ATAKUPENDA TU, IKIWA UTAWEKEZA UPENDO KWAKE

KUPENDWA na kupendana hakuji kwa bahati mbaya. Si kweli kwamba wapenzi wanapokutana kwa mara ya kwanza tu wanakuwa wamependana kwa dhati. Mapenzi hutengenezwa!
Hujengwa na kulindwa kwa muda mrefu. Kuna wakati ukifika, utaona hisia zako zinazidi kukua na kumpenda zaidi mwenzi wako. Si jambo la kushangaza ni matokeo ya wekezo la penzi kutoka kwa mwenzi wako.

Hii inamaana kwamba, waliopendana kwa dhati leo, wakafunga ndoa kwa furaha mbele ya mashahidi, miaka mitano ijayo wanaweza kuchukiana!
Wanaweza kujuta ni kwa nini walioana. Hapo ni kwa sababu kuna mmoja kati yao au wote walishindwa kutengeneza mapenzi katika maisha yao halisi. Rafiki zangu, hapa nazungumza zaidi na wanandoa. Namna ambavyo wanatakiwa kudumisha upendo na kuwekeza kwa wenzao ili maisha yazidi kuendelea kwa amani.
CHETI KWANZA, MTIHANI BAADAYE
Kuna msemo mpya hivi sasa unatamba mitaani, unaweza kuonekana wa kuchekesha lakini una maana kubwa sana.

Watu mitaani wanasema, kozi zote duniani, mwishoni unafanya mtihani kwanza kisha wanapewa vyeti lakini kwenye ndoa unatangulia kupewa cheti kwanza, halafu mtihani baadaye!
Si jambo dogo. Ukichukulia kawaida itakuwa ni kosa, maana ni kweli kuwa, wanandoa wanapofunga ndoa, hupewa vyeti, tena kwa furaha kabisa lakini maisha halisi ndiyo mtihani wenyewe.

Inahitajika hekima ya hali ya juu, kuishi kwenye ndoa huku ukiwa na hakika kuwa kutofautiana ni jambo la kawaida kabisa. Huwezi kuishi kwa amani siku zote.
ACHANA NA MANENO MAKALI
Kuna baadhi ya watu wanapenda kutumia maneno makali sana kwa wenzi wao. Mwenzake akikosea kidogo tu, tayari ameshamcharukia kwa maneno rundo!
“Wewe ulikuwa kwa wanawake zako tu, siyo bure. Haya we’ endelea tu.”
Kauli kama hiyo haina maana kabisa kwenye ndoa zaidi inaharibu tu maelewano.

USIONGOZWE NA HISIA
Kwa bahati mbaya kuna watu ambao huwa na mawazo mabaya dhidi ya wenzi wao. Akili zao zinakuwa za ‘kujiongeza’ kila wakati. Hana mema anayowaza kuhusu mwenzake.
Kukitokea jambo dogo, atafikiri labda mwenzake alikuwa kwenye mazingira mabaya. Unapokuwa na fikra mbaya dhidi ya mwenzako ni kichocheo cha maneno makali na mwisho huharibu moyo wa kupenda.

TAMBUA NAFASI YAKO
Hapa zaidi ni kwa wanawake. Kuna wanawake ambao hawatambui nafasi zao na kama wanatambua basi hawataki kusimama katika nafasi hizo.
Mwanaume siku zote ndiye kichwa cha nyumba. Anatakiwa kusikilizwa, kuheshimiwa na kunyenyekewa. Ndoa yenye mwanamke mwenye kiburi, mbabe, maneno mengi na mwenye kutaka kuongoza familia, akichukua nafasi ya baba, siyo ndoa tena.

MALIZA MATATIZO HARAKA
Hakuna jambo la hatari kama kudumisha matatizo ndani ya ndoa. Iko hivi, hakuna ndoa isiyo na migogoro hata siku moja. Jambo la msingi ni kumaliza matatizo haraka.
Tafuta njia bora, zungumza kwa hekima. Acha papara, mwenzi wako atakuelewa bila shaka yoyote.

WEKEZA UPENDO
Upendo lazima uwekezwe. Kwa kauli chafu, dharau, kiburi na tabia nyingine za hovyo, huwezi kujenga uhusiano bora. Onyesha unavyompenda mwenzako.

Acha kumuumiza, wekeza zaidi na zaidi kwa mwenzi wako ili azidi kukupenda. Akikupenda zaidi nawe utampenda zaidi. Mtapendana zaidi na mtaishi maisha yenye furaha na amani zaidi.
Usiwaone leo wanapendana hata baada ya miaka 20 ya ndoa yao – waliwekeza upendo. Usishangae leo wanafarakana wakati juzi walikuwa pamoja kwa amani na upendo, kuna mmoja wao ameharibu upendo. Amechafua moyo wa mwenzake, hapo sababu ya kupendana huondoka.
Joseph Shaluwa ni Mshauri wa Saikolojia ya Uhusiano anayeandikia Magazeti ya Global Publishers. Kwa sasa anaandaa kitabu chake kipya cha Maisha ya Ndoa.
ujasiriamali

No comments:

Post a Comment

 
Support : WELCOME AGAIN MDADISI
Copyright © 2011. MDADISI WA MAMBO
THIS IS MDADISI
Proudly powered by Blogger