Jeshi la Polisi linamshikilia dereva mmoja wa pikipiki, maarufu kama bodaboda wilayani Mwanga mkoani Kilimanjaro baada ya mke wa askari polisi kukutwa amekufa chumbani kwa dereva huyo.
Tukio hilo ambalo limezua gumzo kubwa wilayani humo lilitokea juzi saa
12:00 jioni katika eneo la New Mwanga wilayani humo na mtuhumiwa
akidaiwa kukutwa akiwa amelewa chakari.
Mkuu wa Wilaya ya Mwanga, Shaibu Ndemanga amethibitisha kuwapo kwa tukio hilo na kusema uchunguzi unaendelea.
“Hilo tukio lina ukweli na bahati mbaya sana mumewe ndiyo kwanza
amehamishiwa Geita na alikuwa akaripoti halafu aje kuchukua familia
yake,” alisema Ndemanga.
Mkuu huyo wa wilaya ambaye pia ni mwenyekiti wa kamati ya ulinzi na
usalama ya wilaya hiyo, alisema hadi sasa haijafahamika nini kilitokea
na kwamba hilo ni moja kati ya mambo ambayo polisi inachunguza.
“Hayo yote kwamba ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo kijana, nini sababu za kifo yatajulikana kadiri upelelezi unavyoendelea,”alisema.
Imeelezwa kuwa jana ilikuwa siku ya askari huyo kuripoti katika kituo chake kipya cha kazi.
“Mpaka sasa hivi haijajulikana nini hasa kilitokea huko chumbani na ilikuwaje akawa chumbani kwa huyo dereva,”alisema
mmoja wa watu waliokuwapo katika eneo la tukio ambaye hata hivyo,
hakutaka kutaja jina lake na kuongeza kuwa jana saa sita mchana, mwili
wa mwanamke huyo ulichukuliwa kutoka Hospitali ya Wilaya ya Mwanga na
kuhamishiwa Hospitali ya Rufaa ya KCMC kwa uchunguzi.
Taarifa za awali zinasema kuwa mwili wa marehemu ulikuwa na mikwaruzo shingoni hali inayotia shaka kuwa huenda alinyongwa.
Habari nyingine zinadai kuwa siku ya tukio, mwanamke huyo alikuwa ameaga
kuwa anakwenda kanisani lakini baadaye simu yake ilipopigwa ilikuwa
ikipokewa na mwanamume.
Ilidaiwa kuwa mume wa marehemu alipojaribu kupiga simu ya mkewe, ilikuwa
ikipokelewa na mtu aliyeonekana kuwa ni mlevi wa kupindukia hali
iliyomtia wasiwasi na kuamua kuwapigia simu marafiki zake wa karibu ili
wamsaidie kumtafuta ndipo walipopata taarifa kuwa ulikuwapo uhusiano
kati ya shemeji yao na dereva huyo wa bodaboda.
Ilidaiwa kuwa marafiki hao walikwenda moja kwa moja nyumbani kwa dereva
huyo wa bodaboda ambako walimkuta akiwa amelewa na walipoingia ndani
walimkuta shemeji yao akiwa ameshafariki dunia.
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
Credit: Mwananchi
Kamanda wa Polisi Mkoa Kilimanjaro, Robert Boaz hakupatikana jana kuzungumzia tukio hilo kwa kuwa alikuwa kwenye ziara ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda huko Gonja wilayani Same.
Credit: Mwananchi
No comments:
Post a Comment