RAMADHANI Masanja ‘Banza Stone’ ni mwanamuziki mkubwa wa muziki wa dansi la kileo. Dansi la kileo ninamaanisha hili linalopigwa na bendi zinazochombeza na sebene za Kikongo.
Sina uhakika sana, lakini sidhani kama itakuwa sahihi kwa shabiki wa muziki huu, kumuondoa Le General katika Tatu Bora, kama ataamua kuwapanga mastaa wake kwa namba, kutokana na uwezo wake wa kuimba, kutunga na hata kuchomeka maneno yanayotoa burudani kubwa kwa mashabiki akiwa jukwaani.
Nimeshawahi kuandika mara nyingi sana kuhusu sifa za mwanamuziki huyu, kiasi kwamba sioni kipya cha kuongeza, labda niwakumbushe tu kwamba tokea alipopata nafasi ya kuonyesha uwezo wake, Banza Stone amekuwa juu hadi leo hii, anapolazimisha yeye mwenyewe kujiporomosha kwa makusudi.
Katika bendi zote alizopitia kwenye miaka hii ambayo wanamuziki wetu waliamua kupiga sebene, kuanzia African Stars, TOT, Bambino hadi Extra Bongo, nafasi yake ilibakia kuwa ya juu, pengine kuliko wanamuziki wote aliofanya nao kazi. Hakuwahi kuchuja na wala mashabiki wanaomuunga mkono na wasiomhusudu, hawakuwahi kutilia shaka uwezo wake.
Banza Stone ninamfahamu kidogo, nimewahi kufanya naye kazi.
Nje ya jukwaa, ni mtu mpole na mwenye utani. Katika kipindi cha karibu miaka kumi iliyopita, imekuwa na nyakati za kusikitisha sana zinazomzonga Banza Stone, wakati flani akiwa Chui na Paka dhidi ya Ally Choki.
Ingawa siyo jambo jema sana kujadili afya ya mtu, lakini inapobidi, haina budi, hasa afya inayozungumzwa ikiwa ni ya mtu wa watu kama ilivyo kwa mwanamuziki huyu. Mara kadhaa, hali yake imekuwa ikibadilika kiasi cha wakati mwingine kutupa hofu kubwa mashabiki wake, achilia mbali wanafamilia yake.
Watu wamekuwa wakisema maneno mengi juu yake, lakini jambo kubwa zaidi linalozungumzwa ni kuhusu mwenendo wake, hasa kila baada ya Mungu kumjaalia na afya yake kutengemaa.
Kuna wakati alidhoofu sana kufikia kiasi cha baadhi ya watu, mara kadhaa kuzusha kuwa alifariki. Kuna waliomtabiria kwamba hatamaliza mwaka, lakini Mungu alikuwa upande wake, akimsaidia kupambana hadi hali yake ilipoimarika.
Banza Stone anakunywa pombe. Kila mara anapotokea katika ugonjwa, marafiki na watu wanaomtakia mema, wamekuwa wakimshauri kuachana na tabia yake ya unywaji pombe uliopitiliza.
Inavyoonekana, yeye mwenyewe haumizwi na hali yake, badala yake, mashabiki ndiyo wamekuwa wakiumia juu yake.
Wanapomuona amekunywa hadi anashindwa kufanya kazi, wakati ni hivi karibuni tu alikuwa mahututi kwa maradhi, wanaumia sana.
Nimshauri tu Banza Stone, hakuna kitu muhimu katika maisha kama afya. Ni lazima afanye kadiri inavyowezekana kuhakikisha anailinda afya yake kwa sababu kila kitu kitafuata.
Afya ndiyo itakayomfanya apate nguvu za kutafuta riziki, vinginevyo atakuwa anawafedhehesha mashabiki wake pale anapozunguka katika bendi na kuanza kuombaomba hela.
Ndiyo, Banza Stone anaomba fedha kwa watu, ingawa kwa kijanja. Wakati flani akitokea katika homa kali, baada ya kupona, alikuwa akienda katika bendi zingine na wanamuziki wenzake wakimuona, kwa kujua kuwa ametokea kuumwa, walimpandisha jukwaani ili awasalimu mashabiki.
Salamu yake ilitoka kwa kupigiwa mojawapo ya nyimbo zake na yeye kuimba. Sauti yake huwanyanyua watu na kwenda kumtunza.
Nimewahi kumshuhudia akifanya hivyo mara mbili usiku mmoja katika bendi mbili tofauti, wakati ule nikiwa ripota mzuri wa habari za burudani.
Wanaotoa fedha hufanya vile kama pole yao kwake. Lakini kumbe, yeye huzitumia vibaya fedha anazopata kwa kuendelea kunywa pombe wakati afya yake haiko sawasawa.
Inaumiza kuona mtu ambaye mamia ya watu wangependa kumuona akiwa na afya njema, yeye mwenyewe anaongoza jitihada za kujimaliza.
No comments:
Post a Comment