Awali
ya yote naomba niseme kwamba, raha ya ndoa ni kumpata mtu ambaye anajua
maisha na anajua mapenzi pia. Ukipata mwanamke ambaye anajua kutafuta
pesa tu lakini kwenye ulimwengu wa mapenzi ni limbukeni, atakusumbua
sana.
Lakini
pia ukijichanganya ukaoa mwanamke ambaye ni mtaalam wa mapenzi lakini
hajui pesa inavyotafutwa, nalo ni tatizo licha ya kwamba kwa wengine si
tatizo kwani wapo ambao hawataki kuoa wanawake wenye vipato kutokana na
yale yanayosemwa kuwa, baadhi yao wakijua kutafuta pesa,wanakuwa na
kiburi.
Hata hivyo, kwa wanaume wanapofikia muda wa kuoa kila mmoja huwa na
chaguo lake. Kila mtu atakuwa na vigezo vyake ambavyo vinaweza
kutofautiana kutoka kwa mmoja hadi kwa mwingine.
Tofauti hiyo
inakuja hata kwenye suala la tabia na uzuri. Kwa mfano, wapo ambao
wanaangalia sana suala la tabia nzuri na muonekano mzuri pia.
Lakini unaweza kushangaa mwanaume akatafuta mwanamke ambaye anakunywa
pombe na anayependa kujirusha kwa kuwa na yeye ni mtu wa mambo hayo.
Aidha, wanaume wengine watakuambia hawataki kuoa wanawake wanaokunywa
pombe, wanaoendekeza mambo ya anasa. Wanataka wanawake wa kutulia
nyumbani, wanaomjua Mungu.
Huo ni utofauti mdogo tu kwa baadhi ya wanaume wanapochagua wanawake wa kuingia nao kwenye ndoa.
Hata hivyo, hili suala la kutaka kuoa mwanamke mzuri huwa lina
tofauti ya aina yake. Mwanamke ambaye wewe unaweza kuona ‘umeng’oa
kifaa’ wenzako wanaweza kukuponda kuwa umependa demu asiye na hadhi
yako. Ukweli uko hivyo kwamba, kibaya kwako ni kizuri kwa mwenzio.
Nigeukie sasa kwenye kile nilichodhamiria kukizungumzia leo. Ni
kuhusu hasara ambazo mwanaume anaweza kuzipata endapo ataoa mwanamke
mzuri kwa sura na umbo, mwenye pesa lakini limbukeni.
Hapa namaanisha kwamba, wapo ambao ni wazuri, waliokwenda shule,
wenye kazi zao ila wanapoingia kwenye maisha ya ndoa, wanawaheshimu
waume zao kupita maelezo. Yaani vipato vyao, elimu na mali zao havina
thamani mbele ya mume.
Ukibahatika kuoa mwanamke wa sampuli hii utayafurahia maisha. Lakini
ukioa aliyejaaliwa vitu hivyo kisha akawa si muelewa wala hajui thamani
ya mume na ndoa, andika maumivu.
Kimsingi zipo hasara nyingi za kuoa
mwanamke mwenye pesa, mzuri kwa muonekanao, ‘aliyebukua’ sana lakini
akawa limbukeni. Leo nitagusia tatu.
Kusalitiwa hakuepukiki
Uchunguzi unaonesha kuwa, wanawake wengi
malimbukeni ambao wanajijua ni wazuri na wana pesa zao wakiudhiwa kidogo
tu ni wepesi kuchepuka hata kwa kuwashawishi wanaume wengine kwa pesa.
Utakuta mume kamkosea kidogo au kamkera bila kudhamiria lakini yeye
anaona njia sahihi ni kutorudi nyumbani. Anaweza kwenda kulala hotelini
mpaka pale mume atakapomfuata na kumpigia magoti. Wapo wanawake wa
hivyo!
Ni wepesi kuomba muachane
Ukifuatilia sana wanawake wenye vigezo hivyo wanajiamini sana, hawa
ndiyo wanaoongoza kwa kuomba talaka. Kosa dogo tu, atakuambia kama vipi
muachane.
Anasema hivyo akijua wapo wanaume wengi wanaomsumbua na hatapungikiwa
lolote. Tena hali inaweza kuwa mbaya sana kama wakati huo hamjajaaliwa
kupata mtoto kwani atajua hatakosa kitu akikuacha.
Pesa anayo, ana uhakika wa kupata mwanaume mwingine fasta, kwa hiyo anaona hana cha kupoteza au kukikosa akikutosa.
Rahisi kukutawala
Chunguza sana utabaini kuwa,
wanaume ambao wanasumbuliwa na wake zao wana vigezo hivyo. Baadhi ya
wanawake wenye pesa na wanajijua ni wazuri wanapenda sana kuonekana wao
ndiyo wenye sauti ndani ya nyumba.
Watakataa kuelekezwa wala kupewa amri na wanaume zao hata kwenye
masuala ya msingi. Hawa ndiyo wale ambao wanataka kurudi nyumbani muda
wowote wanaotaka na wasiulizwe.
Watataka wawe wenye maamuzi ya mwisho na kila jambo la kifamilia washirikishwe laa sivyo kinanuka. Hili ni tatizo!
Kimsingi ninachotaka kukifikisha kwa wanawake ni kwamba, ndoa ni
heshima. Ukijaaliwa kupata mwanaume wa kukuingiza ndani, jitahidi
kuithamini ndoa yako. Jua wapo wanawake wenye kila kitu lakini wamekosa
wanaume wa kuwaoa na wanaitamani heshima ya ndoa.
Ni hayo tu kwa leo, tukutane tena wiki ijayo kwa mada nyingine.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment