SWALI:
Assalam
alaikum, mimi nawa andikia nikiwa mgeni katika dini hiyi ya ALLAH
ninayo mswali ambayo ningelipenda kujua majibu yake kwani yatachangia
kuniweka sawa na kuifuata vyema dini ya ALLAH.
NATAKA
KUJUA KWA NINI DINI YA ISLAM INARUHUSU MWANA UME KUOWA MKE ZAIDI YA
MMOJA (NA KUSUDIA KUOWA WAKE WENGI) NA KWA NINI DINI HAIMRUHUSU MWANA
MKEE WA KI ISLAM KUOLEWA NA MWANA UME ZAIDI YA MMOJA?
JIBU:
Sifa
zote njema Anastahiki Allaah Aliyetukuka Mola wa walimwengu wote,
Swalah na salamu zimshukie kipenzi chetu Mtume Muhammad (Swalla Allaahu
'alayhi wa aalihi wa sallam) na Swahaba zake (Radhiya Allaahu 'anhum) na
watangu wema mpaka Siku ya Mwisho.
Shukrani
ndugu yetu katika Iymaan kwa suala lako nyeti kuhusu mas-ala muhimu
katika Dini yetu tukufu ya Uislamu. ni jambo linaloeleweka kuwa Uislamu
ni mfumo kamili wa maisha ya mwanaadamu kwa ujumla na Waislamu hasa.
Japokuwa mfumo huu ambao unamtoa mtu matatani unakimbiwa na wengi.
Hakuna lolote isipokuwa Allaah (Subhaanahu wa Ta‘ala) na Mtume Wake
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) wametuelezea. Allaah
(Subhaanahu wa Ta‘ala) Anasema:
“Hatukuacha Kitabuni mwetu kitu chochote” (6: 38).
Hakika muulizaji, wewe
ulikuwa Muislamu lakini mazingira yamekufanya wewe ulelekee katika dini
nyengine isiyo ya kimaumbile. Hilo ni kwa mujibu wa Mtume wa Allaah
(Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam): “Kila
kinachozaliwa kinazaliwa katika Fitwrah (maumbile ya asli ya Uislamu
‘Tawhiyd’) ni wazazi wake ndio wanamfanya awe Myahudi au Mkristo au
Majusi” (Al-Bukhaariy).
Ukweli
ni kuwa si kila kitu kimeelezwa hekima yake lakini Wanachuoni
wanajitahidi kuangalia hekima ya mambo kadhaa ambayo yamo katika Qur-aan
Tukufu au Sunnah za Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam).
Hivyo, Imani ya Muislamu ni kuwa hata asipopata hekima ya amri au
katazo fulani basi yeye huwa ni mwenye kusema:
“Tumesikia na tumetii” (2: 285).
Waislamu huwa kabisa hawafuati ile sifa ya Mayahudi ya kusema: “Tunasikia na tunakataa” (2: 93).
Kwa
minajili hiyo, Muislamu huwa hapati shida kutii kwani anafahamu kuwa
Yule Aliyemuumba Ndiye Anayejua lililo zuri kwake na lenye kumfaa na
lililo baya kwake na lenye kumdhuru. Hii ni kanuni muhimu sana kwa kila
mmoja kati yetu, Waislamu kuifahamu. Ni ajabu kuwa Mjapani anatengeneza
gari akawa ni mwenye kufuatwa kikamilifu na aliyenunua gari. Mwenye gari
huyo huwa hata mara moja haendi kinyume na maagizo yaliyotolewa na
mtengenezaji huyo, kwani anajua kwa yakini kuwa akienda kinyume kwa
mfano badala ya kutia petroli katika injini, yeye akatia maji! Hivyo
gari halitaweza kufanya kazi. Vipi maagizo ya Allaah Aliyetukuka tuwe ni
wenye kuyapuuza? Jambo haliingii akilini lakini huwa tunakwenda
kinyume katika maamrisho Yake mengi. Tutanabahi na turudi Kwake kabla
hatujaondoka katika ulimwengu huu.
Hakika
ni kuwa Uislamu umehalalisha uke wenza na ukaharamisha mwanamke kuolewa
na wanaume wengi. Shari’ah hii iko wazi katika machimbuko ya shari’ah
ya Dini juu ya yote ikiwa ni agizo katika Qur-aan. Allaah (Subhaanahu wa
Ta‘ala) Anasema:
“Basi oeni mnaowapenda katika wanawake wawili au watatu au wanne. Na mkiogopa kuwa hamwezi kufanya uadilifu basi oeni mmoja tu” (4: 3).
Hii ni Aayah ambayo itabaki kutumika mpaka siku ya Qiyaamah.
Katika Sunnah, Mama wa Waumimi, ‘Aaishah (Radhiya Allaahu ‘Anha) amesema kuwa wakati wa Ujahiliya kulikuwa na ndoa aina nne:
1. Kama ilivyo wakati huu wetu wa sasa (yaani wakati wao na mpaka sasa kwa mwanamume kwenda kumposa binti kwa wazazi wake).
2. Mume
kwa kutaka apate mtoto mwenye sifa fulani alikuwa akizungumza na
mwanamume mwenye sifa hizo ili awe analala na mkewe. Katikahali hiyo
alikuwa mume mwenyewe akitoka kwenye hiyo nyumba mpaka mkewe apate
mimba. Akishika mimba alikuwa anarudi nyumbani, akitaka alikuwa
akimuingilia au akimngojea mpaka azae.
3. Mwanamke alikuwa anaolewa na wanaume wengi na pindi anapozaa alikuwa
akiwaita wanaume wote. Mjuzi wa kulinganisha sura alikuwa akiitwa na
atakaye chaguliwa alikuwa akichukua jukumu la kumlea mtoto huyo.
Madanguro
ambamo wanawake walikuwa wakiuza miili yao na juu ya nyumba hizo
kulikuwa na bendera yenye kuashiria hilo. Mtu yeyote alikuwa na uhuru wa
kuingia na kukidhi haja zake.
Alipotumilizwa
Mtume (Swalla Allaahu ‘alayhi wa aalihi wa sallam) aina zote za
mahusiano baina ya mume na mke zilikatazwa ila ile yiliyotaja katika
ipengele cha kwanza (Al-Bukhaariy).
Swali
la sisi kujiuliza ni, Je, uke wenza na utovu wa maadili? Kulijibu swali
hili ni lazima tuangalie dini nyengine kama Uyahudi na Ukristo unasema
nini kuhusu hilo kwani tushaona kuwa Uislamu umeruhusu mbali na kuwa
imeweka masharti yake. Kulingana na Uyahudi na ukitazama hasa katika
Agano la Kale utakuta kuwa Manabii watukufu wengi walikuwa na zaidi ya
mke mmoja kwa mfano Abrahamu alikuwa na watatu, Daudi mia moja, Suleiman
mia saba na wengineo. Hawa ni vielelezo kwa wenye kufuata dini hiyo.
Sasa
ikiwa hawa wana wake zaidi ya mmoja upo ubaya gani kwa wafuasi kuwa na
wake wengi. Ruhusa hii ya kuoa zaidi ya mke mmoja ilipigwa marufuku na
kikao cha Marabai cha Worms
katika karne ya 11. Katazo hili mwanzo lilitolewa kwa Mayahudi
waliokuwa wakiishi Ujerumani na Kaskazini mwa Ufaransa lakini baadae
ikawa ni kwa wafuasi wote.
Ukiangalia
Ukristo utakuta kuwa, kwa kuwa Agano la Kale ni sehemu ya Biblia ruhusa
hiyo itakuwepo bila ya matatizo yoyote. Ni yakini kuwa Yesu wa Biblia
alisema hakuna kubatilisha wala kufuta kanuni za Taurati bali kutimiza.
Na juu ya yote hayo hakuna hata msitari mmoja katika Agano Jipya
unaokataza uke wenza.
Westermarck
anasema kuwa hakuna kikao hata kimoja katika karne za awali za Kanisa
zilizokataza uke wenza. Wafalme walikuwa wakioa zaidi ya mke mmoja kwa
mfano mfalme wa Ireland kati ya karne ya sita alikuwa na malkia 2 pamoja
na masuria wawili pia. Madhehebu kadhaa yaliruhusu ndoa hizo bila ya
matatizo yoyote. Mwaka wa 1531 mhubiri wa Anabaptists akiwa Munster
alitangaza hadharani kuwa yule anayetaka kuwa Mkristo wa kweli ni lazima
aoe mke zaidi ya mmoja. Na ulimwengu wote unajua kuwa Mormons
wanachukulia uke wenza kama agizo la Mungu.
Hizi ni dalili zifuatazo kuhusiana na hayo:
Biblia
inatueleza kuwa Ibrahimu (Abramu) alikuwa na wake watatu kama
tunavyoelezwa: "…na Sarai mkewe Abramu…" (Mwanzo 11: 31). Tena: "Kisha,
Sarai akampa Abramu Hagari, mtumwa wake wa kike, Mmisri, awe mke wake"
(Mwanzo 16: 3).
Na
pia: "Abrahamu alioa mke mwingine, jina lake Ketura" (Mwanzo 25: 1).
Naye Ya'quub (Yakobo) alikuwa na wake wane kama tunavyoarifiwa na
Biblia: "Kisha Yakobo akamwambia Labani, 'Muda wangu umetimia, kwa hiyo
nipe mke wangu'. … Lakini jioni, Labani akamchukua Lea, binti yake
mkubwa, na kumpeleka kwa Yakobo. Yakobo akalala naye" (Mwanzo 29: 21 –
23).
Pia:
"Na Yakobo alipomtimizia Lea siku zake saba, Labani akampa Raheli,
binti yake mdogo awe mke wake" (Mwanzo 29: 28). Tena: "Kwa hiyo Raheli
akampa Yakobo mtumishi wake, Bilha, awe mkewe, naye akalala naye"
(Mwanzo 30: 4).
Pia: "Lea alipoona ameacha kuzaa, alimtwaa Zilpa, mtumishi wake wa kike, na kumpa Yakobo ili awe mkewe" (Mwanzo 30: 9).
Biblia
inatufahamisha tena kuwa kumbe anayefaa kuwa na mke mmoja ni askofu
kumaanisha asiyekuwa askofu anaweza kuwa na zaidi ya mmoja. Hebu tusome:
"Basi, askofu anapaswa kuwa mtu asiye na lawama; anapaswa awe na mke
mmoja tu, awe mwenye kiasi, nidhamu na utaratibu" (1 Timotheo 3: 2).
Sijui kwa nini maaskofu wa Kikatoliki hawaruhusiwi kuoa kabisa?
Mwingine
anayefaa kuwa na mke mmoja ni mzee wa Kanisa kama tunavyoarifiwa: "Mzee
wa Kanisa anapaswa kuwa mtu asiye na hatia; aliye na mke mmoja tu, na
watoto wake wanapaswa kuwa waumini" (Tito 1: 6).
Ni
jambo linalojulikana kuwa hata wale wenye kufuata dini za kitamaduni
hasa za Kiafrika wanachukua uke wenza kama jambo la kawaida kabisa.
Hivyo, katika sehemu ya Kenya wamisheni walibidi wakubali hao kushika
baadhi ya mila zao ili wawavutie kuingia katika Ukristo.
Ifahamike
kuwa Aayah tuliyoinukuu juu (4: 3) ina maelezo ambayo yanafaa yaeleweke
ili tuweze kuwa na ufahamu mzuri wa suala hili la uke wenza katika
Uislamu. Dondoo zifuatazo zitatusaidia:
· Uke wenza si lazima lakini ni jambo linaloruhusiwa.
· Ruhusa
hiyo si kutekeleza uchu wa mwanamume wa kujitosheleza kimapenzi bali ni
kuweza kuwa na huruma kwa wajane, mayatima na wanawake wengineo.
· Hata katika hali hiyo ya ruhusa uke wenza umewekewa kikwazo kuwa mwanamume hawezi kuoa zaidi ya wanne.
· Mwanamume
ni lazima awafanyie uadilifu wake zake wote. Huu ni wajibu, na
unahusu makazi, chakula, mavazi, na kuwatendea wema. Haya ni majukumu ya
mume.
· Aayah
inasema “oa” sio kuteka nyara, kubaka au kutongoza. Kwa hiyo, mwanamke
hawezi kushurutishwa au kupatiwa mwanamume ambaye yeye hamtaki.
Swali
ambalo linaweza kujitokea ni kuwa, je uke wenza unaweza kuwa ndio
suluhisho la matatizo yetu ya kijamii? Kabla ya kujibu swali hili
tungependa kusema kuwa Uislamu umekuja na shari’ah yenye kuwafaa watu
wote kwa zama zote na katika nchi zote. Kwa ajili hiyo haukuweka
shari’ah kwa watu wa mijini na kuwasahau watu wa mashambani, au kwa nchi
za baridi na kuwapuuza watu katika nchi za joto, au kwa nyakati fulani
ikasahau zama zijazo na vizazi vijavyo. Uislamu unakisia dharura na haja
za kila mmoja binafsi na jamii kwa ujumla wake.
Kadhaalika ni vizuri tutazame vipengele vifuatavyo:
1. Mume
anayegundua kuwa mkewe hazai kwa sababu ya utasa, maradhi au kwa sababu
nyengine yoyote ile. Je, si bora kwa mwanamke, na ni afadhali kwake
yeye mwanamume; kuoa yule atakayemhakikishia raghba hiyo ya kupata mtoto
na kubaki na mkewe wa kwanza. Bila kufanya hivyo atabaki bila watoto na
kukosa ubaba au amuache mkewe na kuoa mke mwengine. Suluhisho hizo
mbili zote hazifai na inabaki kwetu kuukubali uke wenza.
2. Mwanaume
mwenye mke ambaye wakati wote ni mgonjwa au ana wakati mrefu wa hedhi.
Mume anaweza kuwa na uchaguzi wa kukandamiza matamanio yake kwa uhai
wake wote au amuache mkewe aliye mgonjwa wakati ambao mke anahitaji
huruma zaidi au anaweza mume kubaki naye lakini akawa na vimada nje ya
ndoa. Ukitazama haya mambo matatu utakuta kuwa la kwanza ni dhidi ya
maumbile ya mwanadamu. Uislamu unatambua mahitaji ya kutimiza matamanio
ya kimwili. Suluhisho la pili si la huruma hasa kukiwa na mapenzi baina
ya wawili wapendanao. Suluhisho la mwisho ni dhidi kabisa na mafundisho
ya Uislamu ambayo yanakataza zinaa wazi wazi. Kwa kuwa Uislamu uko dhidi
ya utovu wa maadili, unafiki wa kitabia na talaka ila kwa dharura
zisizoepukika, mbadala muafaka ni uke wenza.
3. Kimaumbile wanaume wana shauku kubwa zaidi kuliko wanawake na hivyo kuweza kuwamudu wake wengi.
4. Kimaumbile
upo wakati mrefu ambapo mwanamke hawezi hutekeleza majukumu yake ya
kindoa kwa mabadiliko ya kisaikolojia na kifiziolojia na kimwili kama
wakati akibeba mimba, hedhi na nifasi. Katika hali ya kwanza wapo
wanawake huwa hawataki kuonana hata na mwanaume na katika mbili za
mwisho Uislamu umekataza mume kumuingilia mkewe.
5. Inajulikana
kuwa wanawake ni wengi zaidi katika ulimwengu. Na vita ambavyo
vinaendelea ulimwengu mzima vinawaacha wajane wengi zaidi na watoto
wanaokosa mapenzi ya baba. Je, hawa wanawake wa ziada watimize uchu wao
vipi? Ni maslahi ya kijamii kuwa wanawake wawe ni wenye kuolewa na hivyo
kupata himaya ya kifamilia. Kawaida hawa wanawake huwa wana hamu ya
kuolewa, nao hawana ila njia tatu mbele yao: Kuishi umri wao bila ya
kuolewa; au walegeze hatamu wakiishi huku wakitumiwa na wanaume kwa
kutimiza matamanio yao; au waolewe na waume wengine wenye uwezo wa
kuwatazama. Suluhisho ni kuchukua msimamo wa tatu wa kuoa wake wengi.
6. Ipo
shida kubwa sana Marekani na nchi za Bara Ulaya ambapo kumepigwa
marufuku mume kuoa mke mwengine. Kwa sababu ya kanuni hiyo iliyo kinyume
na maumbile ya mwanadamu utawakuta wanaume wengi wana vimada nje ya
ndoa. Wanazaa nao watoto lakini hawana jukumu lolote la kuwatazama, kwao
ni kutimiza haja yao ya kimapenzi tu.
7. Mitume
(‘Alayhimus Salaam) ambao ni kielelezo kwetu walikuwa na wake wengi
hata katika Biblia kwa nini hatufuati mienendo yao kwani wao wamekuja na
maisha yaliyo bora kabisa.
8. Wanawake
wengi katika jamii tofauti ulimwenguni wanafadhilisha waume wenye wake
wengi (tazama Campbell, D., In the Heart of Bantuland, uk. 160).
Mbali na hayo yote tuliyoyasema linajitokeza swali:
Kwa nini mwanamke asiolewe na waume wengi?
Katika hili tunasema yafutayo:
1. Ni
hakika kuwa maumbile ya mwanamke kisaikolojia na fiziolojia ni tofauti
na mwanaume. Kisaikolojia ni kuwa mwanamke anatosheka na mume mmoja.
Kifiziolojia mwanamke hawezi kujimudu kuwa na wanaume zaidi ya mmoja kwa
sababu ya mabadiliko ndani ya mwili wake.
2. Katika
tamaduni zote, za zamani na sasa, uongozi wa nyumba (familia) ni wa
mwanaume. Unaweza kufikiria katika familia ambayo ina kiongozi zaidi ya
mmoja, nyumba hiyo itaendeshwa vipi? Ndio wahenga wakawa na msemo:
“Fahali wawili hawakai kwenye zizi moja”.
3. Mwanamke
huyu ataweza vipi kuwaridhisha wanaume hao wote katika chakula na
mapenzi. Tuseme kuwa utawagawia siku, mmoja wao anakuja na mke huyo yuko
katika hedhi naye ana shauku ya juu sana, atafanyaje? Je, mke atachukua
amri kutoka kwa nani?
4. Mke anayeolewa na mume zaidi ya mmoja, anaposhika mimba itakuwaje? Mtoto huyo atakuwa wa nani?
No comments:
Post a Comment