MAMBO YANAYOSABABISHA MTU KUWA NA KIPARA, SOMA KWA UNDANI


Kipara ni kitu ambacho kinawapata watu wengi walioko sehemu mbalimbali duniani. Takwimu zinaonyesha kuwa takriban asilimia 50 ya wanaume kwa nyakati tofauti maishani mwao hujikuta wanapata kipara.
Kwa wanaume, mara chache kipara, kinaweza kuanza mapema kati ya umri wa miaka 14 na 20, lakini wanaume walio wengi hupata kati ya umri wa miaka 30 na 60.
Wanaume wanaopata kipara huanza kuona nywele zikipungua kichwani hatua kwa hatua, kuanzia upande wa mbele au katikati ya kichwa na hatimaye sehemu hiyo huwa haina nywele kabisa.
Ingawa kimsingi kipara hufikiriwa kuwa ni tatizo la kawaida kwa wanaume, wanawake pia wanaweza kukabiliwa na tatizo hili.
 Inasemekana kuwa karibu asilimia 40 ya wanawake nchini Marekani, kutokana na sababu mbalimbali wana tatizo la kipara au kunyonyoka nywele kichwani.
Kila unywele huota na kukua katika kifuko cha nywele kiitwacho kinyweleo kilichoko kwenye ngozi.
Chini ya kila kinyweleo kuna kituta ambacho hushikilia unywele na kituta hiki hujulikana kama foliko ya nywele.
Katika hali ya kawaida wastani wa nywele 50 hadi 100 huchomoka kila siku kutoka katika vifuko vyake katika ngozi ya kichwani na kuanguka chini.
Jambo hili linaweza kugunduliwa kwa urahisi kwa kuona nywele kwenye vitana, chanuo au foronya tunazotumia wakati wa kulala.
Nywele zinapochomoka kwa wingi kuliko kawaida kila siku au zisipoota na kukua ili kuziba pengo la nywele zilizotoka, baada ya muda mtu huwa na kipara. Wakati mwingine nywele hupungua bila kutoka kichwani.
Hali hii inaweza kusababishwa na kupungua kwa unene wa unywele au kutofautiana kwa kasi ya kukua kwa nywele.
Ingawa chanzo hasa cha upara hakifahamiki vizuri, wanasayansi wanasema kuwa kukosekana kwa usawaziko sawia wa homoni ya kiume ya androjeni aina ya dihydrotestosterone (DHT) mwilini, ni moja ya vyanzo vya tatizo hili.
Homoni hii inapoongezeka mwilini hasa katika ngozi ya kichwa, husababisha mgandamizo wa ngozi ya katikati ya kichwa na kuathiri foliko za nywele kwa kuzifanya ndogo kiasi kwamba zinapoteza taratibu uwezo wake wa kutokeza nywele mpya.
Hii ni kwa mujibu wa Dk Emin Tuncay Ustuner, daktari bingwa wa upasuaji wa kurekebisha sura katika Jiji la Ankara nchini Uturuki.
Baadhi ya tafiti zinaonyesha kuwa kutokea kwa kipara kuna uhusiano wa karibu na urithi wa vinasaba au viasili vya kijenetiki vinavyoathiri kuota na kukua kwa nywele katika kipindi fulani.
Utafiti uliofanyika nchini Japan na kuongozwa na Profesa Yumiko Saga wa taasisi ya taifa ya vinasaba katika Jiji la Mishima, ulibaini kuwa viasili vya kijenetiki aina ya Sox21 vinahusika kwa namna moja ama nyingine na utokeaji wa kipara.
Utafiti mwingine, uliofanywa na timu ya watafiti waliokuwa chini ya uongozi wa Dk Krzysztof Kobielak, unahusisha viasili vya kijenetiki aina ya Wnt na BMP (Bone Morphogenetic Protein) na kutokea kwa kipara.
Utafiti huo ulibaini kuwa protini aina ya Wnt inapopungua na BMP inapoongezeka, husababisha seli zinazozalisha foliko za nywele kushindwa kufanya kazi na nywele hushindwa kuota au kukua.
Matokeo ya utafiti huo yalichapishwa katika jarida la kisayansi la Stem Cells, la Septemba na Novemba 2013.
Katika utafiti wao, Dk Lin-hui Su na Tony Hsiu-His Chen uliochapishwa katika jarida la Archives of Dermatology, toleo la 143 la Novemba 2007, walibaini kuwa sumu zinazopatikana katika moshi wa tumbaku pia zinaweza kuathiri foliko za nywele na kuharibu usawaziko wa homoni za kiume mwilini.
Jambo ambalo huchangia kutokea kwa tatizo la nywele kushindwa kuota na kukuwa vizuri hasa kwa wanaume wenye homoni nyingi.
Matatizo mengine ya kiafya yanayohusishwa na kutokea kwa kipara ni tatizo la muda mrefu la msongo mkali wa mawazo, ugonjwa wa kaswende, tiba ya mionzi, matumizi ya dawa za kutibu saratani na matumizi ya dawa zenye homoni.
Matatizo mengine ni pamoja na lishe duni kwa muda mrefu, ugonjwa wa tezi la shingo pamoja na matumizi yaliyokithiri ya dawa za kulainisha nywele zenye kemikali kali.
Ingawa kipara hakiwezi kusababisha mtu apoteze maisha, kinaweza kuwa na athari za kisaikolojia kwa watu wengi hasa vijana wanaopenda mitindo mbalimbali ya urembo wa nywele.
Jambo hili katika nchi zilizoendelea huwafanya baadhi ya watu kufanyiwa upasuaji wa kurekebisha kipara.
Hapa kwetu Tanzania, hospitali za rufaa zinao madaktari wa magonjwa ya ngozi wanaoweza kutoa msaada na ushauri kuhusu namna bora ya kukabiliana na tatizo la kunyonyoka kwa nywele au kipara.
Ili kukabiliana na athari za kisaikolojia zitokanazo na kipara hasa pale inapokuwa vigumu kupata fursa ya kumwona daktari, mtu mwenye tatizo hili anaweza kuvaa wigi au kunyoa nywele zote mara kwa mara.
Kwa ajili ya kukinga ngozi ya kichwa isiathirike kwa mionzi ya jua, mwenye kipara anaweza kuvaa kofia hasa wakati wa jua kali.
Hata hivyo, wapo watu wanaopenda kuwa na kipara kutokana na sababu mbalimbali lakini hushindwa kuwa na hicho cha asili.
Ili kutekeleza kiu yao wao hunyoa upara kwa kumaliza nywele zote kichwani na hii imekuwa ikafanyika kwa vijana, wazee bila kujali jinsi.
Mtaalamu wa magonjwa ya ngozi wa Hospitali ya Rufaa Mbeya, Dk Baraka Chaula anasema kuwa kwa hapa nchini hakuna utafiti juu ya kipara uliowahi kufanyika katika miaka ya nyuma.
“Labda iwe kwa miaka ya karibuni lakini katika miaka iliyopita, sijaona kumbukumbu yoyote ya utafiti wa kipara kufanyika,” anasema Dk Chaula.
Pamoja na hali hiyo, anasema suala la kipara linaweza kuchukuliwa ni sehemu ya tatizo la ngozi kutokana na namna lilivyo, sehemu linapotokea pamoja na athari zake.
Wao kama wataalamu, anasema wanaamini tatizo la kipara linaweza kusuluhishwa iwapo chanzo chake kitagundulika mapema na hatua za kitiba kuchukuliwa.
Anasema kipara kinachosababishwa na kaswende kinaweza kuzuilika iwapo tiba ya ugonjwa itafanyika kwa wakati.
Kuhusu kuwakumba zaidi wanaume kuliko wanawake, Dk Chaula anasema kipara ni tatizo la homoni za kiume zaidi.“Hata wanawake hupata kipara lakini hili huwapata wanaume zaidi kwa sababu ni tatizo la homoni za kiume,” anasema Dk Chaula.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger