Leo
nataka kuzungumzia suala la uhongaji katika uhusiano. Kuhonga ni tabia
ambayo imeshamiri sana katika jamii yetu. Kipindi cha nyuma tumezoea
kusikia ama kuona wanaume wakiwahonga wanawake lakini sasa hivi mambo
yamebadilika.

Wanawake
nao wameingia katika mkumbo wa kuwahonga wanaume ili wakubali kuwa nao
kimapenzi tu ama waoane kabisa.Tabia hii imekuwa ikiwatia majaribuni
walio wengi hali ambayo imesababisha baadhi ya watu wenye tamaa za
kijinga kushawishika kufanya ngono na watu ambao katika mazingira ya
kawaida wasingeweza kufanya nao.
Ni
kitu cha kawaida kabisa kumkuta kijana wa kiume mwenye umri mdogo kuwa
na uhusiano wa kimapenzi na mama mtu mzima ambaye angeweza kuwa mama
yake. Lakini hafanyi hivyo kwa matakwa yake bali kwa kushawishiwa na
pesa ama vitu vingine vya thamani.
Kuna
utata kidogo katika neno hili kuhonga, wapo wanaojiuliza kwamba hivi
ninapompatia mpenzi wangu fedha kwa ajili ya matumizi madogomadogo
nitakuwa nimemhonga? Katika uhalisia neno kuhonga ni kitendo cha
mwanaume kutoa fedha ama zawadi kumpa mwanamke hasa pale anapomtongoza
ili awe mpenzi wake ama mke wake.
Pia
katika kamusi ya kiswahili sanifu neno hilo limetafsiriwa kama malipo
ama zawadi itolewayo ili kupata kile unachohitaji au kutaka jambo f’lani
liharakishwe, kwa maana nyingine ni rushwa.Maana halisi ya kuhonga
itapatikana kutokana na nia ya mwanaume hasa pale anapotoa pesa ama kitu
kingine kwenda kwa mwanamke. Kwa mfano kama unatoa pesa kwa ajili ya
kumsadia mpenzi wako ama kumkidhia haja mke wako kutokana na tatizo
fulani alilonalo, hapo haiwezi ikachukuliwa kwamba umemhonga.
Lakini
kama unatoa kitu ama pesa kutaka kulazimisha ama kumshawishi awe rafiki
yako, mpenzi wako, mke wako ama kwa kutaka kufanya naye mapenzi, hapo
itachukuliwa kwamba umehonga.Kikubwa unachotakiwa kujua ni kwamba,
hakuna uhusiano wowote baina ya mapenzi na pesa. Ndio maana mapenzi
yanaweza kuwepo hata pale pesa inapokosekana.

Kwa kudhibitisha hilo
wengi wanaopata penzi kwa njia ya kuhonga, mapenzi yao hayadumu kutokana
na mmoja kati ya wawili hao kushawishika kutengeneza uhusiano kutokana
na pesa ama kitu kingine.
Utafiti unaonesha kwamba, kwa wanaume walio wengi kuhonga ni sehemu ya maisha yao licha ya kwamba ni katika viwango tofauti.
Hakuna
mwanaume asiyehonga ukiachilia mbali wale ambao ni waumini kikwelikweli
ambao nao sina uhakika kama hawaingia katika kundi la wahongaji kwa
maana halisi ya kuhonga.Licha ya kwamba wapo pia baadhi ya wanawake
ambao wana tabia ya kuhonga wanaume ili wawapende, kasi imeonekana
kuwepo kwa wanaume ambapo hulazimika kutoa mamilioni ya pesa, magari,
simu za mikononi, na vitu vingine vya thamani kwa mabinti ili tu waweze
kuwa na uhusiano wa kimapenzi.
Kimsingi
niseme tu kwamba, katika uhusiano wa kweli baina ya wawili waliotokea
kupendana, suala la kuhongana hakuna. Usimpe mpenzi wako pesa ili
kumlainisha akufanyie jambo fulani kwani ipo siku utakuwa huna pesa na
unataka akufanyie, hapo ndipo mnaweza kuachana.
Msaidie
pale atakapohitaji msaada wako, kama nilivyowahi kusema huko nyuma
kwamba, hutakiwi kuwa mbahili kwa mwenza wako kwani wewe ni yeye na yeye
ni wewe.
No comments:
Post a Comment