DUNIA haina huruma! Siku mbili baada ya kumzika mumewe ambaye alikuwa
bilionea maarufu Dar, Amir Tabu, mjane wake, Mwanahamis Rajab ameingia
kwenye tafrani kubwa na mashemeji zake kisa, mali za marehemu huku
akitimuliwa kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na mumewe.
Tukio hilo la kusikitisha lililoshuhudiwa na wanahabari wetu lilijiri
mapema wiki hii nyumbani kwa mjane huyo, Mbezi-Beach, Dar ambapo
kulikuwa na kikao cha familia, yaani upande wa mume na mke.
Gazeti hili lilijipenyeza ‘kikachero’ kwenye kikao hicho na
kushuhudia mzozo mkubwa kwa upande wa ndugu wa mume wakimtaka mfiwa
atoke kwenye nyumba aliyokuwa akiishi na kumtaka kwenda kukaa kwenye
nyumba yao nyingine iliyopo Bagamoyo, jambo ambalo lilipingwa vikali na
upande wa pili hivyo kuzuka malumbano mazito hadi kikao kuvunjika.
MJANE ANENA
Akizungumza na wanahabari wetu,
mjane Mwanahamis alielezea mkasa mzima namna ambavyo ndugu wa mumewe
walivyojiandaa kumdhulumu mali alizochuma na mumewe.
Alisimulia kwa uchungu: “Mimi na Tabu tulifunga ndoa halali mwaka
2005. Nakaribia miaka 10 sasa katika ndoa yangu japo sikubahatika kupata
mtoto lakini nilimkuta mume wangu akiwa na watoto 6.
“Watoto watatu alizaa akiwa kwenye ndoa nyingine na watoto wengine alizaa nje ya ndoa.
“Kwangu, nahesabu watoto wote ni wangu. Hadi tunafikia kwenye haya
maisha nimepitia magumu mengi kipindi chote hadi umauti unamkuta mume
wangu. “Watoto wake wamekuwa wakiniheshimu kama mama yao, nimemuuguza
mume wangu kwa zaidi ya miaka 4 tangu 2010.
“Katika
kipindi chote hicho sikuwaona ndugu, walianza kuja baada kuona hali ya
mume wangu imekuwa mbaya.“Matatizo ya mume wangu yalianza akiwa kazini
kwenye Kampuni ya Toyota. Alikuwa akisumbuliwa na presha ya macho,
kisukari na kufeli kwa figo zote.
“Wakati umauti unamkuta, tulikuwa Bagamoyo kwenye nyumba yetu
nyingine, huko ndiko chokochoko za dhuluma zilionekana mapema tangu
mwanzo kwani ndugu wa mume wangu walikuwa wananizuia kumuona hata mume
wangu.
“Waliniwekea masharti utadhani hakuwa mume wangu, niliumia sana.
“Siku moja shemeji yangu mmoja aliniomba aone hati zote za magari ya
kisasa, majumba ya kifahari, hoteli, viwanja, bastola, kadi za benki,
leseni ya gereji yake iliyopo Magomeni (Dar) na hati ya Hoteli ya Blue
Nile iliyopo Bagamoyo.
“Mali zote za marehemu nilikuwa nasimamia mimi. Kulipia ada za watoto
shule na matibabu ya mume wangu ila shemeji alivichukua na kukaa navyo,
sikujua anataka kufanya nini nashindwa kumwelewa mbona kabla
hawakujionesha?“Nitapigania jasho langu na mume wangu hadi tone la
mwisho kwani wanataka kunitoa roho kwa presha.”
MAJIRANI WALAANI
Wakizungumza na gazeti hili,
majirani wa mjane huyo walilaani vikali kitendo cha ndugu hao wa mume
kufanya ukatili huo ambao haukubaliki kwenye jamii.
AFISA MTENDAJI
Akizungumzia ishu hiyo, Afisa
Mtendaji wa Kata ya Kawe, Mbezi-Beach B, Hamatton Bhao alisema alipokea
malalamiko ya mjane huyo ambapo mdogo wa mjane alimueleza kuhusiana na
sakata hilo la ndugu wa mume kutaka kumtoa mjane ndani ya nyumba yake
ikiwa ni siku mbili tu tangu amzike mumewe.
Alisema mjane huyo alikuwa akilalamika kudhulumiwa mali alizochuma na
mumewe ndipo alipotoa taarifa Kituo cha Polisi cha Kawe baada ya
wanadugu wa mume kufika nyumbani kwa mfiwa na kufanya vurugu ambapo
polisi walipofika wanandugu walikuwa wameshatimua.
Hata hivyo, polisi waliweka ulinzi wa askari wakiwa na difenda wakiendelea na uchunguzi wa sakata hilo.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment