MWANAMUZIKI wa nyimbo za
Injili nchini, Rose Muhando anasakwa na Jeshi la Polisi Kituo cha
Kijitonyama ‘Mabatini’ jijini Dar baada ya mchungaji mmoja wa Kinigeria
anayefanya shughuli zake nchini DR Congo, Kabagambe Tchanda kumshitaki
akidai kumlipa fedha ili akafanye onesho badala yake akaingia mitini.
Uchunguzi uliofanywa na Uwazi ndani ya jeshi hilo, umegundua kuwa
kuna madai hayo na kwamba mchungaji huyo alitua jijini Dar na kufanya
mazungumzo na Rose kwa ajili ya kwenda kutumbuiza nchini DR Congo, Julai
mwaka huu katika mkutano uliohusisha wageni kutoka Ulaya na kukubaliana
amlipe Dola za Marekani 5,000 (zaidi ya shilingi milioni 8).
Kwa mujibu wa chanzo, ilidaiwa kuwa mchungaji huyo alimkabidhi Rose
dola 1,900 kama utangulizi na kubaki dola 3,100 ambazo angemlipa baada
ya onesho. Makabidhiano hayo yalifanyika Magomeni ya Mwembechai jijini
Dar.
Kutokana na sekeseke hilo, mwandishi wetu alimsaka mchungaji huyo na
alipoulizwa kuhusu kuwepo kwa madai hayo, alikiri na kusema alimuamini
sana Rose lakini cha ajabu mambo yamekuwa tofauti kwa kuwa hakufika
kwenye tamasha.
Mchungaji huyo aliendelea kudai kuwa, kinachomuuma zaidi ni kwamba,
Rose hataki kumrudishia fedha zake na badala yake amekuwa akimzungusha
na chenga kibao.
“Siamini kabisa kama Rose angeweza kufanya vile maana yeye ni
mtumishi wa Mungu, sasa kwa nini afanye mambo yasiyompendeza Bwana?
Nashangaa sana, sijui hata ni nini kimemuharibu huyu! Nikimpigia simu
akipokea kesho haziishi.
“Anashindwa kuwa na utu maana mimi nimeishiwa fedha naishi kwa shida
hapa nchini, angenipatia hizo pesa zingenisaidia sana maana ujio wangu
huu ni kwa sababu ya kudai hizo pesa tu, ndiyo maana nikaamua
kulifikisha suala hili kwenye vyombo vya dola baada ya kuona
hatuelewani,” alisema.
Ili kuweka sawa mzani wa habari, paparazi wetu alimtafuta Rose
Muhando kupitia simu yake ya mkononi ambayo iliita bila ya kupokelewa
licha ya kumtumia ujumbe mfupi wa maandishi aliamua kukaa kimya mpaka
gazeti linakwenda mtamboni.
Kesi imefunguliwa katika Kituo cha Polisi cha Kijitonyama ‘Mabatini’
kwa jalada namba KJN/RB/7122/14 KUJIPATIA PESA KWA NJIA YA UDANGANYIFU.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)



No comments:
Post a Comment