KWAKO jembe, Charles Gabriel ‘Chaz Baba’. Mwalimu
wao kwenye muziki wa dansi Bongo. Uwezo wako nautambua, nimekuwa shabiki
wako kwa muda mrefu kidogo.Ni matumaini yangu uko poa, unaendelea na
mishe zako kama kawaida.
Mimi mzima, namshukuru Mungu maisha yanasonga. Jukumu langu la
kuandika na kukosoa linaendelea na leo nimekukumbuka wewe.Dhumuni la
kukumbuka leo kwanza ni kukukemea kwamba suala la kuthubutu kushika kitu
kizito, kunyanyua mkono na kumtwanga mtu si jambo jema, halifai kuigwa
hata kidogo.
Ndugu yangu, hivi kwanza unafikiria nini ukichukua kitu kizito na
kumpiga nacho mwenzako?Mbona zipo njia nyingi za kufikisha ujumbe wako
kwa mtu na akajua umekasirika, lakini si kumtwanga na kitu kizito au
chenye ncha kali ambacho unajua fika kwamba utamsababishia maumivu
makali mwilini.
Kwa kitendo ulichokifanya kwa mkeo hivi karibuni hakikuwa cha
kiungwana. Ulimtwanga kiasi ambacho kwa macho ya kawaida tu, inaonesha
aliumia sana.Sitaki kujua alikuudhi nini, lakini ustahimilivu unatakiwa
katika maisha ya kila siku.
Hata iweje yule ni mkeo. Unajisikiaje kumuona akiwa na majeraha
chungu nzima mwilini ambayo umesababisha wewe? Si sawa kabisa!Wewe ni
kioo cha jamii, unategemea jamii itajifunza nini kupitia tukio kama lile
ulilolifanya? Unavyotakiwa kujichunga wewe ni mara mia zaidi ya vile
anavyojichunga mwenzangu na mimi kule Tandale Kwa Mtogole.
Jamii inawatazama mastaa kama kioo chao, wanaamini kwamba nyinyi ni
watu wema. Wanaamini mnajua kujitoa, mna upendo na mna nguvu ya kukemea
maovu kwenye jamii na watu wakabadilika.
Umeshindwa kustahimili hasira zako, ona sasa jamii nzima ilijua
kwamba umemdunda mkeo kiasi cha kuwafanya hata wale mashabiki
wanaokufuatilia waone kuwa hukumtendea haki mkeo.Kumpiga mtu siyo dawa
ya kutibu tabia au tatizo lake.
Unaweza ukampa mtu adhabu nyingine ambayo kwa macho ya kawaida
inaweza kuonekana ndogo lakini kumbe ni nzito na ikamfanya mtu aone aibu
kwa kipindi kirefu kama si maisha yake yote.Kunyanyua mkono na kumpiga
mtu ni tabia.
Ukiiendekeza unaweza kufika pabaya ambapo pengine hata hujawahi
kutegemea kama ipo siku unaweza kufika. Hatupendi itokee lakini sheria
zipo.Utakuja siku ujibiwe vibaya na mtu sehemu, ukachukua silaha na
kumdunda kama ulivyofanya kwa mkeo, sheria ikachukua mkondo wake, jela
itakuwa inakuhusu.Achana na desturi ya kupiga, tumia njia mbadala
kumuadhibu mtu.
Kupiga hakusaidii. Kwa leo acha niishie hapo lakini ni matumaini
yangu utabadilika na kuwa mtu safi kama macho ya wengi yanavyokuangalia.
Ni hayo tu!
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


No comments:
Post a Comment