James Chotamasogo akitembelea magongo baada ya kukatwa mguu wa kushoto katika Hospitali ya Ocean Road, kutokana na ugonjwa wa kansa.
Kufuatia tukio hilo, kijana huyo ambaye ni yatima amekosa pakwenda hali iliyomfanya Kanali Kipingu kuchukua jukumu la kumlea.Mwandishi wetu alimtembelea katika Hospitali ya Magonjwa ya Kansa ya Ocean Road, jijini Dar wiki iliyopita ambapo alikuwa na haya ya kusema:
“Mimi ni mtoto wa pili kati ya watatu katika familia yetu, nikiwa mdogo baba aliugua akafariki dunia, tulibaki na mama ambaye muda wote alizidiwa na majukumu, hata hivyo naye hakuchukua muda kwani baada ya miezi miwili tangu baba afariki naye akaaga dunia, tulibaki peke yetu tukiwa hatuna uwezo wa kujihudumia.
“Tulikuwa tukiishi kwa kutegemea kilimo na uvuvi wa samaki katika Kijiji cha Ndewele, Kilolo mkoani Iringa.
Maisha yalizidi kuwa magumu lakini nilipofanya mtihani wa kuhitimu darasa la saba, nilifaulu kwenda kidato cha kwanza tatizo hapakuwa na mtu wa kuninunulia vifaa vya shule.
Kufuatia hali hiyo, nikaja Dar kutafuta kazi ambapo nilipata kibarua cha kutunza bustani na mifugo.
“Nilimweleza bosi wangu huyo kuwa bado nilihitaji kuendelea na masomo, alikubali kunisomesha kwa kunilipia ada kutokana na mshahara wangu. Nilisoma kwa bidii nikijua nitabadili maisha ya familia yetu.
“Siku moja nikiwa naendesha baiskeli nikiwa nimebeba majani ya ng’ombe, niligongwa na gari eneo la Kimara, nikaangukia mtaroni.
“Niliumia lakini nilijikokota hadi nyumbani kwa bosi wangu, wakati huo hakuwepo, alikuwepo mke wake ambaye hakunijali wala kunipeleka hospitali, damu ilivilia katika mguu wa kushoto, nilitumia barafu kuukanda ili kupunguza maumivu, nilikuwa naenda shule huku naumwa, baadaye nilishindwa kufanya shughuli za nyumbani, wakanifukuza nikiwa kidato cha tatu.
“Mzee mmoja alinionea huruma alinichukuwa nikawa naishi kwake, ada ya shule nikawa silipiwi bali chakula na pa kulala nilipewa, baada ya siku chache nikafukuzwa shule kwa kukosa karo.
“Nilienda kwa msaidizi wa mkuu wa shule nikamweleza matatizo yangu ili nisilipe ada, alifikisha kilio changu kwa mmiliki wa shule ambaye ni Kanali Kipingu, alikubali nisome bure na niishi pale shuleni bwenini.
“Mguu wangu ulizidi kuuma nikawa nashindwa kwenda shule,
Kanali Kipingu alinipeleka Hospitali ya Bagamoyo,Lugalo, IMTU na Nasana nako ikashindikana kupona ndipo akanipeleka Kibaha kwa Dk. Bake aligundua nina ugonjwa wa kansa ambayo ilitokana na kucheleweshwa kutibiwa majeraha niliyopata, nilihamishiwa Hospitali ya Taifa Muhimbili, madaktari walinieleza kwa hali iliyofikia, mguu ulitakiwa kukatwa wakashauri nifanye kwanza mtihani wa kuhitimu kidato cha nne.
“Ilinibidi nifanye mtihani, lakini kwa mawazo kwani nilifikiria maisha yangu yatakavyokuwa huko mbeleni, kwa sasa nipo hapa Hospitali ya Ocean Road nimekatwa mguu na naendelea na matibabu, natakiwa kununua mguu wa bandia kwa shilingi milioni moja na laki mbili.
“Nawashukuru madaktari walionihudumia kwani wakati wowote naweza kuruhusiwa, sina mahala pa kwenda lakini namshukuru Kanali Kipingu kwa kuniruhusu nirudi kwenye bweni nikaendelee kukaa na wanafunzi wenzangu. Naomba msaada kwa Watanzania wote.”
Aliyeguswa na habari ya James anaweza kumsaidia kupitia namba zake ambazo ni 0716 101980 au 0753 358172.
No comments:
Post a Comment