KIOJA! Kijana anayejulikana kwa jina moja la Emmanuel (30), amejikuta
akipokea kipigo ‘hevi’ baada ya kukamatwa akiiba katika Chuo cha
Theofilo Kisanji ndani ya Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania
(KKKT) Usharika wa Kijitonyama, Dar.
Tukio hilo lilitokea hivi karibuni kanisani hapo, mchana kweupe
ambapo jamaa huyo ambaye amekuwa akifika mahali hapo mara kwa mara,
alijikuta arobaini yake ikitimia na hivyo kutiwa mikononi mwa wanachuo
ambao kabla ya kuhoji zaidi, walimshushia kipigo cha mbwa mwizi.
“Huyu ndiye huwa anatuibia humu chuoni na kanisani, kila siku watu
wanalalamika kuibiwa vitu vyao. Juzi tu, kuna watu waliibiwa simu,
wengine fedha lakini hatukujua ni nani aliyekuwa akitufanyia hivyo, sasa
huyu tutamkomesha,” alisema dada mmoja huku akiwa na furaha ya
kukamatwa kwa jamaa huyo.
Wanachuo hao, wakionekana kupania kumfundisha adabu na kumwachisha
Emmanuel udokozi, walikuwa wakimhoji maswali huku wakimwangushia kipigo
mfululizo, hali iliyosababisha mwili kutoka damu nyingi iliyotapaa
sakafuni kama buchani.
Kama kawaida, mapaparazi wetu hawakutaka kuishia kuangalia kipigo tu,
waliwaita baadhi ya wanachuo walioibiwa mali zao na mashuhuda
waliomuona jamaa huyo akiiba na kueleza mchezo mzima ulivyokuwa.
“Nilikuja hapa chuoni saa tisa (alasiri) nikaelekea mapokezi na baadaye darasani.
Nilipofika hapo, nikamuona mtu akisimama ghafla, nikashtuka lakini
sikutaka kuwa na wasiwasi sana, nilidhani ni mwanachuo wa hapa,” alisema
msichana mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Adolphina na kuendelea:
“Nikaondoka hapo na kupanda juu (ghorofani). Moyo wangu ukawa mzito,
ghafla nikajikuta nikishuka ngazi na kurudi kule mapokezi. Nilipofika
mapokezi, yule mtu niliyemuona pale hakuwepo, nilipoanza kumtafuta,
nikaona akielekea getini kwa mwendo wa harakaharaka, hapo ndipo
nilipoanza kupiga kelele za mwizi, naye akaanza kukimbia mpaka
alipokamatwa,” alisema Adolphina.
Jamaa huyo alipopekuliwa begi alilokuwa nalo alikutwa na vyeti
mbalimbali vya shule ya sekondari ya mkoani Mbeya, cheti cha kuzaliwa,
cheti cha TRA na vyeti vingine vingi, vyote vikiwa si vyake.
Mbali
na vyeti hivyo, pia alikuwa na kadi za mashine za ATM zikiwepo za CRDB,
NMB na NBC, hali iliyoonesha kwamba huwa anazitumia kwa ajili ya
kuchukulia ‘mkwanja’ kutoka katika akaunti za watu.
Alipopekuliwa zaidi mifukoni mwake alikutwa na simu aina ya Huawei
yenye thamani ya shilingi 360,000 na Nokia Asha yenye thamani ya
shilingi 150,000, ambazo zote ziliibwa ndani ya chuo hicho siku chache
zilizopita.
Askari wa Kituo cha Polisi Kijitonyama – Mabatini ndiyo walimuokoa
jamaa huyo mikononi mwa wanachuo hao ambapo walifika eneo la tukio baada
ya kujulishwa na mmoja wa watu walioshuhudia jamaa huyo akisulubiwa kwa
hasira.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment