Dodoma/Dar es Salaam. Ni
matukio nadra kutokea katika maisha, lakini haya ndiyo yaliyomkuta
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Vicky Kamata, baada ya kuugua ghafla saa
36 kabla ya harusi yake.
Kuugua kwa bibi harusi
huyo mtarajiwa, kumezua gumzo katika Viwanja vya Bunge mjini Dodoma na
maeneo mengine nchini, kutokana na kile kilichoelezwa kwamba harusi hiyo
ilipangwa kuwa ya kifahari ikitarajiwa kutumia Sh96 milioni.
Kamata ilikuwa afunge ndoa jana katika Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi, Sinza Dar es Salaam na tayari kadi za mialiko zilishasambazwa kwa watu mbalimbali wakiwamo wabunge.
Habari za
kuugua ghafla kwa mbunge huyo ambaye pia ni msanii wa muziki aliyetamba
na kibao chake cha ‘Wanawake na Maendeleo’ zilianza kuzagaa kwa kasi
juzi jioni nchini.
Kamata
ambaye pia ni mtetezi wa haki za wanawake, aliugua usiku wa ijumaa
kuamkia jumamosi na kupelekwa katika Hospitali ya Tabata General,
iliyopo Segerea ambapo amelazwa.
“Niliugua
tumbo ghafla, nilipata maumivu makali sana nikampigia daktari wangu na
nilipomweleza jinsi ninavyojisikia, aliniambia niende hospitali haraka
na kutokana na hali ilivyo, waliamua nilazwe,” alisema Kamata akiwa
kitandani katika hospitali hiyo.
Kamata alifafanua kuwa, pamoja na mambo mengine, hali yake ya ujauzito imekuwa ikimsumbua na kuchangia yeye kulazwa kwa mara ya
pili sasa katika kipindi cha wiki mbili. Mbunge huyo ambaye alitakiwa
kufunga ndoa leo, alisema kuwa kutokana na maradhi hayo, haelewi hatima
ya ndoa yake, ingawa wanafamilia na wanakamati wanaendelea na mipango ya
harusi kama ilivyopangwa.
“Mama
anaenda nyumbani sasa hivi kuniandalia nguo na kila kitu, lakini sijui
itakuwaje kwa sababu daktari amesema kutokana na hali yangu ilivyo,
itakuwa vigumu kuvaa viatu virefu na kupata usumbufu wote wa purukushani
za harusi,” alisema.
Aliongeza kuwa mipango yote ya harusi ipo tayari kinachosubiriwa na siku yenyewe, lakini kwa bahati mbaya jambo hilo limetokea na haliwezi kuepukika.
Vicky
alisema wanakamati wa Dar es Salaam na wale wa Dodoma, wanaendelea na
vikao ingawa, wamechanganyikiwa kutokana na sintofahamu iliyopo, kama
harusi itafanyika au haitafanyika.
Ndugu wa
mbunge huyo akiwemo mama yake mzazi Kamata walionekana hospitalini hapo
wakiendelea kumfariji na kujadili kuhusu hatima ya harusi hiyo,
iliyokuwa ikingojewa kwa hamu na wanafamilia wote.
Daktari wa
Kamata, aliyefahamika kwa jina la Diwani Msemo, alieleza kuwa mbunge
huyo alifika hospitalini hapo akiwa na maumivu makali ya tumbo
yaliyofanana na uchungu wa kuzaa, hali iliyoonyesha kuwa ujauzito wake
unatishia kutoka.
“Ukipata
yale maumivu kama mimba ni changa inakuwa kama tishio la mimba kutoka,
siyo hivyo tu, bali alikuwa anatapika na presha ikashuka. Kwa kweli
mimba yake ipo katika hatari,” alisema
Alisema
pamoja na kumpa matibabu, walishauriana kuwa apumzike kwa siku tano ili
kuhakikisha kiumbe kilichopo tumboni kipo salama.
“Ilikuwa ni
uamuzi mgumu kwa sababu ni siku yake ya harusi, lakini tunaangalia
umuhimu wa kiumbe na kama ataenda, itabidi asaini ili ijulikane kuwa
hatukumkubalia. Kwa kifupi hayuko fiti kwa shughuli hiyo,” alisema.
Harusi ya
Kamata iliandikwa pia na mitandao mbalimbali ya kijamii nchini na jana
redio moja ilitangaza kuugua kwake, ikisema kumetokana na matatizo ya
ujauzito.
Kumekuwa na
uvumi unaosambazwa kwa kasi juu ya sababu za kuahirishwa kwa harusi
hiyo, lakini kwa sababu ya maadili ya uandishi hatutaweza kuziandika
katika gazeti hili.
Paroko aliyekuwa afungishe ndoa anena
Padri wa
Kanisa Katoliki Parokia ya Bikira Maria Mama wa Mkombozi , Sinza Dar es
Salaam, Cuthbert Maganga alipohojiwa kuhusu taarifa za kufungwa kwa ndoa
hiyo, alikiri kwamba iliandikishwa ili ifungwe kanisani hapo.
Hata hivyo
akasema ilishindikana, baada ya wahusika kukwama kuwasilisha baadhi ya
nyaraka muhimu zilizohitajika, ili kukamilisha sakramenti hiyo.
“Ilitarajiwa
kufungwa Mei 24 mwaka huu yaani jumamosi (jana), lakini kwa taratibu
za kanisa letu ilishindikana kwa sababu bibi harusi alishindwa
kuwasilisha cheti chake cha ubatizo, pia hakuwa amepata kipaimara, vitu
hivyo ni miongoni mwa vitu muhimu vinavyohitajika ili kukamilisha
Sakramenti ya Ndoa,” alisema Padri Maganga.
Alisema Kamata ndiye aliyekwenda kuandikisha ndoa hiyo, kwa kuwa ni muumini wa kanisa hilo anayetokea Kanda D.
Juhudi za
kumtafuta bwana harusi, Charles Gardner hazikuweza kufanikiwa baada ya
simu yake kuita bila kupokelewa, hata alipotumiwa ujumbe wa maandishi
hakuwa tayari kujibu.
Hata hivyo,
baadhi ya rafiki wa karibu wa Gardner walieleza kuwa wamejulishwa kuwa
ndoa hiyo haipo na kwamba jana bwana harusi huyo mtarajiwa alionekana
akiwa katika hali isiyo ya kawaida.
“Nilijaribu
kumuuliza kuhusu harusi yake, lakini hakuwa tayari kunieleza bayana, ila
hayupo katika hali yake ya kawaida,” alisema mmoja wa rafiki zake.
Chanzo - Mwananchi
No comments:
Post a Comment