KESI ya Nabii na Mtume Josephat Elias Mwingira wa Kanisa la Efhata,
kudaiwa kuzaa na mke wa Dk. William Morris, Dk. Phillis Nyambi
inaendelea kuunguruma katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu jijini Dar
ambapo mlalamikiwa huyo wa pili katika shauri hilo amekiri kuzaa nje ya
ndoa.
Mlalamikiwa huyo, Dk. Phillis Morris Nyambi katika majibu yake ya
kimaandishi yaliyotolewa Januari 22, mwaka huu mahakamani hapo (nakala
tunayo), amekiri kuzaa na mtu ambaye alisema hamfahamu wala hajui
alipo!!
Mwanamke huyo ambaye kitaaluma ni daktari kama alivyo mumewe, raia wa Liberia, amekana kuzaa na Nabii Mwingira.
ATOA SABABU ZA KUZAA NJE YA NDOA
Wakili Mbogoro
anayemwakilisha mahakamani Dk. Phillis alisema mteja wake yalimpata ya
kuzaa nje ya ndoa baada ya mlalamikaji (mume) kumtelekeza kwa miaka
saba, kuanzia 2002-2009.
“Mlalamikiwa wa pili akiwa ni binadamu akajikuta akishindwa majaribu,” alisema wakili huyo katika majibu hayo.
Aliongeza kuwa mlalamikaji alielezwa hali halisi na akamhakikishia
mlalamikiwa mbele ya wazee kwamba anapaswa kulaumiwa na atamtunza mtoto
aliyezaliwa nje ya ndoa kama wake.
Hata hivyo, mke huyo aliiambia mahakama kuwa kila mtu ajiulize kwa
nini mlalamikaji amekuja juu kuhusiana na mtoto aliyezaliwa nje ya ndoa
na sababu gani hajachukua hatua yoyote baada ya miaka mitatu tangu
azaliwe (2009 hadi 2012) licha ya kudaiwa kuwa shauri hilo lilifikishwa
polisi.
OMBI LA KUPIMWA UKIMWI
Kuhusu ombi la
mlalamikaji kuitaka mahakama iamuru walalamikiwa Nabii Mwingira na Dk.
Phillis kupimwa Virusi vya Ukimwi, Wakili Mbogoro amelipinga kwa madai
ya kesi kupitwa na wakati.
Akifunga utetezi wake, Mbogoro ameitaka mahakama kuitupilia mbali kesi hiyo na mlalamikaji kulipa gharama.
Dk. Morris anayewakilishwa na Wakili Desidery Ndibalema amemshitaki
Nabii Mwingira kama mlalamikiwa namba moja na mke wake mlalamikaji, Dk.
Phillis ni mlalamikiwa wa pili na tayari shauri hilo lililopelekwa
mahakamani Novemba 21, mwaka jana limepewa jalada lenye usajili namba
306 la 2013 katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar.
Mlalamikaji amedai kuwa wawili hao wamemvurugia ndoa yake baada ya kujiingiza katika uhusiano wa kimapenzi na kuzaa mtoto mmoja.
Kutokana na mambo hayo, ameiomba mahakama iwaamuru walalamikiwa hao wamlipe fidia ya shilingi bilioni 7.5.
Dk. Morris alifunga ndoa na Dk. Phillis Desemba 28, 2001 katika Kanisa la Saint Albano, Upanga jijini Dar.
MWINGIRA KIMYA
Mpaka mahakama inaahirisha kesi
hiyo, Nabii Mwingira hakuwa amewasilisha utetezi wake na shauri hilo
limepangwa kusikilizwa tena Februari 22, mwaka huu.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment