Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania
(TFF) na Kocha wa Taifa Stars, Kim Poulsen wamekubaliana kuvunja mkataba
katika makubaliano ambayo ni siri kwa pande zote mbili.
Uamuzi huo umetangazwa leo (Februari 27
mwaka huu) jijini Dar es Salaam kwa pamoja na Rais wa TFF, Jamal Malinzi
na Kocha Poulsen mbele ya waandishi wa habari.
Rais Malinzi kwa niaba ya TFF ametoa
shukrani za dhati kwa Kocha Poulsen kwa ushirikiano na mchango ambao
ameutoa kwa Tanzania kuanzia kwenye mpira wa miguu wa vijana.
Naye Kim amewashukuru Watanzania kwa
ushirikiano waliompatia kwa kipindi cha miaka mitatu alichokaa nchini
kuanzia Mei 2011 alipoteuliwa kuwa kocha wa timu za Taifa za vijana, na
baadaye Taifa Stars.
Akizungumzia benchi jipya la ufundi la
Taifa Stars, Rais Malinzi amesema linatarajiwa kutangazwa hivi karibuni
likiongozwa na kocha kutoka nje ya Tanzania.
Amesema kwa upande wa mechi dhidi ya
Namibia itakayochezwa Machi 5 mwaka huu jijini Windhoek, Stars
itaongozwa na Kaimu Mkurugenzi wa Ufundi, Salum Madadi akisaidiwa na
kocha Hafidh Badru kutoka Zanzibar.
Katika hatua nyingine, Kocha Madadi
amewaondoa wachezaji watano wa Yanga katika kikosi kilichotajwa awali
ili wapate fursa ya kuitumikia timu yao kwenye mechi mbili za Ligi ya
Mabingwa Afrika dhidi ya Al-Ahly ya Misri.
Wachezaji hao ni Athuman Idd, David
Luhende, Deogratius Munishi, Frank Domayo, Kelvin Yondani na Mrisho
Ngasa. Pia kipa Ivo Mapunda ameondolewa katika kikosi hicho baada ya
kupata msiba.
Nafasi zao zimezibwa na wachezaji Abdi
Banda (Coastal Union), Himid Mao (Azam), Juma Luizio (Mtibwa Sugar),
Said Moradi (Azam) na Shabani Kado (Coastal Union).
Taifa Stars itaingia kambini keshokutwa
(Machi 1 mwaka huu) jioni kwenye hoteli ya Accomondia jijini Dar es
Salaam, na itaondoka Machi 3 mwaka huu alfajiri kwa ndege ya South
African Airways na kurejea nchini Machi 7 mwaka huu saa 8.15 mchana.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment