye ukubwa wa miligramu mbili.
Pia, vichocheo vinavyotoka baada ya tendo hilo kama ‘melatonin,’
‘oxytocin’ na ‘vasopresin’, zinamsababisha mwanaume apate usingizi
mzito.
No comments:
Post a Comment