Wakati sakata la kuokotwa kwa viungo vya
binadamu likiendelea kutikisa nchi, Chuo Kikuu cha Afya na Sayansi
Shirikishi Muhimbili (MUHAS), kimesema kuwa hutumia maiti 25 kwa
kuwafundishia wanafunzi kila mwaka.
Pia chuo hicho hakijawahi kuagiza maiti
kutoka nje ya nchi na kwamba ni mtu mmoja tu aliyewahi kutaka maiti ya
mtoto wake itumike kufundishia.
Kauli hiyo ya MUHAS imekuja siku chache
baada ya Serikali kuamua kuifungia Hospitali ya Chuo Kikuu cha Kimataifa
cha Tiba na Teknolojia (IMTU), baada ya kubaini kasoro kadhaa katika
utendaji wake.
Juzi, Serikali ilifanya ukaguzi wa
kushtukiza IMTU, baada ya hospitali hiyo kukumbwa na kashfa ya utupaji
wa mabaki ya viungo vya binadamu katika Bonde la Mto Mpiji, jijini Dar
es Salaam mwanzoni mwa wiki iliyopita.
Hata hivyo, wakati Tume ya Watu 15
iliyoundwa na Serikali kuchunguza suala hilo ikiendelea na kazi, Mkuu wa
Kitengo cha Anatomy MUHAS, Profesa David Ngassapa amebainisha kuwa chuo
hicho hutumia maiti 25 kwa mwaka.
Ngassapa alisema kuwa wanafunzi wa mwaka
wa kwanza hutumia maiti 20, huku madaktari wanaorudi chuoni hapo kwa
ajili ya mazoezi wakitumia maiti tano.
“Sheria ya mwaka 1963 inatutaka baada ya
matumizi tuondoe mwili kwa heshima zote na miongoni mwa vitu ambavyo
wanafunzi wanasisitizwa ni kuhakikisha wanaiheshimu miili hadi hatua za
mwisho,” alisema Ngassapa.
Alieleza kuwa pamoja na sheria kutoa
ruhusa ya kutumia maiti katika mafunzo, bado imeweka vipengele
vinavyowataka madaktari kuiheshimu miili ya watu, hadi hatua ya mwisho.
Ngassapa aliongeza: “Sheria inaruhusu
kuhifadhi mabaki ya miili kwa njia mbili; kuizika na kuichoma moto, pia
hospitali inaweza kuhifadhi mabaki hayo hata kwa miaka mitano.”
Hajawahi kuagiza miili kutoka nje
Akizungumzia utaratibu wa nchi
kubadilishana maiti kwa ajili ya mafunzo, Profesa huyo alisema kuwa kwa
zaidi ya miaka 30 aliyokuwa katika kitengo hicho, hawajawahi kuagiza
maiti kutoka nje ya nchi.
Alisema maiti zilizopo nchini zinatosha
kufundishia wanafunzi wote wa udaktari kwa kuwa siyo Hospitali ya Taifa
Muhimbili(MNH), pekee inayotegemewa kutoa miili hiyo.
Alisema kuwa siku za nyuma, Serikali
ilikuwa ikiagiza mifupa kutoka nje ya nchi kwa ajili ya mafunzo, lakini
sasa kila kitu kinafanyika hapa nchini.
Ngassapa alisema kuwa miili
iliyoharibika kwa ajali au magonjwa haifai kutumiwa kwa kuwa mwanafunzi
anatakiwa kujifunza kwenye mwili uliokamilika.
Amkumbuka mtu aliyetoa maiti ya binti yake
Alisema kuwa historia ya Tanzania
inaonyesha kuwa ni mtu mmoja pekee ndiye aliwahi kujitolea maiti ya
binti yake ili itumike kufundishia.
“Alijitolea kwa kuwa binti yake huyo
alianza kuugua akiwa na umri wa miaka miwili hadi alipofikisha miaka 12,
muda mwingi akiwa amelazwa hospitalini hapa,” alisema.
“Alipofariki dunia mzazi alisema mtoto
huyo ni wa hospitali na anamtoa kwa ajili ya matumizi ya hapa. Ibada ya
mazishi ilifanyika eneo la chumba cha kuhifadhia maiti,” alisema
Ngassapa.
Alifafanua kuwa hata baada ya
kukabidhiwa maiti hiyo, waliendelea kumhifadhi kwa miaka minne, hadi
walipojiridhisha kuwa wazazi hawatabadilisha mawazo.
Sheria inayotumika
Mkuu huyo wa kitengo kinachoshughulikia
mwili na viungo vyake, alisema kuwa sheria ya Serikali ya mwaka 1963,
ndiyo inayoruhusu chuo chochote cha afya kuchukua mwili kama umekaa
katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa siku 14 bila ndugu kujitokeza.
Ngassapa alifafanua kuwa licha ya sheria
kuwataka kuchukua mwili uliokaa katika kipindi hicho, chuo huuhifadhi
mwili huo kwa siku 30, ili kujiridhisha pasipo shaka kwamba hakuna ndugu
anayejitokeza kuuchukua.
Alibainisha kuwa baada ya hapo, huuweka
dawa ili usiharibike, kisha huuacha kwa wiki mbili au tatu zaidi
wakisubiri kama ndugu wanaweza kujitokeza.
“Inapothibitika kuwa hakuna anayejitokeza, chuo huuchukua na kuutumia kwenye mafunzo,” alisema.
Alifafanua kuwa sheria pia inakitaka
Kitengo cha Anatomy kuandika barua kwa mkuu wa chuo na Mahakama Kuu,
kutaarifu kuwa wamechukua mwili kutoka katika chumba cha kuhifadhia
maiti.
Rais wa Chama cha Madaktari Tanzania
(MAT), Dk Primus Saidia juzi alisema kuwa miili ni mali ya Serikali na
kwamba chochote kinachofanyika kwa binadamu lazima kifuate sheria
zilizowekwa na Serikali.
Pia alisema kwamba sheria inaruhusu nchi
kubadilishana maiti, lakini hana uhakika kama jambo hilo limewahi
kufanyika nchini, ingawa ana uhakika kuwa haiwezekani hospitali zikakosa
maiti za kufundishia.
No comments:
Post a Comment