SIKU chache baada ya kulipuka kwa kitu
kilichosadikiwa kuwa ni bomu kwenye Kanisa la Kiinjili la Kilutheri
Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Kaskazini Mashariki ya Ziwa Victoria,
Makongoro Misheni, Mwanza, wananchi wameendelea kuishi kwa hofu kwa
kutokea mlipuko mwingine.

Kufuatia mlipuko huo,
imeelezwa kuwa wakazi wa Mwanza hususan waumini wa kanisa hilo wamekuwa
wakiishi kwa hofu kwani wanaamini kuwa aliyekuwa ametega bomu hilo
alikuwa na lengo la kuangamiza watu wengi kwa wakati mmoja.
Wakizungumza na mwandishi wetu kwa sharti la kutochorwa majina yao
gazetini, wakazi wa Makongoro Misheni wamesema hawana imani na mtu
aliyetega bomu hilo kama atakuwa na lengo la kutimiza azima yake
aliyokuwa ameipanga au atashindwa kutokana na ulinzi mkali wa jeshi la
polisi ulioimarishwa.
“Tunaishi kwa mashakamashaka maana hatujui aliyetega bomu lile
alikuwa na lengo gani kwetu, kitendo cha kulitega bomu hilo kanisani
kinaashiria mtu huyo alikuwa na lengo wa kuangamiza watu wengi kwa
wakati mmoja,” alisema mmoja wa wakazi hao.
Aidha, mwingine aliomba jeshi la polisi kuendesha msako mkali
kuhakikisha mtuhumiwa wa bomu hilo anakamatwa na kufikishwa katika mkono
wa sheria.
“Tunaomba polisi watusaidie kuendesha msako mkali ili mtuhumiwa
apatikane na kufikishwa mahakamani ili na sisi tuwe na imani ya
kuabudu,” alisema.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Valentino Mlowola alisema uchunguzi
wa awali unaonesha bomu hilo lilitengenezwa kienyeji na uchunguzi
unaendelea ili kuwabaini walioliweka kanisani hapo.
No comments:
Post a Comment