JESHI
la Polisi Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, jana limelazimika kutumia mabomu
ya machozi na kuwatia mbaroni waumini 29 wa Kanisa la Moravian Usharika
wa Kinondoni, Dar es Salaam baada ya kutokea vurugu za waumini kanisani
hapo.
Akizungumza
na Majira, Kamanda wa Mkoa wa Kipolisi Kinondoni, Camillius Wambura,
alikiri jeshi hilo kuwatia mbaroni waumini hao na kusema kuwa, taratibu
zikikamilika watafikishwa mahakamani.
Hali
ya kuvunjika kwa amani kanisani hapo, ilianza saa moja asubuhi ambapo
pande mbili za waumini hao ambazo zimekuwa zikipingana muda mrefu,
zilishindwa kuelewana na kusababisha vurugu ambazo ziliingiliwa kati na
jeshi hilo.
Awali
kulikuwa na habari kuwa, zaidi ya watu 30 walikuwa ndani ya kanisa hilo
eneo la juu tangu juzi ambapo jana asubuhi, watu hao walipelekewa
vyakula na waumini wenzao ambao hawakulala ndani ya kanisa hilo.
Wakati
waumini hao wakianza kuingiza chakula ili kuwapelekea wenzao waliokuwa
juu wakati eneo la chini wakiendelea na ibada, ndipo hali ilipoanza
kuchafuka baada ya upande mmoja kuzuia chakula kisipelekwe kwa waumini
waliokuwa juu ya kanisa hilo.
Polisi
walifika eneo la tukio saa 1:40 wakiwa katika gari lenye namba za
usajili PT 2118 ya Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kinondoni iliyoandikwa (OCD
Kinondoni), ikiwa na askari ambao walipiga kambi nje ya kanisa hilo.
Askari
hao hawakuingilia mzozo huo lakini waliwaonya waumini hao kuwa kama
mmojawapo ataanza kumshika mwenzake na kusababisha vurugu basi
watamkamata mara moja lakini ikiwa hawatagusana wao hawataingilia.
Waumini
hao waliendelea kuzuiana ambapo vyakula vilivyoletwa kanisani hapo
ambavyo ni chipsi, kuku, soda, maji na miswaki vilimwagwa na vyombo
kutupwa nje ya eneo la kanisa hali iliyosababisha waumini hao kuanza
kushikana ambapo wengine walitumia hadi mafagio ili kupigana.
Baada
ya kuona hali hiyo Jeshi la Polisi lililazimika kuwakamata wale
waliosababisha vurugu hali iliyosababisha askari mmoja kung’olewa
vifungo vitatu vya shati lake wakati wa vurugu za kuwakamata.
Baadaye
polisi waliamua kuwaachia waumini waliowakamata ambao ndio walioanza
kuwagusa wenzao lakini waliwaachia na kuamua kuondoka eneo la kanisa
wakiwa na gari lao.
Dakika
chache baadaye, liliingia basi dogo likiwa na waumini zaidi ya 20 ambao
inadaiwa walitokea katika Kanisa la Mabibo na kuanza kuimba ndipo hali
ikachafuka ambapo polisi walirudi haraka kanisani hapo wakiwa wameongeza
askari wengine, kupiga mabomu ya machozi na kuwatia mbaroni waumini
hao.
Akizungumza
na waandishi wa habari, Mchungaji wa Kanisa hilo, James Mwakalile,
alisema anajisikia vibaya sana kuona mgogoro ukiendelea na wanaogombana
ni walei si viongozi.
Alisema yeye anataka amani katika kanisa hilo na amejitahidi sana kuwaita upande wa pili ili wazungumze lakini hakuna lililofanyika.
Alisema yeye anataka amani katika kanisa hilo na amejitahidi sana kuwaita upande wa pili ili wazungumze lakini hakuna lililofanyika.
Majirani
waishio jirani na kanisa hilo, wamesema wamechoshwa na hali ya mgogoro
unaoendelea kwani wanaoleta vurugu hizo wengi si wakazi wa hapo na
kuitaka Serikali kulifunga kanisa hilo kabla mauaji hayajatokea.
Credit: Majira
No comments:
Post a Comment