Mamia
ya wasichana waliotekwa na kundi la Boko Haram nchini Nigeria wanadaiwa
kuonekana wakioga na kuwapikia wanamgambo wa kundi hilo.
Aidha taarifa zinaeleza wengi wa wasichana hao wanashikiliwa katika kambi tatu tofauti nje ya Nigeria.
Mmoja
wa viongozi wanaohusika katika majadiliano ya kutaka wasichana hao
waachiliwe huru, Dk Steven Davis alikaririwa na Shirika la Utangazaji
la Uingereza (BBC) akieleza hayo.
Dk
Davis, ambaye ni raia wa Australia na wenzake walio katika harakati za
kuwakomboa mabinti hao, waliwaona baadhi ya wasichana hao wakioga na
upande mwingine walikuwa wakiwapikia watekaji ambao ni kundi la
wanamgambo wa Boko Haram.
Davis
alisema majadiliano ya kutaka kuachiliwa kwa wasichana hao yalikuwa
katika hatua za mwisho kufanikiwa lakini makamanda wa kundi hilo
walipinga wazo hilo dakika za mwisho wakihofia kukamatwa.
Hata
hivyo, alisema juhudi zozote za kuwanusuru wasichana hao kwa nguvu
hazitafua dafu isipokuwa kwa njia ya mazungumzo na makubaliano ya
amani.
Mei
14, Serikali ya Nigeria ilieleza kuwa ipo tayari kufanya mazungumzo na
kundi hilo kuwezesha kuachiwa kwa wasichana hao zaidi ya 200.
Waziri
wa Elimu, Tanimu Turaki, alisema serikali ipo tayari kwa mazungumzo.
Alisema kuwa waliamua hatua hiyo itumike kwa kuwa utekaji huo umeibua
hali ya hofu kuhusu ulinzi wa wanafunzi katika shule mbalimbali nchini
humo.
Baada
ya utekaji huo, Boko Haram walijinadi kuwa, watawauza mabinti hao kama
watumwa. Rais Goodluck Jonathan alipitisha kuwaachia wafungwa wao lakini
waziri huyo alisema imekuwa vigumu kujadiliana.
Hata
hivyo, Serikali ilisema njia zote za kuwapata wasichana hao ziko
mezani na wapo tayari kwa majadiliano lakini kundi hilo limekuwa
likibadili uamuzi mara kwa mara.
Boko
Haram ilionesha katika video inayosadikiwa kuwa ni ya wasichana hao,
kundi la mabinti takribani 130 wakiwa wamevaa vazi za kiislamu la hijabu
lakini hawakueleza video hiyo imechukuliwa wapi na lini.
Wasichana
hao wakiwa mchanganyiko, wakristo na waislamu walitekwa na kundi hilo
usiku wa Jumatatu, Aprili 14 mwaka huu katika hosteli ya shule mjini
Chibok, Jimbo la Borno.


No comments:
Post a Comment