MWANAFUNZI wa Shule ya Msingi Ludewa mkoani Njombe,
Ibrahim Faraja Chipungahelo (9) ameuawa kikatili na mbwa wanaosadikiwa
kuwa na kichaa kisha kuliwa nyama.
Tukio hilo lililoacha simanzi kubwa kwa wakazi wa Ludewa mjini
lilijiri saa 7 mchana wa Agosti 8, mwaka huu katika eneo la Ikilu ambapo
marehemu na wenzake walikuwa wakipita nje ya nyumba ya mtu
aliyejulikana kwa jina la Bosco Lingalangala (Boli) kwenda kuchuma
mapera sehemu.
MASHUHUDA
Kwa mujibu wa mashuhuda wa tukio hilo, mama Kumba na
mama Haule ambao ni wakazi wa Kitongoji cha Ibani Kata ya Ludewa, wakiwa
majumbani mwao walisikia kelele za watoto huku wakimwita mwenzao kwa
jina ‘Ibrahim…Ibrahim’.
“Tulipowauliza kuna nini, wakasema mwenzao Ibrahim amekamatwa na
mbwa. Ndipo tukatoka kwenda kumuokoa lakini tulipofika tulimkuta
marehemu amelala kifudifudi huku mbwa wakiendelea kumla! Tuliogopa sana,
pia tulishindwa kumuokoa, tukakimbilia polisi kutoa taarifa,” alisema
mmoja wa wanawake hao.
DAKTARI ALIVYOSEMA
Kwa mujibu wa taarifa ya
Dokta Sira Rajabu wa Hospitali ya Wilaya ya Ludewa aliyeufanyia
uchunguzi mwili wa marehemu Ibrahim, ulikuwa na majeraha makubwa mwili
mzima huku paja la mguu wa kulia likiwa limeondolewa nyama kabisa.
MGANGA WA MIFUGO
Akizungumza na mwandishi wetu
wakati wa msiba wa mtoto huyo, Mganga wa Mifugo wa Wilaya ya Ludewa,
Simon Haule alisema mbwa hao walikuwa hawajapata chanjo kwa zaidi ya
miaka miwili. Kwa hiyo tayari walikuwa na ugonjwa wa kichaa ambacho
kisingeweza kupona tena zaidi ya kuwaua.
DIWANI AZUNGUMZA MAKABURINI
Akizungumza kwenye
mazishi ya mtoto huyo, Diwani wa Kata ya Ludewa, Monica Mchiro alisema
mawasiliano yalifanywa kati yake na mmiliki wa mbwa hao lakini majibu
aliyoyatoa yalikosa ushirikiano kwa sababu aliahidi kuchukuwa hatua za
kisheria kwa yeyote ambaye angewadhuru mbwa wake.
WANACHOKIJUA MAJIRANI
Baadhi ya majirani ambao
hawakupenda majina yao yaandikwe gazetini, walisema mbwa hao walikuwa
wakifungiwa kwenye banda na kupewa nyama mbichi kwa kurushiwa na
wahudumu lakini siku ya tukio walifunguliwa na kuanza kuzagaa mitaani
kwa nia ya kujitafutia chakula wenyewe baada ya kukosa kwa muda mrefu.
WANANCHI WAANDAMANA, WAWAUA MBWA
Kufuatia tukio
hilo la kusikitisha, Agosti 10, mwaka huu baadhi ya wananchi wa Kata ya
Ludewa waliandamana ili kushinikiza haki itendeke baada ya kuambiwa kuwa
mmiliki wa mbwa hao alitishia kumshtaki yeyote ambaye angehusika kuwaua
mbwa wake.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti katika mkutano wa dharura
ulioitishwa na Diwani Mchilo, wananchi hao walisema mbwa hao walikuwa
tishio kwa muda mrefu kwani walishateketeza mifugo mingi wakiwemo mbuzi
22 na ndama 1, lakini cha kushangaza kila walipolipeleka suala hilo
kwenye vyombo vya dola, mmiliki alitaka ushahidi.
Katika hali isiyokuwa ya kawaida, wananchi hao walisitisha mkutano
huo na kuandamana mpaka kwenye nyumba ya mmiliki wa mbwa hao ambapo
waliwaua kwa kuwapiga risasi.
MIZOGA MITAANI
Kwa hasira, waliondoka na mizoga na kupita nayo mitaani huku wakiimba nyimbo mbalimbali za kikabila na kawaida.
WACHOMA MOTO MIZOGA
Baada ya kuzunguka na mizoga
ya mbwa hao kwa muda mrefu, mwishowe walikwenda kwenye ofisi ya kata
ambako waliichoma moto na kuiteketeza kabisa huku wakishangilia.
MKUU WA WILAYA
Kufuatia tukio hilo, Mkuu wa
Wilaya ya Ludewa, Juma Madaha ameviagiza vyombo husika ikiwemo idara ya
kilimo na mifugo na jeshi la polisi kuchukuwa hatua za kisheria kwa
yeyote anayehusika na tukio hili akiwemo mmiliki wa mbwa hao.
Marehemu Ibrahim Faraja Chipungahelo alizikwa Agosti 9, mwaka huu kwenye Makaburi ya Ludewa, Njombe.
KAMANDA WA POLISI
Naye Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Njombe, ACP Fulgensi Ngonyani alikiri kutokea kwa tukio hilo na
kuongeza kuwa upelelezi unaendelea sanjari na kuwahoji watu mbalimbali,
akiwemo mmiliki wa mbwa hao anayeishi jijini Dar es Salaam.Mungu ailaze
pema peponi, roho yake. Amina.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







No comments:
Post a Comment