UKATILI: BINTI ASIMULIA WATANZANIA WANAVYOTUMIKISHWA CHINA


Wakati wanawake kwa wanaume wengi huenda barani Asia, hasa China kununua bidhaa kwa ajili ya kuja kuzichuuza, hali sasa ni tofauti kwa kuwa kuna wasichana ambao huenda huko kwa ahadi za ajira, lakini huishia kufanya ukahaba kwenye madanguro, gazeti hili linaweza kukuthibitishia.

Wasichana hao hutafutwa na mawakala wa hapa nchini ambao kazi yao huwa ni kutafuta wasichana wazuri na baadaye kuwashawishi kwa kuwaeleza fursa za ajira za hotelini zilizo barani Asia.

Msichana akikubali, wakala huchukua jukumu la kumtafutia viza ya kuingia China na baadaye kuwasiliana na mwenyeji wake, maarufu kama Lady Boss, ambaye hutuma tiketi ya ndege kwa ajili ya kumsafirisha 'mwajiriwa' mpya.

Hata hivyo, hali hubadilika mara wafikapo huko kwa kuwa 'mwajiri' huyo humpokonya hati ya kusafiria na baadaye kumpa maelekezo kuwa atatakiwa kulipa Dola 200 kila siku ambazo atakuwa akizipata kwa kufanya umalaya kwenye klabu na maeneo ya biashara.
Tayari wasichana kadhaa wa Kitanzania wamenaswa katika mtego huo na kujikuta wakilazimika kuuza miili yao ili wamudu ada ya Dola 200 pamoja na fedha za kujikimu, akiwemo Munira Mathias mwenye umri wa miaka 23 ambaye alimudu kuvaa ujasiri wa kuweka bayana uovu huo katika mazungumzo yake na gazeti hili.
Binti huyo Mtanzania aliyesafiri kwa saa 18 kwenda Guangzou, China alitakiwa kupumzika kwa saa mbili tu kabla ya kupelekwa kuanza 'kazi' ambayo hakuitarajia.
"Baada ya kupumzika kwa saa mbili tu, nilipelekwa kwenye klabu," anasema Munira wakati akisimulia mkasa wake.
"Sikuwa na kazi nyingine zaidi ya kucheza muziki na wanaume ambao licha ya kwamba sikuwahi kuwaona, walinichangamkia kama vile wananifahamu."
Munira aliondoka Januari mwaka huu kwenda China ambako aliahidiwa kuwa angeajiriwa hotelini, lakini alikutana na 'ajira' ya ukahaba, huku akilazimika kuwalipa 'waajiri' wake Dola za Marekani 200 kila siku.
Binti huyo, ambaye alifanikiwa kuchomoka mikononi mwa waajiri hao baada ya viza yake kuisha, alisema kwa siku 91 alizokaa China, alipata mateso ambayo hatayasahau ikiwamo kupigwa, kubakwa na kundi la wanaume raia wa Nigeria, pia kulazimika kutoa mimba aliyoipata kwa kubakwa.
"Nilifika Guangzhou kama saa 9.00 alasiri za China na kulikuwa na baridi sana," anasema Munira akisimulia jinsi alivyokanyaga kwa mara ya kwanza ardhi ya nchi hiyo akiwa na matumaini ya kuanza maisha mapya.
"Wakati huo nilikuwa nikijaribu kupata mawasiliano na mwenyeji wangu ambaye niliagizwa kutoka Magomeni, Dar es Salaam.

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger