UKISTAAJABU ya Musa
utayaona ya Firauni! Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linamng’ang’ania
mfanyabiashara maarufu wa Wilaya ya Mvomero, Johnson Damian Mkude (39)
akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake wa kuzaliwa, Mathias kisha
kuondoka nacho kwenda kwa mganga kwa kile kilichodaiwa ni kufanyiwa dawa
ili awe bilionea, Uwazi lina mkasa wote.
Tukio hilo ambalo kwa sasa ndiyo gumzo mkoani hapa lilijiri usiku wa
Agosti 3, mwaka huu katika mashamba ya Kata ya Mlali ambapo ndugu wa
marehemu waliokuwa wakimsaka ndugu yao walifanikiwa kuona kiwiliwili
Agosti 6, mwaka huu.
MWILI WAZIKWA KATIKA SHAMBA LA MTU
Mwandishi
wetu alifika eneo la tukio na kushuhudia kiwiliwili kikiwa kimeharibika
vibaya. Ilibidi baba wa marehemu, mzee Damian Mathias Mkude (63) amwombe
mmiliki wa shamba hilo lililopo kwenye Kijiji cha Mbalala, Kata ya
Mlali kumzika mwanaye hapo ambapo alikubali.
BABA WA MAREHEMU
Akizungumzia tukio hilo kwa uchungu, baba wa marehemu mzee Mkude alisema:
”Mwezi mmoja kabla ya tukio, Johnson alinichonganisha na Mathias,
nakiri hadi marehemu anakufa nilikuwa sina uhusiano naye mzuri kutokana
na maneno aliyoniambia kaka yake.
“Lakini nilipomuuliza kuhusu hayo maneno, Mathias alikanusha,
nikaamua kuyafanyia uchunguzi. Wakati naendelea na uchunguzi Agosti 3,
mwaka huu, majira ya jioni, giza halijaingia niliwaona wanangu (Jonson
na Mathias) wamepakizana kwenye bodaboda.
“Siku hiyohiyo, saa 5 usiku, mke wa Mathias, Revina Evarist akaja
kwangu na kunijulisha kwamba mumewe hajarudi nyumbani na si kawaida yake
kufika muda huo. Tulipompigia simu hakuwa hewani. Kwa vile nilimuona
akiwa na kaka yake, nikampigia yeye lakini simu yake ilizimwa.
“Ilipofika saa 7 usiku tukaamua kwenda kwa kaka yake, tukamkuta.
Nilipomuuliza mdogo wako yuko wapi akasema hajui. Akajiunga na sisi,
tukaendelea kumtafuta mdogo wake kwa zaidi ya siku 2 bila mafanikio,”
alisema mzee huyo.
MAITI ILIVYOONEKANA
Mzee huyo akasema Agosti 6, mwaka huu alipata taarifa kwamba kuna maiti imeonekana kwenye mashamba ya Mlali.
“Nilishtuka sana kusikia hivyo, nikamtuma mkwe wangu, mume wa mtoto
wangu mkubwa na mtoto wa dada yangu, Gasper Msimbe. Walisafari hadi Kata
ya Mlali kushuhudia maiti hiyo.
“Walipofika waliikuta maiti haina kichwa lakini walimtambua kuwa ni
Mathias kwa nguo na viatu. Walinijulisha haraka ambapo nilikwenda eneo
la tukio. Nilipofika niliumia sana kushuhudia mwanangu asiyekuwa na
hatia kauawa kikatili huku mwili wake uliokuwa hauna kichwa ukitoa
harufu kali kwa kuharibika.”
BAADA YA MAZISHI
“Sasa kilichonishangaza ni
kwamba, baada ya mazishi kule shambani, zimesikika tetesi kuwa, Johnson
ndiye aliyemchinja mdogo wake na kutoweka na kichwa kwa imani za
kishirikina ili awe tajiri mkubwa.
“Nikaambiwa anashikiliwa kwenye Kituo cha Polisi Mzumbe (kabla ya
kupelekwa mkoa). Nilikwenda, nikamkuta amewekwa chini ya ulinzi huku
akiwa na hirizi alizokamatwa nazo akiwa kwa mganga wa kienyeji eneo la
Sangasanga, Mvomero.”
BABA AOMBA KICHWA CHA MWANAYE
“Pale kituoni,
polisi walinitaka nimsalimie lakini nikakataa mpaka arudishe kichwa cha
mdogo wake. Tena naliomba jeshi la polisi kumbana Johnson ili kama kweli
amechukua kichwa cha mdogo wake akirudishe nikizike hapa nyumbani
Kijiji cha Nyandila,” alisema mzee huyo.
MKE WA MTUHUMIWA AZUNGUMZIA KUFUNGA NDOA
Uwazi
lilifika nyumbani kwa Johnson ambapo mke wa mtuhumiwa, Mchilo Peter (33)
alikiri mumewe kuswekwa mahabusu akituhumiwa kumkata kichwa mdogo wake.
Alipotakiwa kueleza chochote kuhusu tukio hilo, mwanamke huyo alisema kwa mafumbo:
“Huko ni kukosa elimu, kwa nini mganga akudanganye. Kama ni gari mbona
yeye hana, mume nimeanza kuishi naye tangu mwaka 2000, namwambia
tufunge ndoa hataki, Jumapili kusali hataki, yuko bize kusaka pesa.
“Siku ya tukio kachukua pesa zote ndani zaidi ya shilingi laki 7. Leo
baada ya njaa kuwa kali nimeamua kufungua duka licha ya kupokea vitisho
kwamba kuna kundi la watu linataka kuvamia duka kwa lengo la kuchoma
moto kama hawatapewa kichwa cha Mathias,” alisema mama huyo.
Alipoulizwa kuhusu mali wanazomiliki, alisema wana nyumba, duka na nguruwe wawili.
MTUHUMIWA ALIJULIKANAJE?
Kwa mujibu wa Diwani wa
Kata ya Nyandila (Chadema), Peter Joseph Zengwe, Agosti 15, mwaka huu
baada ya mauaji hayo kutokea, vijana wawili, Amos na Mohamed Chali
walikamatwa na polisi wakidaiwa kuhusika na mauaji hayo.
“Siku chache baada ya mauaji hayo, Amos na Mohamed Chali walifuja
pesa kwa kunywa pombe kupita kiasi ambapo mmoja aliropoka kilabuni
kwamba walilipwa fedha nyingi kwa kumuua Mathias.
“Baada ya
majigambo hayo, watu wakatoa taarifa polisi na wahusika wakakamatwa na
ndiyo waliomtaja Johnson,” alisema diwani huyo.
MGANGA AINGIA MITINI
Uwazi lilifanikiwa kufika
Sangasanga kwa mganga huyo na kuambiwa kuwa alikimbia kwa kutumia mlango
wa nyuma baada ya polisi kufika kwa ajili ya kumkamata.
MATUMIZI YA KICHWA
Habari zilizoenea kwenye
kijiji alichokuwa akiishi marehemu Mathias zinadai kwamba, mganga huyo
ambaye jina halikujulikana mara moja, alimwambia mtuhumiwa kuwa,
angekifanyia dawa kichwa hicho ambapo angekiweka dukani ili kuvuta
wateja wengi kwa siku, hivyo ndani ya mwaka mmoja tu angekuwa bilionea.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)







No comments:
Post a Comment