HAYA NDIO MAMBO MAKUU 5 YA KUSHANGAZA WAKATI WA MAZISHI YA NGWEA..!!
HUKU Albert Kenneth Mangwea ‘Ngwea’ akiwa kaburini siku ya pili leo kufuatia kufariki dunia ghafla usingizini nchini Afrika Kusini, Mei 28, mwaka huu, mambo matano ya kushangaza yamezuka katika kipindi chote cha msiba, Risasi Jumamosi linakupa kila kitu.
Kwa mujibu wa utafiti wetu wa kina, waombolezaji mbalimbali wamekuwa wakiyazungumzia mambo hayo huku wengine wakihoji kuwepo kwake.
1. RIPOTI YAFICHWA KIBINDONI
Usiku wa kuamkia mazishi yaliyofanyika kwenye Makaburi ya Kihonda, Morogoro, paparazi wetu alipata bahati ya kuzungumza na mama wa marehemu Ngwea, Denisia Mangweha.
Katika mazungumzo hayo, mwanahabari wetu alimuuliza mama huyo kama alikuwa amekabidhiwa ripoti ya daktari inayotatua fumbo la nini kilimuua Ngwea.
Haya hapa majibu ya mama huyo:
“Sijapata wala sijui chochote kuhusu hiyo ripoti, wala sijui nani anayo.”
Jumanne iliyopita, ilidaiwa kuwa Mtangazaji wa Clouds FM, Millard Ayo aliyekuwa ‘Sauzi’ ndiye aliyekabidhiwa ripoti hiyo ambapo na yeye aliikabidhi kwa ndugu wa marehemu.
Kwa kawaida, ripoti inayoweka wazi kiini cha kifo cha marehemu husomwa siku ya mazishi, jambo ambalo halikufanyika siku ya kumzika Ngwea.
MANENO YA WATU MAKABURINI
Baadhi ya waombolezaji waliokuwa makaburini hapo, walitoa hisia zao wakidai kwamba, inawezekana ripoti hiyo haikuwa nzuri hivyo ili kulinda heshima ya marehemu ililazimika kuiacha kibindoni.
2. MAMA WA MAREHEMU AMTAMBUA DEMU MZUNGU
Jumatano, siku moja kabla ya mazishi, mama wa marehemu alimshika mkono aliyekuwa mchumba wa marehemu, yule mwanamke Mzungu akisema Albert (Ngwea) alikuwa akienda naye nyumbani hapo (Morogoro).
Alisema mara kadhaa walitoka yeye, marehemu na Mzungu huyo kwenda kula ‘bata’ mahali kabla ya kurejea Dar. Kwa hiyo Mzungu ni mwanamke aliyekuwa akitambulika na mama wa marehemu.
Cha kushangaza, dada wa marehemu aitwaye Neema Mangweha, alisema mchumba wa marehemu anayemjua yeye anaitwa Siwema ambaye kwa sasa ana ujauzito wa mwanamuziki maarufu wa muziki wa kizazi kipya Bongo.
3. MTOTO WA MAREHEMU AIBUKIA MAKABURINI
Alhamisi, wakati msafara wenye mwili wa marehemu ukiwa makaburini, mwanamke mmoja aliyejitambulisha kwa jina la Paulina Jeremiah akiwa na mtoto wa kike alijitokeza hadharani na kukutana uso kwa uso na paparazi wetu akidai mtoto huyo ni wa marehemu Ngwea.
Mwanamke huyo, mkazi wa Kigamboni, Dodoma alisema mtoto huyo anaitwa Neema Albert, alimzaa mwaka 2001 wakati huo Ngwea alikuwa akisoma Sekondari ya Mazengo.
Wakati anajieleza hayo, ndugu wawili wa marehemu walitokea, mmoja akiitwa Anthony Kenneth Mangweha na kumsikiliza mama Neema.
Anthony alimuuliza mama Neema kama kuna ndugu yeyote wa marehemu anayetambua uwepo wa mtoto huyo, mama Neema akawataja.
Aliwataja vijana watatu kwa jina mojamoja, Frank, Jotam na Amani ambapo alisema waliwahi kutumwa na marehemu kwenda Dodoma kumwangalia mtoto huyo.
Anthony alikiri kuwa vijana hao watatu ni ndugu wa familia hiyo na akamtaka mama Neema kupoa, baada ya mazishi na kurudi nyumbani watakaa kuzungumzia suala hilo.
4. M 2 THE P AIBUKIA KWENYE KUAGA MWILI
Katika hali iliyowashangaza wengi, msanii wa Bongo Fleva aliyepata matatizo na marehemu lakini yeye akapona, Mgaza Pembe ‘M 2 THE P’ aliibuka kwenye Uwanja wa Jamhuri mjini Morogoro ambako mwili wa marehemu ulikuwa ukiagwa.
Baadhi ya watu waliomtambua msanii huyo walionekana kumshangaa sana huku wakihoji ametua lini kutoka Sauzi.
M 2 The P alishindwa kuhimili wakati anapita kwenye mwili wa marehemu, alimwaga machozi, hali iliyosababisha waombolezaji wawili kumshika kulia na kushoto na kumtoa eneo hilo.
MAVAZI YAKE SASA!
Kikubwa kilichoibua maswali kutoka kwa waombolezaji ni jinsi msanii huyo alivyovaa. Wengine waliamini vaa yake ilisababishwa na kutaka kujificha watu wasimtambue. Pia wapo waliodai inawezekana alitoroka huko Sauzi.
Alivaa suruali ya ‘jinzi’, fulana ya mikono mifupi, miwani na kofia kubwa licha ya
hali ya hewa Morogoro kuwa si ya baridi sana kiasi cha kuvaa hivyo.
5. KUMBE MAREHEMU ALITUMIWA FEDHA SAUZI
Tofauti na mashabiki wake walivyoamini kuwa marehemu alikuwa akipiga fedha ndefu Sauzi na kuzituma Bongo kwa wanafamilia, mmoja wa ndugu zake alibumburua siri kuwa kuna wakati hali ilikuwa mbaya hadi ikabidi amtumie shilingi laki moja na nusu.
“Watu wanadhani labda Albert (Ngwea) alikuwa mambo safi muda wote Afrika Kusini kama vijana wengi wanavyoamini. Si kweli kuna wakati kabisa alikuwa akinipigia na kuniambia hali ilivyokuwa mbaya,” alisema ndugu huyo kwa sharti la kutotajwa gazetini.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment