TUNAENDELEA na makala haya ambayo tuliyaanza wiki
mbili zilizopita, mwigizaji Sabrina Rupia ‘Cathy’ anafunguka hatua
mbalimbali ambazo alipitia katika maisha yake.
Mwandishi: Kwa nini uliamua kufanya shughuli za ufugaji?
Cathy: Ufugaji na kilimo ni vitu ambavyo vimo kwenye
damu, nimezaliwa na kukulia mashambani na katika ufugaji wa kienyeji,
mama yangu alikuwa anakamua maziwa na kuuza wakati mwingine sisi
tulizungusha kwa wateja wetu.
Mwandishi: Ulikuwa unapata wapi pesa za kununulia vifaa vya shule? Cathy:
Mama hakuwa na shida ya kutusomesha ama kutununulia madaftari kwani
alikuwa na uhakika akikamua ndoo kadhaa za maziwa basi atanunua
madaftari na sare za shule kwa hiyo maisha yalisonga kama kawaida.
Mwandishi: Kwa sasa na wewe unafanya hizo kazi au uigizaji ndiyo kila kitu kwako? Cathy:
Kwa kweli maisha yangu ni ya kufanya kazi, nina vikundi vya kina mama
ambavyo pia vinasaidia sana katika maisha ya kina mama wanaojituma,
lakini pia ni mfugaji wa kuku, nina kuku wengi sana nyumbani na nina
mashamba wakati mwingine huwa naingia shamba kulima mimi mwenyewe. Mwandishi: Unawezaje kujigawa katika ufugaji na uigizaji?
Cathy: Ni kujipanga tu, ukinikuta nyumbani nafanya
kazi kama mama mwenye familia na kama nikufanya filamu yangu nafanya au
kama kuna mtu anahitaji kunishirikisha basi naenda kufanya hivyo kama
kuna nafasi.
Mwandishi: Ni changamoto zipi unazokutana nazo katika ufugaji. Cathy:
Nyingi sana kwa sababu kuku wa biashara wanahitaji uangalizi wa hali ya
juu kama mtoto, wanaugua mafua, kuharisha na magonjwa mengine kwa hiyo
najitahidi kufanya kila jitihada ili wasiugue na kunitia hasara.
Mwandishi: Unazungumziaje mchepuko katika ndoa za sasa. Ya kwako imetulia? Cathy:
Wanaume na wanawake wanapaswa waheshimiane na waheshimu misingi ya ndoa
lakini pia wamjue Mungu. Yangu nashukuru haina matatizo.
Mwandishi: Inasemekana wewe ni mmoja wa wasanii
wenye utajiri wa kutosha katika wasanii wa filamu hapa Bongo, funguka
kuhusiana na mali zako.
Cathy: Mimi sio tajiri, matajiri wapo wamekaa
wanaletewa, wanalala mpaka saa nne, wakiamka wananyoosha miguu na kunywa
juisi safi hela zinaingia wakiwa wamekaa.
Mwandishi: Kwani wewe huamka saa ngapi?
Cathy: Saa kumi na moja alfajiri mara nyingi nakuwa
nishaamka, wafanyakazi wangu wanaamka baadaye na nikiamka huwa
nakimbizana na kazi za hapa na pale.
Mwandishi: Kutokana na mikikimiki yako umepata nini?
Cathy: Nashukuru Mungu nimejenga, nina sehemu ya
kuweka mbavu zangu, nina mabanda ya kuku, nina mgahawa wangu, nina
mashamba kwa ajili ya kilimo, nina gari kadhaa basi siku zinaenda ila
sina mali nyingi za kutisha.
Mwandishi: Katika mahusianao ni kitu gani unachokipenda?
Cathy: Nampenda sana mume wangu kwa sababu ananifanya vile navyotaka kuwa ananipa muda wa kutosha kufanya shughuli zangu.
Mwandishi: Katika mahusianao ni kitu gani hupendi kufanyiwa? Cathy: Kukosa amani na upendo.
Mwandishi: Nini ulipenda kwa mume uliye naye? Cathy: Kwanza umri wake ulinivutia kwa sababu tumepishana kiumri. Mwandishi: Wewe na mumeo mmetofautiana miaka mingapi? Cathy: Dah! Sipendi ishu ya miaka wala kumuongelea mume wangu ila yeye kanizidi kiumri ni mtu mzima kiasi.
Itaendelea wiki ijayo
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment